INJILI YA MILELE - 2

79 views
Skip to first unread message

eliezer.mwangosi

unread,
Apr 28, 2016, 11:02:24 PM4/28/16
to
SIKILIZA: INJILI YA MILELE - MAZIWA YASIYOGHOSHIWA

MADA: UHUSIANO ULIOPO KATI YA NEEMA YA KRISTO NA SHERIA (TORATI) - 2

Somo hili ni muendelezo wa Somo no. 1, hivyo unashauriwa kusoma na kulielewa Somo lilotangulia kabla ya Somo hili. Roho mtakatifu atuongoze kuisikia sauti ya Mwokozi kupitia ujumbe huu. 

Kupitia utata uliopo kati ya Neema na Sheria katika safari ya wokovu, kuna hatari ya makundi mawili kupotea na kuukosa uzima wa milele, moja ni lile linaloamini kuwa HAKI au Utakatifu unapatikana kwa kushika Amri (Sheria/Torati) za Mungu, na lingine ni lile linaloamini kuwa HAKI inapatikana kwa Imani, hivyo Amri (Sheria/Torati) za Mungu hazina Sehemu katika maisha ya Mkristo. Je Biblia inasemaje? 

Kwanza kabisa tuangalie utata uliopo kwenye neno Torati, lina maana gani? Imeanza na Ililetwa lini? Mungu aliitoa kwa makusudi gani? Je sisi tulio okolewa kwa Neema inatuhusu kwa namna yoyote?

Maana ya Torati:
Kwa lugha ya asili,  TORATI maana yake ni SHERIA Ambayo ndani yake ina; MAUSIA, SHERIA, AMRI, HUKUMU, SHUHUDA - Soma 1Wafalme 2:3-4 "Uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia Zake, uzishike Sheria Zake, na Amri Zake, na Hukumu Zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika TORATI ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo na kila utazamako. Kwa tafsiri ya kawaida Torati (Torah) ni Muongozo (Instruction or Guide).

Kwa muktadha wa Biblia na wayahudi walivyoamini, Torati ni Vitabu vitano 5, vilivyoandikwa na Musa - Mwanzo, Kutoka, Mambo ya walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati. Kwa Wayahudi ukisema Torati maana yake ni maandishi yote ya Musa aliyoyaandika kutoka kwa Bwana. Wayahudi walitengeneza Sheria 613, kutoka katika Vitabu vitano vya Musa, kwa ajili ya msistizo na urahisi wa kufundisha. 

Sheria hizo 613 ziligawanywa katika Vitabu 31 kutokana na matumizi - Mfano: Utii kwa Mungu, Utakaso, Usafi, Vita, Wafalame, Hukumu na Adhabu, Huduma za Hekalu, Kafara, Mashamba, Mavuno, Familia, Vyakula, Biashara na mikopo, Sikukuu n.k. Unaweza kuzihakikisha kupitia tovuti hii: "http://therefinersfire.org/original_commandments1.htm". Unaweza pia kupata maelezo zaidi kupitia tovuti zingine, tafuta - 613 Laws.  Mbali na hizo zilizoandikwa, walikuwa nyongeza ambazo hazikuandikwa bali zilikuwa zinarithiwa kwa mdomo.

Zingatia:
Kiuandishi Torati inajumuisha sheria za aina mbili, ya Kwanza ni - Amri au Sheria inayoonyesha Dhambi, kwa muhtasari ziko AMRI 10 - Kwanza zilipotolewa kwa Musa, ziliandikwa na Mungu mwenyewe juu ya mawe "Kutoka 31:18", zilikuwa zinatunzwa ndani ya Sanduku la Agano - "Kumbukumbu la torati 10:5", Ni za milele, Takatifu na kamilifu "Warumi 7:12, Zaburi 111:7-8, Mathayo 5:17-19, Zaburi 19:7", Ndio jumla ya Mapenzi ya Mungu ambayo inampasa mwanadamu kutenda "Mhubiri 12:13, Yakobo 2:10-12". Kutozitii ndio UASI au DHAMBI. 

Sehemu ya Pili - ndio inayojumuisha Sheria zingine zote zilizobaki, pamoja na hukumu, maagizo, mashauri n.k. Hizi ziliandikwa "Kutoka 31:19", Ilitunzwa nje ya Sanduku "Kum la Torati 31:26", Baadhi ziliondolewa, zilikuwa kivuli au mfano katika mpango wa ukombozi "Waebrani 9:10-11, Waefeso 2:15". Pia zingine hatulazimiki kuzishika kiroho kutokana na mfumo wa jamii, mfano - Sheria za vita, mahakama, Tohara, Kusaza mavuno, kuwaua waovu, riba za mikopo. nk. Ingawa kuna Sheria nyingi bado jamii inazitumia hata katika serikali zetu, mfano. Sheria za Afya, kupumzisha mashamba, sheria za mahakama, mirathi na wajane nk.

