MAHUSIANO - KIJANA NA MAISHA
*** Wazee na washauri wa Vijana pia wausome ujumbe huu na kuwapelekea ***
MADA: KWA NINI VIJINA WENGI WANAANGUKIA PUA KATIKA KUOA?
Mithali 14:12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.
Mada hii imejikitita kuwashauri vijana wa KIUME ili kujiepusha na majanga ambayo wengi wanayapatia wanapoingia katika NDOA.
Kizazi chetu kinazidi kukumbwa na janga la kuvunjika kwa ndoa changa, kama sio ndoa kuvunjika, basi ni mioyo kujaa maneno ya "LAITI NINGEJUA NISINGEOA". Na wengine hawataki kusikia habari za KUOA, japo wanaishia kuwa na NDOA za masaa.
Zifuatazo ni baadhi tu ya sababu zinazojeruhi mahusiano ya vijana, hasa katika mchakato wa UCHUMBA na hatimaye NDOA.
1. Kujenga nyumba ya mahusiano katika Michanga au Matope.
Hii inajumuisha, mahusiano yoyote yanayoanzishwa bila kumhusisha Mungu, yanaanzishwa kwa tamaa za macho, na kuwa chini ya adui, roho ya ulimwengu huu. Ni wepesi wa Kusikia neno la Mungu, kulitamka kwa nyimbo na maombi, lakini mioyo yao kwa hila imetekwa.
Neno la Mungu linasema "...Mke mwenye Busara, mtu hupewa na BWANA" Mithali 19:14, "Bwana asipoijenga nyumba, waijengao wafanya kazi bure ..." Zaburi 127:1. Kijana! Utawezaji kuzuia mafuriko na dhoruba zisibomoe nyumba yako uliyoijenga kwenye tope au mchanga? Huko ni sawa na kujilisha UPEPO.
2. Hawana elimu ya kutosha juu ya kujitambua katika eneo hili ya mahusiani ya Uchumba na ndoa.
Kutangaza kuwa amepata mchumba siku ya kwanza alipomwambia binti NAKUPENDA na kumjibu NAMI NAKUPENDA utafikiri ulijua! Kabla hata ya kufahamiana kwa undani. Hawajui tofauti kati ya urafiki na uchumba. Hivyo utakuta Kijana ana Wachumba zaidi ya mmoja au wengi, wote akiwa amewalengeshea.
Nilishafundisha kwa undani juu ya jambo hili, unaweza kuwa na marafiki wengi, ambao mwisho unapata mchumba mmoja ... huyo ndiye unamtamkia kuwa unata awe Mchumba wako. Hatua ya uchumba sio ya kuchunguzana.
Urafiki ni uwanja wa wazi kwa ajili ya kufahamiana kwa undani bila mkataba wowote wa kuoana. Vijana wengi wanatumia Kick ya uchumba ili ampate binti, hilo ni KOSA kubwa, anzisha mazoea ya kawaida na urafiki wa kawaida kwa ajili ya kupata ufahamu wa ndani juu ya maisha yao.
3. Tatizo lingine kubwa zaidi ni kuchanganya mambo haya mawili. Kukidhi tamaa za mwili na kutafuta mchumba mwaminifu. Anatamani Mungu ampatie MKE MWEMA, wakati huohuo amejisalimisha na amekuwa mtumwa wa roho za NGONO.
Watu hao ni rahisi kumuomba Ngono binti ambaye alishamuomba urafiki, akisisitiza kuwa, Ngono ndiyo ishara ya binti kuonyesha ukubali, HII NDIYO KONA AMBAYO WENGI WAMEJERUHIWA NA ADUI.
Sikilizeni; tendo lolote la zinaa au uashertani, ngono nje ya Ndoa HALALI, ni mshale urukao mchana na Kujeruhi. Pasipo Mungu pana upendo bandia, wa kukidhi tamaa ya mwili, kama ilivyokuwa kwa Amnoni na Tamari.
