NENO LA LEO - KUJILISHA UPEPO.
Muhubiri
2:11 "Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua."
Nakumbuka kisa cha Baba mmoja tajiri, aliyekuwa na uwezo wa kufanya lolote kwa sababu ya mali alizokuwa nazo. Alikuwa akiambiwa habari za Mungu, anasema "Mungu anatafutwa na maskini na wazee, umesikia wapi matajiri wanahangaika na Mungu, ili viweje?".
Katika wakati asioudhania, akaugua ugonjwa ambao tiba yake ilikuwa ni pamoja na mashariti haya; asile chakula kilichoungwa chumvi, asile vyakula vya nyama, chakula kisipikwe kwa mafuta, asitumie sukari wala aina yoyote ya soda au juice za viwandani, asitumie kileo cha aina yoyote n.k. Siku moja akiwa kitandani hajiwezi alisikika akisema "KWELI MAISHA NI UPEPO".
Rafiki sikiliza, kuna watu ni matajiri, lakini wanaziangalia mali zao kwa macho, wanafaidi wengine. Elimu, uzuri, mali, vyeo, vipaji, bila Mungu ni kujilisha Upepo, dunia inapita tena haraka, hakuna anayejua mwisho wake ila ni Mungu pekee anayejua.
Kuna watu wananyanyua mabega na kunyanyasa wenzao kwa sababu tu ya nafasi au maisha na mali walizo nazo, lakini jiulize wanamzidi Sulemani hata kwa lolote? Mwingine utakuta ana mke mmoja, nyumba ndogo mbili na makahaba hawazidi 10, anajiona ndio mwenyewe, uliza Sulemani alikuwa nao wangapi? .... Bado akaona maisha Mungu ni Kujilisha UPEPO.
Jambo ambalo ni la hakika ni hili, watu wote wanapopitia changamoto wanamhitaji na wanamtafuta Mungu, hapo ndipo wengi wanakuwa wamechelewa, wengi wanalala mauti bila matumaini. Neno la leo linatuongoza kumtafuta Mungu sasa kabla ulimwengu haujageuka.
Kwa wale wanaopitia dhoruba fulani sasa, bado neema ya Mungu ipo, inua macho yako juu mtazame Mwokozi wako, ahadi hii itatimia kwako, "Mathayo
11:28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha."
NAKUTAKIA JUMATATU NJEMA YENYE BARAKA TELE
Na: Ev. Eliezer Mwangosi