Torati au Sheria ilianza lini? 
Kutokana na maelezo hayo hayo juu, Baadhi ya Sheria au Torati  ilianza tangia Mwanzo Kabla ya Musa au Taifa la Isareli. Mapenzi ya Mungu yalikuwepo na yatadumu kuwepo MILELE ndio manana Dhambi inadumu hadi leo. Kizazi cha Nuhu, bila kusahau Sodoma na Gomora waliangamizwa kwa sababu ya kutotii Sheria za Mungu Kabla ya Taifa la Izraeli kuwepo na Torati kutolewa kwa Musa. Mfano - Mwanzo 4:7, Mwanzo 13:13, Mwanzo 6:5-8, Sheria ya kafara Mwanzo 22:13.

Kwanini Mungu alimpatia Musa Torati?
1. Kuwakumbusha Mapenzi yake au Sheria zake ambazo waisareli walizisahau wakiwa Utumwani Misri, ili wasimtende Dhambi. Ambazo kuanzia Mwanzo kwa Adam, kizazi cha Nuhu, hadi Ibrahimu baba yao alizishika kwa Imani na kuhesabiwa haki Kabla yao. Sheria ya Milele aliiandika katika vipande vya mawe, kwa ufupi zikiwa 10, ambazo baadaye Yesu alizifundisha kwa Mapana akieleza namna ya kuzitenda.

2. Kuwafundisha namna ya kuishi ili wafanikiwe, kiroho na kimwili, kama taifa lenye jamii isiyo kuwa na, Utawala wenye mamlaka, wala Madaktari na Bwana afya, wala vikosi vya maskari wa vita na ulinzi, wala wanasheria na mahakimu, wasio na washauri wa ndoa, wala wataalamu wa biashara na mikopo, hakuwa na Mabwana shamba n.k. Mungu aliamua kuwapatia kanuni zote za maisha ili kuwafanikisha katika maisha. Hivyo kanuni zote na maagizo ya Torati kwa waisraeli yalitolewa kwa sababu ya Upendo wa Mungu kwa watu wake wapate kufanikiwa. Yoshua 1:7-8.

3. Katika pambano kuu kati ya Wema na Ubaya, Mungu aliweka Mpango wa Ukombozi kwa wanadamu walioanguka dhambini, Kabla ya Yesu kuja; Mungu alitoa sheria zilizokuwa zinalenga kifo cha Yesu msalabani, kulikuwa na sheria za huduma za Kafara na Upataniso. Hizi ziliambatana na vyakula, vinywaji, miandamo ya miezi... na zilikuwa siku zilipokuwa zikifanywa ilikuwa ni Mapumziko rasmi (Sabato), Mfano soma: Mambo ya walawi 4:26-29, 16:5-30, 23:26-38, 25:8-10 pia Hosea 2:11 nk. Sheria zote za huduma za  kafara na upatanisho, ZILIKAMILISHWA na kifo cha Yesu pale msalabani. 

Jambo la Msingi kufahamu ambalo Shetani hataki likae katika akili zetu ni hili; Mungu ni PENDO na kwamba wakati wote anatuwazia mema ili tufanikiwe, Torati au Sheria zimetolewa na Mungu ili mwanadamu, kwa nyakati tofauti, apate kufanikiwa katika nyanja zote. 1Wafalme 2:3-4. Tukijua hilo, tutakuwa na hekima ya kujua lipi ni hitaji letu kwa sasa ili tufanikiwe kiroho na kimwili na lipi halitakiwi kwa sasa kutokana na Neno la Mungu. 

Hitimisho:
Mungu ni Upendo - 1Yohana 4:8, 16. Mungu wakati wote hutuwazia mema ili tufanikiwe - Yeremia 29:11, 33:9. Mungu hana kigeugeu - Malaki 3:6, wala hawezi kusema uongo - Hesabu 23:19.  Hivyo hawezi kutoa sheria zenye kudhuru maisha mwanadamu, halafu ajutie na kufanya marekebisho. Ndio maana mtume Paulo anasema Torati asili yake ni ya Rohoni. Na Yesu alikuja ili Torati itimizwe ndani yetu kwa Imani - Warumi 8:3-4.

Mungu awabariki mnapoendelea kutafakari ujumbe huu, japo unaweza kuwa na maelezo kwa kifupi juu ya Torati - Somo la 3, tutaanza kujifunza Kazi ya Neema juu ya Amri au Sheria za Milele, zinaoonyesha mapenzi ya Mungu na Uovu. Pia tutajifunza maana ya Yesu kuja KUTIMILIZA Torati na Manabii - Mathayo 5:17-20.

WEMA WA MUNGU UENDELEE KUWA JUU YA KILA MMOJA ANAYEHITAJI KUNYWA MAZIWA YASIYOGHOSHIWA.

Na: Ev. Eliezer Mwangosi
Simu: 0767 210 299 - Kwa ajili ya maswali, ushauri na Maombi kwa wenye Shida.




Sent from Samsung tablet
Reply all
Reply to author
Forward
0 new messages