Maelezo ya uthibitisho ya Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema
(mbunge) juu ya kauli ya uwongo iliyotolewa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo
P.K. Pinda (mbunge) wakati akijibu maswali kwa Waziri Mkuu katika kikao cha
tatu cha mkutano wa pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Tarehe 10 Februari, 2011
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu
wa Hansard ya tarehe 10 Februari 2011, nilikuomba “kupata ufafanuzi
kwamba Mbunge anaweza akachukua hatua gani kama anaona mtu mwenye nafasi kubwa
katika nchi kama Waziri Mkuu analidanganya
taifa na kulidanganya Bunge.” Badala ya kunipatia ufafanuzi niliouomba,
Mheshimiwa Spika ulitoa kauli ifuatayo, kwa mujibu wa Hansard hiyo:
“Mheshimiwa Mbunge, Bunge hili lazima liwe na adabu inayostahili. Kwa
hiyo kama tutafanya Bunge letu hili ikawa ni
mahali, sasa unataka kusema Waziri Mkuu kwa ahadi aliyoweka ndani ya Bunge hili
anadanganya? Kama anadanganya naomba
ukaiandike vizuri kabisa kuhusu kudanganya kwake, halafu nitakuambia tufanye
nini.”
Mheshimiwa Spika,
Baada ya
maelekezo hayo ya awali, ulitoa maelekezo ya ziada kwamba “nampa mpaka tarehe 14
asubuhi alete maandiko ya kuthibitisha maneno aliyoyasema…. Kwa hiyo
tarehe 14 kipindi cha asubuhi atoe maelezo ya kwamba Waziri Mkuu amesema uongo.
Maana yake alichosema kwamba Waziri Mkuu amesema uongo sasa anataka tumpe
Mwongozo wa namna ya kufanya na akasema aandike. Sasa kifungu hiki cha 64
kinamdai alete maelezo hayo mpaka tarehe 14.”
Mheshimiwa Spika,
Maneno yote
ya Hansard niliyoyanukuu hapo juu yanathibitisha kwamba mimi sikusema Waziri
Mkuu amesema uongo, bali niliomba mwongozo wa Spika kuhusu hatua zinazoweza
kuchukuliwa na Mbunge endapo kiongozi wa ngazi za juu kama
Waziri Mkuu atasema uongo au kulidanganya Bunge. Hata hivyo, kwa vile
umenielekeza nitoe maelezo uthibitisho kwamba Waziri Mkuu alisema uongo au
kulidanganya Bunge, na kwa kutimiza maelekezo yako, naomba sasa nithibitishe
kwamba kauli ya Waziri Mkuu kuhusu matukio yaliyopelekea mauaji ya wananchi wa
Arusha na Mbarali yalikuwa ya uongo na kwamba Waziri Mkuu alilidanganya Bunge.
1. UONGO WA KWANZA
Mheshimiwa Spika,
Waziri Mkuu
amenukuliwa kwenye Hansard ya tarehe 10 Februari 2011 akidai kwamba
“… tumepoteza maisha ya Watanzania watatu bila sababu.” Huu
ni uongo wa kwanza wa Waziri Mkuu Bungeni. Ukweli ni kwamba waliopoteza maisha
ni Watanzania wawili – Dennis Michael Shirima na Ismail Omari – na
Mkenya mmoja aliyejulikana kwa jina la Paul Njuguna.
2. UONGO WA PILI
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu
wa Hansard ya tarehe 10 Februari 2011, Waziri Mkuu alitamka maneno yafuatayo
kuhusu suala la maandamano ya Arusha: “Mliomba wenyewe mfanye maandamano,
hatukukataa, mkakaa na askari pale mkaelewana vizuri. Mkakubaliana kwamba sisi
tunafikiri ili tuweze kuwadhibiti vizuri na kuwalinda vizuri, tutumie route
moja tu. Wenzangu nyie mkakataa.” Kauli mbili za mwisho kwamba zina maana
kwamba Jeshi la Polisi lilipendekeza kwamba njia moja ya maandamano ndiyo
itumike na kwamba viongozi wa CHADEMA walikataa pendekezo hilo. Kauli hiyo, Mheshimiwa Spika, ni ya
uongo na ilikuwa na lengo la kulidanganya Bunge.
