‘Lakini saa inakuja, nayo saa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli.Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.Mungu ni Roho nao mwabuduo yeye imewapasa Kumwabudu katika roho na kweli’ Yohana4:23-24
Makusudi ya injili ya Yohana ni ili tupate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kuamini tuwe na Uzima kwa jina lake (Yohana20:31)
Katika mazungumzo yake Yesu alimwambia mwanamke Msamaria amsaidiki yeye na kwamba saa inakuja nayo saa ipo ambayo watu hawatamwabudu Baba (Mungu) katika Mlima wala kule Yerusalemu bali watamwabudu katika roho na kweli kwa kuwa yeye ni Roho.
Kuabudu ni kuonyesha thamani, heshima,upendo,utii,shukrani,sifa,kuomba,kubariki,kuonyesha furaha na unyenyekevu na moyo wa kupondeka katika kumtumikia na kutambua ukuu wa Mungu wetu.Tunamwabudu Mungu kwa sababu yeye ni Muumbaji wa vitu vyote, ni Mkuu, kazi zake ni za kushangaza, ni Mungu wetu aliye hai na aliyeumba vitu vyote. Na imeandikwa tumsujudie Bwana Mungu wetu na tumwabudu yeye peke yake (Luka4:8). Asili ya kumwabudu Mungu inataka tumsujudie kwa roho zetu na kweli mbele yake katika hali ya unyenyekevu na kupondeka na yeye aweze
kutunyanyua.Biblia inasema katika Yakobo4:10 ‘Mujinyenyekeze mbele ya BWANA naye atawanyanyua ninyi’.
Mungu ni Roho
Mungu ni Roho yaani, Mungu, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Mungu ni Roho, na si mwili yeye hana mwanzo wala mwisho. Tunapokea Roho wa Mungu ndani ya roho zetu wakati tunapo amini Yesu Kristo na kuzaliwa upya katika roho zetu kwa maji na kwa Roho (Yohana3:6 – Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili na kilichozaliwa kwa Roho ni roho).Roho Mtakatifu hufanya kazi ya kuwasiliana kati ya roho zetu na Mungu.Mungu hutupa pumzi ya uzima katika roho zetu na pia akili zetu hutokana na pumzi ya Mungu (Ayubu32:8-pia imo roho ndani ya mwanadamu na pumzi ya Mwenyezi Mungu huwapa akili). Pia sisi hatukuipokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu (1Korintho2:12)
Kumwabudu Mungu katika Roho
Mungu ametufunulia sisi wakristo kwa Roho ili tumwabudu kutoka ndani ya roho zetu, akili zetu, nguvu zetu.Katika Waefeso Efeso1:17 inasema ‘Mungu ametupa roho ya hekima ya ufunuo katika kumjua yeye’ na pia Roho ndiye ashuhundiaye kwamba tunamtumikia Mungu katika kweli yake kwa sababu Roho ndiye kweli(1Yoh5:7).
Kuabudu kwa Roho ni lazima roho zetu na mawazo yetu, tabia na matendo yetu yabadilishwe na tuweze kumpa sifa, heshima,utukufu,kumshukuru,kuomba,kuhubiri, kutoa, na mambo yote yanayohusu kujitoa kwa ajili ya kazi ya Mungu wetu. Lengo la kumwabudu Mungu ni kuonyesha ukuu wake Mungu na tunavyo mthamini katika maisha yetu. Kuabudu kwetu lazima kuonyesha uaminifu wetu kwa Mungu kwa sababu ya neema yake katika kumtoa Mwanae Yesu Kristo ili awe Mwokozi wa maisha yetu.
Watu wengi hukosa lengo linapokuja suala la kuabudu Mungu.Mara nyingi tumechoshwa na ibada zetu za kanisani siku ya jumpili, katikati ya wiki, nyumbani, kazini, safarini, shambani, kwenye biashara na sehemu zote ambazo tunaweza kuwa tunafanya shughuli zetu za kila siku.Wakati mwingine tumechoka kuwahi kufika kwenye ibada zetu na pia kuna wakati wa kuimba nyimbo za kusifu au kuabudu tunarudia maneno bila kujua maana. Hii yote ni kwasababu roho zinakuwa hazijatawaliwa na Roho wa Mungu.Tunapomwabudu katika Roho tunaonyesha kuwa roho zetu zinamekubali kuzaliwa upya.Neno la Mungu linasema katika Wafilipi 3:3 ‘ Maana sisi tu tohara tumwabuduo Mungu kwa Roho na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili’.
Tunapozaliwa mara ya pili Mungu ambaye ni Roho hutufanya tuwe hekalu lake.Na kwa kuwa sisi tumekuwa hekalu la Mungu na Roho wa Mungu hukaa ndani yetu (1Korintho3:16), ni lazima roho zetu zimsifu na kumtukuza Mungu kwa roho ya upendo, furaha, uaminifu. Mungu ni mmoja ambaye ana hatima yetu ya maisha yetu katika mikono yake. Wafilipi 2:12 inatuambia, ‘utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.’ Wokovu wetu ni jambo kubwa sana na wala halikutokea kwa bahati mbaya. Lazima tuheshimu Mungu kwa kuogopa na kutetemeka
ndani ya roho zetu tunapomwabudu na kumtumikia. Wokovu wetu unategemea juu ya kama ibada zetu ni za kumpendeza Mungu au la.
