Ibwe Salimu
unread,May 25, 2012, 8:20:33 AM5/25/12Sign in to reply to author
Sign in to forward
You do not have permission to delete messages in this group
Either email addresses are anonymous for this group or you need the view member email addresses permission to view the original message
to Universities
Na Mhe Zitto Kabwe
Mwalimu Azaveli Lwaitama ni mwalimu na mlezi wangu nje ya darasa.
Alipokuwa Katibu wa Umoja wa Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
mimi nilikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Idara ya Uchumi. Nilikuwa
nashinda kwenye Ofisi ya UDASA tukijadiliana kuhusu Umajumui wa
Afrika
(Pan-Africanism), Ujamaa na harakati za kulinda haki za watu. Ilikuwa
ni nadra kwa mwanafunzi wa uchumi kuwa karibu na mwalimu wa lugha na
mnadharia mkubwa. Wanafunzi wa uchumi tulikuwa tunajidai na kujivuna.
Tulikuwa tunajiona bora sana maana darasa letu halikuwa linazidi watu
40 na kwa kweli wote hawamalizi. Darasa langu tulimaliza wanafunzi 25
tu kati ya 40 tulioanza. Mwalimu Lwaitama ni mpenzi mkubwa wa
Muungano
kama nilivyo mimi. Tumeapa kuulinda kwa namna yeyote ile. Yeye
alikuwa
mhafidhina (conservative) sana akitaka Muungano wa muundo huu
aliouacha Mwalimu Nyerere. Mimi nataka kuulinda kwa kuufanyia
marekebisho makubwa sana ya kimuundo. Hatukuwa tunakubaliana.
Wiki iliyopita Mwalimu Lwaitama kaandika kuhusu muundo wa Muungano
katika makala zake za kila wiki katika gazeti la kimombo la The
Citizen. Amebadili msimamo. Ameona sasa muundo wa Muungano ulivyo sio
endelevu. Ametoa mapendekezo niliyoyatoa siku za nyuma katika
mazungumzo yetu ingawa yeye bado anayasema kwa shingo upande.
Lwaitama
sasa anataka Serikali mbili zilizonyumbuliwa. Anapendekeza Waziri
Mkuu
wa Muungano mwenye nguvu za za kitendaji. Nampongeza kwa kuboresha
mawazo yake.
Hata hivyo bado Mwalimu wangu na Watanzania wengi wamejikita katika
mjadala wa Serikali ngapi. Idadi ya Serikali inaonekana kama ndio
dawa
ya kero za Muungano. Ni kweli Wazanzibari wanataka uhuru zaidi na
wengine hawataki kabisa Muungano. Unawalalia. Unawanyima uhuru wa
kuamua baadhi ya mambo yao na japo halisemwi unawanyima wanasiasa wa
Zanzibar mamlaka ya masuala mengine ambayo yangewafanya
wajilimbikizie
madaraka.
Huku bara napo kuna watu, tena wanaongezeka kwa kasi kweli kweli,
wakitaka Tanganyika yao. Tena wengi vijana. Demografia zetu
zinaonyesha kwamba Watanganyika waliozaliwa Tanganyika ni takribani
asilimia 12 tu ya Watanzania. Asilimia 70 ya Watanzania wamezaliwa
wakati Muungano umeshasherehekea miaka 15 ya kuzaliwa kwake. Lakini
wanataka Tanganyika yao. Wamechoshwa na kelele za Wazanzibari.
Hawawataki Wazanzibari kujaa kwenye Bunge la Muungano wakati wapo
kiduchu sana. Wanasiasa nao, japo hawasemi waziwazi wanataka wawe na
mamlaka zaidi bila kulazimika kushauriana na wanasiasa wa Zanzibar.
Linapokuja suala la wagombea Urais ndio kabisa wanakereka kutafuta
mgombea mwenza kutoka Zanzibar. Wachambuzi wa historia za kisiasa
siku
wakiamua kufanya tafiti watachoka na roho zao watakapoona aina za
wagombea wenza ambao wagombea Urais huteua, hasa kutoka sisi vyama
vya
upinzani.
Kimsingi idadi ya wapinga Muungano inazidi kuongezeka siku hata siku.
Ukiwauliza kwa nini hawataki Muungano wanasema aah, basi tu. Kama ni
Mzanzibari atasema Tanganyika wanatutawala. Kama ni Mtanganyika
atasema Wazanzibari wamezidi kelele, tunataka Tanganyika yetu. Sisi
‘Unionists’ (Wanamuungano) nao hatuna majibu ya kuridhisha sana na ya
kukonga nyoyo. Isipokuwa tu, Muungano huu ni wa aina yake Afrika na
Duniani. Ni alama pekee ya kuonyesha Mwafrika kupinga mipaka ya
kikoloni. Sasa hili haliwaingii kichwani
‘secessionists’ (Wanautengano) na hatuna la kuwasaidia. Lakini ni
lazima tuurekebishe Muungano huu. Ulivyo sasa utavunjika tu. Kuulinda
Muungano ni kuufanyia marekebisho makubwa. Mwalimu Lwaitama kaliona
hilo. Pendekezo lake liboreshwe sasa. Sio rahisi sana.
