MAMBO 7
UNAYOHITAJI KUYAJUA JUU YA MPANGO WA MUNGU ALIONAO
KWA AJILI YA MAISHA
YAKO
Utangulizi:
“Mwaka 1986 nilipata msukumo ndani
yangu mkubwa sana wa kutaka kumtumikia Mungu. Wakati huo nilikuwa nafikiri
ukitaka kumtumikia Mungu ni lazima uwe mchungaji. Kwa hiyo nikaamua kutafuta
chuo cha Biblia ili nipate kusomea uchungaji. Nikapata chuo cha Biblia cha
kusomea uchungaji, na nikapata pia mtu aliyekuwa tayari kunisomesha mpaka niweze
kuhitimu. Lakini siku moja mchana Roho Mtakatifu alisema nami wazi wazi moyoni
mwangu ya kuwa sijaitwa kuwa mchungaji kwa hiyo nisiende kusomea
uchungaji.
Ikabidi niwaombe radhi wale
waliokuwa tayari kunisaidia kusomea uchungaji ya kuwa nilikuwa hapo mwanzoni
sijasikia sauti ya Mungu vizuri. Na kwamba sitaweza kwenda tena kusomea
uchungaji, maana Roho Mtakatifu ameniambia sijaitwa kufanya huduma
hiyo.
Karibu kipindi hicho hicho
nilipata kitabu cha mhubiri mmoja wa Marekani ambaye alieleza juu ya wito wake
ulivyo, na kile ambacho Yesu alisema naye. Anasema alifanya kazi ya uchungaji
miaka 12 lakini hakuwa na amani ndani yake, ingawa kazi ya Mungu ilikuwa
inaendelea vizuri, watu walikuwa wanaokoka, wanapona magonjwa yao, na pia
kujazwa Roho Mtakatifu.
Pamoja na mafanikio hayo bado
ndani yake hakuwa na amani. Anasema moyoni mwake alikuwa anajisika kama vile mtu
ajisikiavyo anaponawa miguu yake huku amevaa soksi! Kuona hivyo akaamua kuacha
kufanya kazi ya kichungaji; na akaanza kufundisha semina mbalimbali za neno la
Mungu. Ndani ya moyo wake akapata amani ambayo alikuwa hajawahi kuipata katika
muda wote ule wa miaka 12 aliyohudumu kama mchungaji. Pia, wakati huo Yesu
akamtokea katika maono na akamwambia ya kuwa alipoanza kufundisha ndipo
alipoanza awamu ya kwanza ya huduma aliyoitiwa! Na kwamba miaka 12 ya uchungaji
haikuhesabiwa, kwa sababu huo haukuwa wito wake! Yule mhubiri alishangaa sana na
akamuuliza Yesu ni kwa nini basi alikuwa anambariki katika huo uchungaji? Yesu
akamwambia alikuwa hambariki yeye kama mhubiri, bali alikuwa anabariki neno la
Mungu alilokuwa analihubiri!
Nilipotafakari ushuhuda huu wa mhubiri wa Marekani; na pia nilipokumbuka
nilivyozuiwa kwenda kusomea uchungaji; nilijikuta nimeingia katika maombi mazito
na ya muda mrefu nikitaka nijue wito wangu toka kwa Mungu.
Nikiwa naendelea na maombi hayo nikaongozwa kusoma mstari huu wa Yeremia 29:11
unaosema “ Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo
ya amani, wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho?”
Niliposoma mstari huu kwenye tafsiri mojawapo ya kiingereza niliona
ikisema “ Maana najua mipango niliyowapangia ninyi, asema Bwana, ni mipango
ya kuwapa mafanikio, wala si ya kuwafanya msifanikiwe, ili niwape maisha mazuri
ya baadaye…..”
Ndani ya mstari huu, Mungu alituongoza mimi na mke wangu kujua wito tulioitiwa
na kuanza kutembea katika mpango aliotupangia katika maisha yetu
pamoja.
