Yohana 15:5 "Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote."
Ni jambo la kawaida kuwasikia watu wakikiri kuwa, haiwezekani mtu kushinda dhambi, na imefikia hata baadhi ya wahubiri nao utawasikia wakisema; sio rahisi mtu ashinde dhambi kabisa, na kwa mawazo na maneno hayo wengi wanaendelea kuishi maisha ya ukinyonga.
Utasikia mtu anasema, hii ni tabia yangu nimezaliwa nayo sio rahisi kuishinda, au yule ameshindikana ni tabia yake, hadi imefikia siku hizi mashoga na wasagaji wanadai ni maumbile hawawezi kujizuia. Kizazi hiki kimefikia kuhalalisha dhambi za Uongo, Masengenyo, Wivu, Fitina, Hila n.k. Kuwa ni hulka za watu ambazo sio rahisi kuziacha.
Asilimia kubwa ya vijana hasa wa kiume wanaamini kabisa haiwezekani kuishinda tamaa ya Ngono, na shetani anawaongoza kuamini kuwa hakuna aliyewahi kushinda, hivyo huishia maisha ya zinaa na huku wakidumu kufanya usanii katika mambo ya Imani, mwisho wanaishia kurushiwa mishale na kujeruhiwa na ADUI.
Rafiki; mawazo yako ni sahihi, mwanadamu kwa kuzaliwa hawezi kuishinda dhambi wala kufanya jema lolote mbele za Mungu, ndio maana Yesu alisema, ni wale tu waliounganishwa naye kama TAWI na SHINA ndio wanaoweza kuzaa matunda, yaani kutenda yampendezayo Mungu.
ZINGATIA: Maisha ya kukubaliana na dhambi ya aina yoyote ni udhihirisho wa kutounganishwa na Yesu Kristo, hilo ni tawi lililokatwa, limenyauka, haliwezi kamwe kuzaa matunda. Hata hivyo bado lipo tumaini, kama una hali hiyo, fanya uamuzi wa kujisalimisha kwa Yesu Kristo leo ili AKUSHINDIE, NI HAKIKA PEKE YAKO HUWEZI.
Je una changamoto iliyokuzidi? Je unapitia dhoruba na huoni jinsi ya kuivuka? Ni maumivu gani unayapitia? NI HAKIKA PEKE YAKO HUWEZI, Mwambie Yesu atakushindia.
MUNGU AWAPATIE SIKU NJEMA YENYE MAFANIKIO TELE.
Na: Ev. Eliezer Mwangosi.