Mara nyingi mabinti waaminifu, wanaokataa kutoa ngono kwa vijana marafiki au wachumba wao, wanaachwa eti kwa sababu wanaonekana kutowajali, hivyo vijana wanaruka kama ndege kwenda kutua matawi mengine yoyote na kujenga viota.
VIJANA WANGU, Huko ni kuchanganyikiwa, hayo ni mapepo na roho za mashetani, mwisho wake ni mauti, badala ya kufurahi kumpata Binti mweye hofu ya Mungu, anayefaa kwa ajiri ya Ndoa, wewe unatafuta maloli ya jeshi, ambayo muda wote yamebeba mizigo.
4. Mambo mengine ni pesa ... vijana wengi siku hizi wanatafuta wanawake wenye PESA, huo ni ujinga, nani amekwambia pesa zinajenga NDOA? Hata hivyo wewe Mwanaume, ndiye Kichwa cha nyumba, mwanamke ni msaidizi, inakuwaje mnapoteza mwelekeo na kutafuta kuwa tegemezi?
Ukimpenda mwanamke kwa pesa yake uwe tayari kumpenda anayemuwezesha, kuna wengine wanaona binti anapendeza ana pesa bila kujua pesa anazitoa wapi. Usipende MALI itakujeruhi, wewe ni mwanaume omba Mungu atakusaidia, kubali muanze maisha na hali yoyote, Mungu amesema, ataibariki nyumba ya wenye haki.
Baadhi ya matokeo ya tabia hizo za vijana kutojitambua ni hizi:
1. Wengi wameangukia PUA kuoa wasiowatarajia, kwa kutanguliza ngono, wengi wanalazimika kuoa mabinti wajanja wanaotegeshea mimba, wanaona aibu kumtelekeza binti na mtoto.
2. Mabinti wengi wanawanasa vijana WAPIMA OIL, kwa madawa ya Kishirikina, utashangaa kijana hajielewi, anamwacha binti mcha Mungu, Bikra safi, anaenda kujiegesha katika tundu bovu.
Ndoa yoyote ikianzishwa na mivuto ya kishirikiana au mivuto yoyote ya kidunia, hilo ni tundu bovu, ibirisi ndiye mshika usukani wa mahusiano yenu. Ushirikina na Maluweluwe ya mizimu, ni nyumbani pake.
3. Vilio vya mabinti mnaowaharibu kwa hila, na baadaye kuwapiga VIBUTI, huku mkiwa mmewapotezea muda, na kuwatia hasara, Mungu anavisikia vilio vyao na masononeko yao, Mungu anawalipia visasi, majuto yao yanageuka baadaye kuwa yenu.
Mnacho watendea mabinti leo, ndicho kitakachowatokea maisheni mwenu katika ndoa. Wengi wanajiuliza na kutafuta nani analoga ndoa zao, ni vurugu tu utafikiri kuna PEPO, kumbe ni laana za vilio vya mabinti waliowatelekeza zinawafuata.
USHAURI:
Wote walio na marafiki ambao mumewatangazia au mumeonyesha kuwaoa, wakati hamjafanya maamuzi juu yao, waambieni UKWELI kuwa hamjafanya maamuzi hayo ili wasiweke tumaini, na lisijekuwa tanzi yenu baadaye.
Ombeni rehema za Mungu, mkitubu kwa yaliyopita na kusahihisha yanayoendelea. Yeye ni mwaminifu atawashindia.
MWISHO:
Iweni wakweli, Iweni waaminifu, Mtegemeeni Mungu naye atawajazi haja zenu juu ya kupata wenzi BORA wa Maisha sio BORA wenzi.
NAWATAKIA VIJANA WOTE MAFANIKIO NA BARAKA TELE
Nawakaribisha kwa maswali na ushauri ... kwa inbox.
Na. Ev. Eliezer Mwangosi
Simu:
+255 0767 210 299.
UKIPATA UJUMBE HUU, MPELEKEE PIA MWENZAKO.