Katika barua hii fupi tunataka tukushirikishe mambo 7 muhimu ambayo unapaswa
kuyajua juu ya mpango wa Mungu alionao kwa ajili ya maisha yako. Kutokana na
mambo haya saba yanazaliwa mambo mengi yaliyo muhimu sana kwa kila mtu kuyajua
kufuatana na mpango ambao amepangiwa. Sisi tunayaweka mambo haya kwa muhtasari
tu, lakini tunaamini Roho Mtakatifu atakufunulia na kukufundisha mengi
zaidi.
Jambo
la Kwanza:
Lijue kwanza kusudi la Mungu juu ya maisha yako, kabla ya kuujua mpango wa
Mungu juu yako! Kwa sababu mpango upo tu kwa ajili ya kutekeleza hatua na
njia ya kuhakikisha ya kuwa kilichokusudiwa kimefikiwa. Bila kulijua kusudi,
mpango wa utekelezaji unakosa msukumo na unakosa mwelekeo! Bila kulijua
kusudi la Mungu kukuweka duniani wakati huu, mpango wo wote unaotekeleza ili
kufanikisha maisha yako, unakosa msukumo na unakosa mwelekeo. Matokeo yake ni
mipango yako kutofanikiwa, na ikifanikiwa mafanikio hayo yanakuwa ni ya muda
mfupi tu.
Imeandikwa katika Mithali 19:21 “Mna hila nyingi (au mipango mingi) moyoni
mwa mtu; lakini shauri (au kusudi) la Bwana ndilo litakalosimama (au ndilo
litakalofanikiwa)”. Pia, ukisoma katika kitabu cha Isaya 46:10 Mungu
anasema; “ Nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo
yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri (au kusudi) langu litasimama (au
litafanikiwa), nami nitatenda mapenzi yangu yote”.
Kwa kutafakari mistari hii utajua ya kuwa: kusudi la Mungu halibadiliki na
limewekwa ili kufanikiwa na kumfanikisha kila mtu anayelitekeleza. Mipango ya
kutekeleza kusudi inaweza kubadilika, lakini kusudi lenyewe la Mungu huwezi
kulibadilisha.
Kwa mfano, kusudi la Mungu mojawapo lilikuwa ni kuwa na wanadamu wenye sura
yake. Mpango wa kuwapata ilikuwa ni kwa njia ya ndoa. Lakini dhambi ilipoingia,
Mungu akabadilisha mpango, na kuamua kutumia njia ya kuhubiri neno ili watu
wazaliwe mara ya pili, ili kusudi lake la kuwa na wanadamu wenye sura yake
lipate kutimia!
Mfano mwingine, ni wa kusudi la Mungu la kuwafikisha nchi ya Kaanani, wana wa
Israeli baada ya kuwatoa Misri. Mpango wa Mungu ilikuwa ni kumtumia nabii Musa
lakini Musa hakuweza na badala yake Mungu akamwinua Yoshua ili kumalizia
utekelezaji wa mpango huu!
Fahamu hili; wewe ni sehemu ya mpango wa Mungu katika kutekeleza kusudi lake
alilonalo. Ukivuruga maisha yako, na usipotaka kutubu; na hata kama ukitubu
lakini usifuate mpango wa Mungu, kuna uwezekano mkubwa wa Mungu kuinua mtu
mwingine ili atekeleze hilo Mungu analotaka! Kwa Kiingereza chepesi tunaweza
kusema: A plan of God is a set of coordinated steps which are implementable
within a specified time in order to accomplish an identified purpose of
God. Na neno hili Purpose of God lina maana ya: God’s motivation
behind a vision you pursue; A reason God has in creating a thing or a person, An
end result God expects out of a particular plan; A destination God wants you to
reach on your journey He has led you to take.
Kiswahili chepesi cha neno kusudi kinachotumika na wengi ni Neno ‘Lengo.’ Kusudi
au lengo la watu wengi linalowafanya wafanye biashara ni ili kupata utajiri.