Mheshimiwa Spika,
Ukweli wa
jambo hili ni kwamba tarehe 31 Desemba 2010, Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya
Arusha Mjini alitoa taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha
Mjini yenye kumb. Na. CDM/AR/W/20/10 yenye kichwa cha habari: “TAARIFA YA
MAANDAMANO NA MKUTANO WA HADHARA TAREHE 5 JANUARI 2011.” Sehemu ya barua
hiyo ilimjulisha Mkuu wa Polisi wa Wilaya kwamba “… CHADEMA (Wilaya
ya Arusha Mjini) tutakuwa na maandamano ya amani tarehe 5 Januari 2011
yatakayohitimishwa na mkutano wa hadhara katika viwanja wa NMC – unga
Ltd.” Aidha, barua hiyo ilipendekeza njia ifuatayo ya maandamano hayo:
“Maandamano hayo yataanzia maeneo ya Phillips saa NNE asubuhi, kuelekea
Sanawari, Mianzini, Stand Kuu kuelekea Mnara wa Azimio, kupitia Polisi –
Manispaa – Clock Tower kushukia Sokoine Road, kasha Friends’ Corner
na kuingia viwanja vya NMC.” Nakala ya taarifa hiyo ya CHADEMA kwa Jeshi
la Polisi Wilaya ya Arusha Mjini imeambatanishwa katika maelezo haya kama Kielelezo ‘A.’
Mheshimiwa Spika,
Mnamo
tarehe 2 Januari 2011, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini
alimwandikia Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini barua nyingine yenye
kumb. Na. CDM/AR/W/20.1/11 ambapo alimjulisha kwamba “msafara wetu
utabaki kama tulivyoainisha kwenye barua (ya
tarehe 31 Desemba 2010.)” Vile vile barua hiyo ilimjulisha Mkuu wa Polisi
wa Wilaya juu ya “… vituo maalumu vya wananchi kukutana ili baada
ya hapo waweze kujiunga na maandamano (msafara mkuu).” Nakala ya barua ya
tarehe 2 Januari 2011 nayo imeambatanishwa kama
Kielelezo ‘B’ kwenye maelezo haya.
Kwa
ushahidi huu wa maandishi, ni wazi kwa hiyo kwamba kauli ya Waziri Mkuu kwamba
Jeshi la Polisi la Wilaya ya Arusha Mjini ndio waliopendekeza njia ya
maandamano ilikuwa ni ya uongo na/au ililenga kulidanganya Bunge.
Mheshimiwa Spika,
Mnamo
tarehe 3 Januari 2011 viongozi wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha Mjini walikutana
na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha ili kujadili
masuala mbali mbali yanayohusu maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 5
Januari. Moja ya mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo ndani ya Ofisi ya
Kamanda wa Polisi wa Mkoa ilikuwa ni kuchagua njia muafaka zaidi ya maandamano
hayo. Kufuatia mazungumzo hayo, mnamo tarehe 4 Januari 2011 Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Arusha SSP Zuberi Mwombeji alimwandikia Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya
ya Arusha Mjini kumjulisha kwamba “kimsingi mmekubaliwa kufanya
maandamano na mkutano wenu wa hadhara tarehe 5 Januari 2011….”
Katika
barua hiyo, Mkuu wa Polisi aliitaka CHADEMA ichague moja kati ya njia mbili za
maandamano ambazo zilijadiliwa na kukubaliwa katika mkutano wa tarehe 3
Januari, yaani njia ya “kuanzia Phillips, Sanawari Mataa, kushuka na
barabara ya AICC, Goliondoi, Sokoine Road, Friends Corner na kuingia uwanja wa
NMC”; au “kuanzia Phillips, sanawari Mataa, Mianzini Mataa, Florida
Annex, Stand, CRDB Bank, Friends’ Corner hadi uwanja wa NMC.”
Nakala ya barua ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya yenye kumb. Na. AR/B.5/VOL.II/63
imeambatanishwa kama Kielelezo ‘C’
kwenye maelezo haya. Siku hiyo hiyo ya tarehe 4 Januari 2011 Mwenyekiti wa
CHADEMA Wilaya alimtaarifu Mkuu wa Polisi Wilaya kwamba maandamano yangepitia
njia ya Phillips, Sanawari Mataa, Mianzini
Mataa, Florida Annex,
Stendi Kuu ya Mabasi, CRDB Bank, Friends’ Corner na kuingia viwanja wa
NMC – Unga Ltd.
Kufuatana
na mtiririko huu wa matukio, sio kweli kwamba Polisi ndio waliopendekeza njia
ya maandamano na wala sio kweli kwamba CHADEMA walikataa njia hiyo iliyopendekezwa
na Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba Polisi
walipendekeza njia ya maandamano na CHADEMA wakaikataa ilikuwa ni kauli ya
uongo na yenye lengo la kulidanganya Bunge.