Kumwabudu Mungu katika Kweli
Lazima tumwabudu Mungu katika kweli. Neno ni Mungu na neno lake ni kweli. Wakristo ni lazima kumwabudu kulingana na neno lake. Hapa Bwana anatueleza kuwa lazima neno lake tulijue ili lituweke huru na litutakase maisha yetu ya kiroho na kimwili tuwe safi. Kuabudu katika kweli ni kuamini neno la Mungu na kuwa huru kifira kwa kuondoa maneno yote yasiyo mpendeza Mungu.
Tumwabudu kwa kujitoa mioyo, roho na nguzu zetu kwake huku tukiwa tumetakaswa na Neno lake kwa sababu ya ile kweli tuliyokwisha kuipokea. Tunapolishika neno la Mungu linatutakasa na kutufanya tuwe safi na hapo ndipo tunaweza kumwabudu Mungu tukiwa wasafi maana yeye ni Mtakatifu. Neno la Mungu linasema katika Yoh17:17‘Uwatakase kwa ile kweli neno
lako ndiyo kweli’. Pia neno la Mungu tunapolishika linatufanya tuifahamu kweli yake (Yohana8:32 – Tena mtaifahamu kweli nayo kweli itawaweka huru).
Kwa kuamini injili ya wokovu katika Kristo ambaye yeye ni kweli, hema ya Mungu, tunapata kuishi na Kristo ndani yetu ambaye yeye ni Mungu. Kwahiyo ni lazima tunapoabudu Mungu tuwe wa kweli katika njia zetu na wakamilifu wa nafsi kwa kujitakasa katika neno lake.Tukishika neno la Mungu litatuweka huru na kuwa mbali na dhambi.
Mungu anaona uzuri wa kuabudiwa katika namna ile, ‘kwa roho na kweli’ ndiyo maana anasema anawatafuta wanaomwabudu katika roho na kweli. Hasemi tunaweza kumwabudu Mungu kwa namna tunayotaka sisi.
Adui wa mkristo katika kuabudu Mungu
1.Shetani- Shetani ni adui yetu mkubwa na hupenda kuona watu wa dunia hii wa kimtukuza yeye kwa kuwajaribu na fahari za dunia hii na kukamata muda wao ili waone mahitaji ya mwili ni muhimu sana kuliko kumtumikia Mungu wa kweli.Tunaona namna shetani alipomjaribu Yesu kwa kumpandisha juu na kumwonyesha miliki zote za dunia na atampa zote ikiwa atamsujudia (Luka4:6-7- Ibilisi akamwambia Nitakupa wewe Enzi hii yote na fahari yake kwa kuwa imo mikonani mwangu nami humpa ye yote kama nipendavyo.Basi wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako)
2. Mwili - Mara nyingi mwili hupingana na roho kwa kuleta vishawishi vya kufanya lile ambalo hupendi kulitenda.Ndiyo maana utakuta wakristo wengi siyo watendaji wa Neno.Mtume Paulo alilia kwa sababu ya mwili wa mauti(Roma7:18 Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani ndani ya mwili wangu, halikai neno jema, kwa kuwa kutaka nataka bali kutenda lililo jema sipati)
3.Kujivuna - Watu wengi wamejaa majivuno,viburi na njia mbovu kiasi kwamba hawana muda na hawezi kuona thamani ya kujitoa kwa Mungu aliyewaumba katika kumwabudu kwa unyenyekevu.Mungu anachukia kiburi,majivuno,uovu,kinywa cha ukaidi pia anakichukia(Mithali8:13)
4. Mapokeo- Kuna wakristo wengi wanendelea kuabudu mapokeo ya dini na wanashindwa kuabudu Mungu katika njia ya kweli kwa sababu ya upofu wao katika kuijua Habari Njema (1Korintho2:14)
Mungu anapenda tumwabudu katika roho na kweli namna ambayo yamfaa Mungu.Maisha yetu yaonyeshe kwa mataifa kuwa tunamtegemea Mungu na kuweka imani ndani yake-kwamba yeye amefanya kila lililopendeza duniani na mbinguni, na yeye ndiye anayestahili kuheshimiwa.Yeye ndiye nguvu yetu na msaada wetu katika maisha yetu.Tusiabudu watu,kazi,mali,dhehebu,siku,sikukuu,sanamu au chochote kile bali tumwabudu Mungu katika roho na kweli ambayo ni njia pekee tunayoweza kumpendeza Mungu wetu katika maisha yetu ya sasa na mwisho wake tupate uzima wa milele.
Nawapenda wale wanipendao,Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona Mitahli8:17