Lakini kibiblia utajiri siyo mwisho wa safari bali ni sehemu ya mpango wa Mungu
wa kuimarisha utekelezaji wa agano lake duniani. Hii ni kufuatana na mstari wa
Kumbukumbu ya Torati 1:18.
Jambo
la Pili:
Mpango wa Mungu juu yako si wa kuutafuta; upo tayari maana uliandaliwa kabla
hujazaliwa! Ile tu kwamba umezaliwa na unaishi, ina maana kuna mpango ambao
Mungu ameuandaa unaohitaji mtu kama wewe kuutekeleza – kiumbo, kimwili, kiakili
na kiroho! Wazo hili tumelipata kutokana na kusoma mistari hii ya Waefeso 1: 3-
5, na Waefeso 2:10.
Kwa hiyo ni muhimu sana ujizoeze kumwomba Mungu akuwezeshe kujua jinsi
anavyosema na watu wake; lakini pia akupe hekima na ufunuo wa kutafsiri na
kuelewa anachokuambia. Pia usisahau kuomba Neema ya kukitekeleza.
Kama umesoma vizuri na kulielewa jambo la kwanza tulilokuambia juu ya kulijua
kusudi la Mungu kabla ya mpango wake; utakuwa umejua ya kuwa kusudi ni kubwa
ki-umuhimu kuliko mpango. Ndiyo maana Mungu hawezi kubadilisha kusudi lake ili
kukidhi mipango yetu ya kibinadamu.
Tena utakuwa umepata picha moyoni mwako ya kuwa wewe ni sehemu tu ya watu wengi
ambao Mungu anao na amewaweka ili kuhakikisha mipango Yake inafanikiwa ili
kusudi lake alilolikusudia lisimame.
We are not designed to work alone or implement His plans alone!
Hatukuumbwa ili tufanye kazi peke yetu, au hatukuumbwa ili tutekeleze mipango ya
Mungu peke yetu. Kufanikiwa kwa mtu mmoja kunategemea mafanikio ya mtu mwingine.
Mnayeshirikiana naye akifanikiwa na wewe pia unafanikiwa! Au kama unashirikiana
na mashine au chombo Fulani – kufanikiwa kwako kunategemea pia mafanikio ya
utendaji wa mashine hiyo au chombo hicho.
Jambo
la Tatu:
Mungu ametenga muda maalumu wa kutekeleza kusudi lake na mipango yake! Maana katika
Mhubiri 3:1,17 tunasoma ya kuwa , “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati
kwa kila kusudi chini ya mbingu ….. Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu
wenye haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila
kazi”.
Tunataka ujue ya kuwa mipango ya leo inaweza isifae kesho. Kilichofanikiwa mwaka
uliopita kinaweza kisifanikiwe kikitekelezwa mwaka huu. Lazima kujifunza kwenda
na wakati wa Mungu na kujua tunachojua kukifanya ndani yake.
Kufuatana na kitabu cha 1 Mambo ya Nyakati 12:32, wana wa Israeli walijua siri
hii wakati Daudi akiwa mfalme wao. Na hii ni kwa sababu Mfalme Daudi alikuwa
analitumikia kusudi la Mungu na wala si kusudi lake mwenyewe wala la wana wa
Israeli (Matendo ya Mitume 13:36)
Umuhimu wa kujua nyakati za Mungu tunauona pia tunaposoma katika Matendo ya
Mitume 17:26 na kuelewa ya kuwa kabla mwanadamu hajaumbwa, Mungu aliweka kwanza
nyakati kwa ajili ya utekelezaji wa kusudi na mipango Yake akimtumia mwanadamu
huyo.
Jambo
la Nne:
Mungu anapoweka wazo ndani yako juu ya mpango wake anaotaka uutekeleze, ujue
basi katika mawazo ya Mungu mpango huo tayari umekwishatekelezwa na
kumalizika.