Sasa tufanyeje? Serikali moja itaimeza Zanzibar. Serikali Tatu ni
gharama kuendesha na Serikali mbili zimeimeza Tanganyika na watu
wanataka Tanganyika yao na zinainyima uhuru Zanzibar na watu wanataka
wawe huru zaidi. Mfumo wa Serikali ngapi na kadhalika ni moja ya
mikakati ya wanasiasa katika kusaka vyeo. Sisemi sio halali kujadili
lakini kiukweli mfumo gani wa Muungano hautaongeza fungu la dagaa kwa
mwananchi wa Kagongo au sinia la ubwabwa kwa mwananchi wa Mkanyageni.
Waingereza wana msemo ‘unataka kula keki yako na kubaki nayo’, basi
tuwe na Serikali zote.
Nimeanza na Mwalimu Azaveli Lwaitama. Naboresha hoja yake kwa kurudia
niliyowahi kuyasema huko nyuma kuhusu muundo wa Muungano. Tuwe na
Dola
Moja tu. Ndio, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wala sio Shirikisho
la Tanzania (kwanza litatuondoa kwenye kiti chetu kule Umoja wa
Mataifa maana kwa jina letu sisi tunakaa katikati ya Uingereza na
Marekani. Katikakati ya mabwana wakubwa, labda ndio maana wanatupa
misaada sana, unajuaje?). Tuwe na Rais mmoja tu mwenye mamlaka kamili
ya Asasi za Dola – Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Uhamiaji, Sera za
Fedha na jukumu la jumla la kusimamia ustawi wa Jamhuri ya Muungano
wa
Tanzania. Achaguliwe na Watanzania wote wa pande zote mbili za
Muungano kwa kupata zaidi ya nusu ya kura za pande zote za Muungano.
Tuachane na mambo ya Mgombea Mwenza. Tumejaribu tumeona hana maana
zaidi ya kutembea na mikasi tu.
Zanzibar iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote ambayo sio ya
Muungano. Tanganyika iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote
ambayo sio ya Muungano. Hawa watateuliwa na Rais wa Muungano kutoka
chama chenye Wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi
Tanganyika
na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Wote watakuwa ni Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano kwa utaratibu kwamba iwapo Rais anatoka Zanzibar,
basi Waziri Mkuu wa Tanganyika atakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na wa
Zanzibar atakuwa Makamu wa Pili wa Rais. Kule kule kwenye misingi
haswa ya Muungano. Hawa wataongoza Mabaraza yao ya Mawaziri na
watakuwa na nguvu ya kuteua na kufukuza Mawaziri wanavyotaka.
Hawatakuwa Wabunge katika Bunge la Muungano.
Bunge la Muungano litakuwa dogo lenye Wajumbe wasiozidi 101 pamoja na
Rais wa Bunge la Muungano. Wabunge wa Muungano watatoka kwenye mikoa
(au Majimbo kama sera ya Majimbo itakubalika). Kwa utaratibu wa sasa
kila mkoa utachagua wabunge 2 mmoja mwanamke mmoja mwanaume kwenda
Bunge la Muungano. Wajumbe wa Ziada watatokana na uwiano wa kura
ambazo kila chama kimepata kwenye kura za Rais wa Muungano. Idadi hii
yaweza kupunguzwa na hata kuwa na Wabunge 51 tu akiwemo Rais wa Bunge
la Muungano ambapo kwa mikoa ya sasa kila mkoa utachagua Mbunge 1 na
wengine watokane na uwiano. Rais wa masuala ya Muungano atakuwa Mkuu
wa Shughuli za Serikali katika Bunge la Muungano na Rais kwa mwaka
mara moja atahutubia Baraza la Taifa (Wabunge wa Bunge la Muungano na
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka kila upande wa Muungano).
Wazungu wanaita hotuba hii ‘State of the Union’ (Hali ya Taifa) na
wengine huita ‘Queen’s Speech’ (Hotuba ya Malkia).
Mkuu wa nchi mmoja, Dola moja ya Jamhuri ya Muungano. Serikali mbili
na kila upande una Serikali yake yenye mamlaka kamili ya maisha ya
watu wao ya kila siku. Haya matatu pamoja na Serikali ndogo ya
Muungano. Lakini tutakuwa tumepata kila kitu labda. Wenye kutaka
Uhuru
mpaka Zanzibar watapata. Wenye kutaka Tanganyika watapata na wenye
kutaka Muungano kama Dola yenye nguvu watapata.