Salaam,
Ukiona vema wapelekee wengine wasioupata ujumbe huu wa matumaini kwa watu wote, au nitumie contact zao. Naamini utabarikiwa.
Ujumbe unatoka: 1Nyakati 29:15
Kwani sisi tu wageni mbele zako, na wasafiri, kama walivyokuwa baba zetu wote; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana.
tAFAKARI:
Ni kawaida kwa mwanadamu kuishi bila kufikiri kwamba, kuna saa ambayo uhai utakoma. Shetani ametega mitego ambayo kila kunapokucha anajipatia maelfu ya watu wanaokufa wakiwa upande wake. Hebu kila mmoja ajiulize ingelikuwa Mungu amezima kibatari cha uhai wako usiku wa kuamkia leo, ungekuwa Upande gani? Je ni kweli tumejiandaa kusafiri ikiwa mauti yanatupata? Kama sivyo unafikiri ni wakati gani muafaka? Majibu ya wengi ni ya kujidanganya na kujilisha upepo. Kifo hakina hodi, ni sawa na muwindajia anavyomlenga swala kwa mshale, ndivyo mwanadamu anavyolengwa na mshale wa mauti bila kujua.
Mpendwa ni mara ngapi tumesikia watu wanakutwa na Mauti bila kuumwa? Unashangaa mtu anaenda kazini akiwa mzima, anakutwa amekufa kwenye gari lake au ofisini, wengine wanapanda basi vizuri unashangaa amekaa kwenye kiti wenzie wanashuka yeye anabaki amelala usingizi wa mauti. Mwanadamu fikiria juu ya ajali zinavyochomoa uhai wa watu, bila kusahau maafa ya Matetemeko, mafuriko, vibunga mpaka vya bahari kuhamia nchi kavu, milipuko ya mabomu kama si vita, magonjwa ya kila namna yakiwapata watoto hadi wazee. Rafiki wewe kuwa hai leo, unafikiri ni kwa juhudi yako? Hapana ni NEEMA YA MUNGU.
Daudi anasema sisi ni wasafiri na wageni hapa duniani, maisha ni kama vivuli, je tuko tayari kusafiri dakika yoyote? Ni rahisi kusema ndiyo: lakini hebu jiulize, huo mzigo wa Ulevi, kuishi na hawala au ndoa isiyo halali, kutomsamehe yule aliyekukosea, chuki na moyo wa visasi, hako karushwa, na hako kauzinzi ambako unasema utaacha ukioa au kuolewa, uongo na masengenyo, wivu na husuda, bila kusahau Uonevu na upendeleo kwa unaowaongoza, lakini hata Uchoyo na kutopenda ndugu, ugonvi na manyanyaso, na hizo Disko na starehe unazozipenda zaidi ya Kupenda Mungu n.k. Mizigo yote hiyo unamwachia nani? Mbinguni hakuna nafasi ya kukaa Mioyo iliyobeba mizigo kama hiyo. Hebu kila mtu afanye uamuzi sasa wa kufanya matengezo, saa ya wokovu ni sasa, achana na mambo ya kuwa mtu wa Dini za mtindo. WOKOVU NI HAKIKA.
NEEMA YA MUNGU IKATUSAIDIE KUISHI MAISHA YA MATUMAINI KATIKA ULIMWENGU WA SASA NA HATIMAE UZIMA WA MILELE
Ev: Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733
Kwa masomo zaidi fungua mitandao ifuatayo: http://emwangosi.blogspot.com/ (Vijana) http://kayanafamilia.blogspot.com/ (Ndoa) http://matengenezo.blogspot.com/ (Ujumbe wa Matengenezo)