Kwa mfano; mara kwa mara tunawaambia wenzetu waliomo katika kamati za semina
tunazoandaa sehemu mbali mbali ya kuwa – katika mawazo ya Mungu semina hizi
tayari zimekwisha fanyika na Mungu ameona matokeo yake.
Watu wengine wakitusikia tukisema namna hii huwa hawatuelewi. Lakini sisi
tunaamini kabisa ya kuwa pale Mungu anapotupa wazo la kuifanya semina mahali
Fulani, kwake Mungu semina hiyo ameitekeleza na kufika mwisho, na ndipo
anapotuambia.
Kazi yetu inabaki kuomba Mungu atuwezeshe kuyajua na kuyatekeleza anayotaka
tuyafanye, ili kusudi la kuwepo semina hiyo lifikiwe. Ndiyo maana katika Isaya
46:10 Mungu anasema; “nitangazaye mwisho tangu mwanzo, ….. mambo
yasiyotendeka bado; nikisema, shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi
yangu yote”.
Kwa hiyo basi ina maana Mungu anatangaza mambo yasiyotendeka bado jambo hilo
likiwa ndiyo linaanza tu! Pia, hawezi akautangaza mwisho wa jambo likiwa ndiyo
tu linaanza kama hajauona huo mwisho wake utakavyokuwa! Na kama anaujua mwisho
wake, jambo likiwa tu ndiyo linaanza,ina maana hatua zilizopo kati ya mwisho na
mwanzo unazotakiwa kuzifanya anazijua na yuko tayari kukuongoza ili uweze
kulifikisha jambo hilo katika mwisho wake mzuri uliokusudiwa na
Mungu.
Ndiyo maana katika Yeremia 29:11 anasema; “ Maana nayajua, mawazo
ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani, wala si ya mabaya, kuwapa
ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.
Tulipojua hili, ndani ya mioyo yetu tulipata utulivu mkubwa sana wa kuwa na
uhakika wa kuwa Mungu anaweza kutuongoza katika mipango anayotupa, kwa mfanikio
toka mwanzo hadi mwisho wa mipango hiyo. Tunataka na wewe ujue hili ya kuwa
Mungu hawezi kukupa jambo la kufanya ambalo hajui mwisho wake utakuwaje! Ukijua
hili litakusukuma kuwa karibu na Mungu ili umjue zaidi kwa namna ambavyo akikupa
mpango wa kuutekeleza, atakuongoza pia katika utekelezaji wake hatua kwa hatua
hadi ufike katika mwisho ule ambao ulikusudiwa.
Jambo
la Tano:
Upo upako wa Roho Mtakatifu wa kukusaidia kuanza mpango ambao Mungu amekupa
uutekeleze, na ule wa kukusaidia uweze kuumalizia huo mpango
vizuri.
Upako ni uwezo wa Mungu au nguvu za Mungu ndani ya Roho Mtakatifu ili kutusaidia
kuyatimiza makusudi ya Mungu katika maisha yetu.
Ndiyo maana Yesu Kristo anamwita Roho Mtakatifu ya kuwa ni “msaidizi”.
Soma Yohana 14:16,17, 26 na Yohana 16:7 -15. Kumbuka msaada unapelekwa pale
panapohitaji msaada. Roho Mtakatifu hawezi kukulazimisha kukupa msaada usioutaka
– labda mtu mwingine amwombe Mungu kwa ajili yako.
Yesu Kristo maana yake Yesu ‘mpakwa mafuta’. Kwa kuwa neno ‘Kristo’ maana yake
ni ‘masihi’ au ‘mpakwa mafuta’. Kwa hiyo anapojiita Yeye ni Alfa na Omega
(Ufunuo wa Yohana 1:8), ana maana ndani yake unapatikana upako wa kuanzia (Upako
wa Alfa), na pia ano upako wa kutusaidia kumalizia jambo vizuri hadi mwisho
(Upako wa Omega).
