NENO LA LEO - TOKENI KWAKE ENYI WATU WANGU
Ufunuo 18:4 "Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka Mbinguni, ikisema, TOKENI KWAKE, ENYI WATU WANGU, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake".
Wakati dunia yetu ikiwa inazidi kupunga mkono wa KWAHERI, ikiaga taratibu lakini kwa uhakika, ikifikia mwisho kutokana na kikombe cha uovu kujaa, kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu na Miji ya Sodoma na Gomola; Mungu anatoa onyo la Mwisho. Mwenye masikio na asikie.
Shetani na mawakala zake, wakiwemo viongozi wa dini mbalimbali na manabii watendao kazi ya Injili kwa Hila, wameijaza Dunia kila namna ya uchafu, na wengi bila kujua wanaandaliwa hukumu ya mwisho. Dunia hii iko chini ya Laana kubwa, japo masikio ya wanadamu yametiwa pamba, na macho yao yametiwa upofu, wasiweze kuipambanua Dhambi. Dini zimekuwa za mtindo na nadharia tu, hofu ya dhambi haipo tena.
Nabii Isaya alitabiri: Isaya 24:4-6 " Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana WAMEZIASI SHERIA, WAMEIBADIRI AMRI, WAMELIVUNJA AGANO LA MILELE. Ndiyo sababu LAANA imeila Dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na HATIA ......". Viongozi wa Dini waliohusika kubadili Amri za Mungu na wale wanaoendelea kufundisha Amri tofauti na NENO la Mungu, ndio wanaendelea kukijaza kikombe cha UOVU na kuilemea Dunia.
Kuna watu ambao walisha chagua kupotea na kuwa Kuni katika moto wa Jehanamu, lakini kwa bahati mbaya sana, kuna watu wa Mungu wazuri, ambao wamedhamiria kupata uzima wa milele, ila adui shetani amewapotosha kwa njia ya Manabii na Viongozi wa dini walio amua kupotosha kweli ya Mungu. DHAMBI ni UASI wa sheria za Mungu, leo hii SHERIA za Mungu zimekuwa kitu kigeni kwa watu wa Dini, unashangaa watu wanabishana juu ya Utii wa Sheria za Mungu na kuzua Uongo kuwa Yesu aliziondoa, wakati Yesu alikuja kutuokoa, yaani kutupatia msamaha na USHINDI wa dhambi.
Dhambi za Ushoga, Usagaji, na mbaya zaidi kujibadili Jinsia, na uzazi wa chupa wa kununua mayai ya kiume na kupandikizwa tumboni mwa mwanamke, ili kupata mtoto nje ya tendo la ndoa, ni UCHAFU uliokijaza kikombe cha uovu dunia yetu, na kuiamsha hasira ya Bwana. LAANA zote hizi ni matokeo ya kutiwa giza, Katika kuipambanua na kuitii sheria ya Bwana.
Rafiki; huu ni wakati wa kumwambia Bwana akupatie macho ya kuiona sheria ya Bwana kama alivyoitoa, ruhusu Yesu akupatie uwezo wa Roho mtakatifu ili uweze kutembea katika utii na ushindi na hatimaye kuwa kati watakatifu, hao wazishikao Amri za Mungu na Imani ya Yesu - Ufunuo 14:12 "Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao Amri za Mungu, na Imani ya Yesu".
WITO: TOKENI KWAKE ENYI WATU WANGU .... MPINGENI SHETANI ..... MTIINI MUNGU.
Hebu kila mmoja ajifunze Amri za Mungu na kuruhusu Roho mtakatifu atawale maisha yetu, ili tuishi maisha matakatifu bila kuhukumiwa. Wokovu halisi ni maisha ya utii wa Amri za Mungu ndani ya Kristo. Hebu tafakari: Zaburi 119:155 "Wokovu u mbali na wasio haki, kwa maana hawajifunzi Amri zako".
WEMA WA MUNGI UKAWE JUU YA KILA MMOJA MWENYE KUISIKIA SAUTI YA WITO HUU MKUU. NAWATAKIA SIKU NJEMA.
Na: Ev. Eliezer Mwangosi - Simu: 0767 210 299.