Ndiyo maana biblia inamtaja Yesu kama mwanzilishi (Alfa) na mkamilishaji (Omega)
wa imani yetu! (Waebrania 12:2). Kwa hiyo kama una jambo ambalo Mungu ameliweka
ndani yako na hujui namna ya kuanza kulitekeleza, basi ni vizuri umwombe Mungu
akupe upako wa Alfa ili ukusaidie kuanza. Na kama umeanza kulifanya jambo
alilokupa Mungu kufanya, lakini hujui namna ya kumalizia, basi ni vizuri umwombe
akupe upako wa Omega ili akusaidie namna ya kulimazia jambo hilo
vizuri.
Jambo
la Sita:
Uwe mwangalifu sana na uhusiano unaokuwa nao na
watu mbalimbali; - maana unaweza kukwamisha au kufanikisha mpango wa Mungu juu
yako!
Tunaamini unakumbuka jinsi ambavyo Mtume Petro alimkataza Yesu huku akimkemea
baada ya Kristo kuelezea mpango wa Mungu juu yake wa kwenda Yerusalemu
kusulubiwa. Yesu na Petro walikuwa marafiki, lakini shetani alimtumia Petro ili
amkatishe tamaa asiendelee na mpango wa kwenda Yerusalemu kusulubiwa. Yesu
akamkemea Petro akisema; “ Nenda nyuma yangu, shetani; u kikwazo kwangu;
maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”.
Hata ikiwa mbele yako kuna mapambano na majaribu ya namna gani, unahitaji
marafiki wanaokutia moyo kusonga mbele, na si rafiki anayekutia moyo ili urudi
nyuma na kuuacha mpango wa Mungu.
Ukisoma Kutoka 32:1-8, 21-26 utaona jinsi ambavyo Haruni alivyoshindwa
kuwasaidia wana wa Israeli walipokuwa wamechoka na kukata tamaa katika kumsubiri
Musa atoke mlimani alikokwenda kuongea na Mungu. Kufuatana na Yoshua 1:6 na
2Mambo ya Nyakati 20:20 kuna watumishi ambao ndani yao ameweka neno kwa ajili
yako ili likusaidie ufanikiwe.
Kwa hiyo uwe mwangalifu ndani ya moyo wako ili ujue unampa nafasi mtumishi wa
Mungu wa namna gani na nafasi ya namna gani. Soma 2 Wakorintho 7:2! Je! Ushauri
anaokupa unakukwamisha zaidi au unakufanikisha? Je! ushauri anaokupa unakufanya
uwe huru zaidi ndani ya Kristo au unajikuta unapoteza uhuru wako? Je! akikukuta
umekwama kwenye dhambi au kwenye majaribu anakupa neno la namna gani? – je,
linakusaidia utoke katika hali hizo na ushindi wa Yesu au neno hilo analokupa
linakufanya ujihukumu na kujilaumu zaidi?
Jambo
la Saba:
Mpe Mungu utukufu na kumrudishia sifa anazostahili kwa Mungu kukutumia na
ukafanikiwa katika kutekeleza mpango wake juu ya maisha yako!
Ukifanya hili siku zote itakuwa ishara toka kwako ya kuonyesha ya kuwa
umefanikiwa si kwa uwezo wala nguvu zako bali kwa Roho wa Mungu. Hili ndilo wazo
la Zekaria 4:6.
Lakini pia ukiwa na nia na moyo huu ndani yako Yesu Kristo atainuliwa katika
mipango yako; na itakuwa rahisi watu wanaokuzunguka kumwona Mungu katika maisha
yako. Yesu alisema; “ Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote
kwangu” (Yohana 12:32).
Je! mipango unayofanya ambayo unasema Mungu amekuongoza kuifanya, huwa inampa
Mungu utukufu kwa kiasi gani? Je! umewahi kulifikiria hili? Ni muhimu kufikiria
hili kila wakati maana imeandikwa: “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo,
fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Baba kwa yeye”
(Wakolosai 3:17) “…… mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa
Mungu” (1 Wakorintho 10:31)
Tuzidi kuombeana!
Ni sisi katika utumishi wa Kristo,
Christopher na Diana Mwakasege