3. UONGO WA TATU
Mheshimiwa Spika,
Aya ya tatu
ya kauli ya Waziri Mkuu inadai kwamba Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya
CHADEMA kihalali lakini CHADEMA wakaamua “… kufanya maandamano yale
bila kujali kabisa kwamba utaratibu uliokuwa wamekubaliana mmeukiuka
wenyewe.” Kauli hii ya Waziri Mkuu ni ya uongo na ilikuwa na lengo la
kudanganya Bunge. Kwanza kabisa, utaratibu wa
Jeshi la Polisi kupiga marufuku maandamano ulikuwa ni ukiukaji wa sheria husika
za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu
wa Sheria ya Jeshi la Polisi, mara baada ya taarifa ya maandamano na mkutano wa
hadhara wa CHADEMA kutolewa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya, njia pekee halali ya
kusitisha maandamano na mkutano uliopangwa ilikuwa ni kwa Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Arusha kutoa amri ya kusitisha maandamano na mkutano huo. Sheria hiyo
inasema wazi kwamba Ofisa wa Polisi aliyepewa taarifa ya maandamano au mkutano
wa hadhara hatatoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo
“isipokuwa tu kama amejiridhisha kwamba
maandamano au mkutano huo unaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha
usalama na/au utulivu wa umma au kutumiwa kwa malengo haramu.”
Aidha, kwa
mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, chama cha siasa kikishatoa taarifa ya
mkutano kinaruhusiwa kufanya mkutano huo isipokuwa tu na kama kitapokea amri
kutoka kwa ofisa wa polisi mwenye mamlaka ya eneo husika ikielekeza kwamba
mkutano huo usifanyike kama ilivyopangwa. Na
chini ya sheria hii vile vile, ofisa wa polisi aliyepewa taarifa ya mkutano
haruhusiwi kutoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo mpaka
atakapojiridhisha kwamba mkutano au maandamano hayo yana lengo la kutekeleza au
kutumiwa kwa malengo haramu; au kama maandamano au mkutano huo unaweza au
umelenga kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa
umma katika eneo husika.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
vyovyote vile, kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya
Siasa, amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano au mkutano wa hadhara
uliotolewa taarifa ni lazima itolewe na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na ni lazima iwe
ni ya maandishi. CHADEMA haijawahi kupokea wala kuonyeshwa amri ya Mkuu wa
Polisi wa Wilaya ya Arusha ya kupiga marufuku maandamano ambayo Mkuu huyo huyo
wa Polisi wa Wilaya alikuwa ameyaruhusu kwa maandishi! Aidha, tumeona taarifa
ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe
13 Januari 2011 ambayo imedai kwamba CHADEMA iliandikiwa barua yenye kumb. Na.
ARR/B.5/1/VOL.VIII/24 ya tarehe 4 Januari 2011 iliyoandikwa na “Jeshi la
Polisi mkoani Arusha kwa mujibu wa sheria … kusitisha maandamano hayo ya
CHADEMA….” Madai hayo hayana ukweli wala msingi wowote kisheria kwa
sababu Kamanda wa Polisi wa Mkoa hana mamlaka yoyote kisheria ya kusitisha au
kupiga marufuku maandamano au mikutano ya hadhara. Mtu pekee mwenye mamlaka
hayo chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa ni
‘ofisa polisi mwenye mamlaka ya eneo’ la mkutano, kwa maana
nyingine, Mkuu wa Polisi wa Wilaya!
Aidha, tuna
taarifa kwamba jioni ya tarehe 4 Januari 2011 Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi
Mwema alitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba maandamano na mkutano wa
hadhara wa CHADEMA yamepigwa marufuku kutokana na kuwepo kwa ‘taarifa za
kiintelijensia’ kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani wakati wa maandamano
na/au mkutano huo wa hadhara. Tangazo hilo la Inspekta Jenerali wa Polisi
lilikuwa haramu na ni ukiukaji wa makusudi wa Sheria ya Jeshi la Polisi na
Sheria ya Vyama vya Siasa kwa sababu Inspekta Jenerali wa Polisi hana mamlaka
yoyote kisheria ya kuzuia au kuruhusu maandamano na mikutano ya hadhara ya
vyama vya siasa. Vile vile utaratibu wa kutoa amri za kuzuia ama kusitisha
maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa kutumia matangazo ya
televisheni na/au waandishi wa habari ni utaratibu mgeni katika nchi ya Tanzania na
hautambuliwi kabisa na sheria hizo!
Mheshimiwa Spika,
Hata kama
‘taarifa za kiintelijensia’ alizozisema Inspekta Jenerali wa Polisi
Saidi Mwema zilikuwa na ukweli - kwamba kulikuwa na uwezekano wa uvunjifu wa
amani iwapo maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA ungeendelea kama
ilivyokuwa imepangwa - bado Jeshi la Polisi la Tanzania lisingepaswa kutoa amri
ya kuzuia na/au kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA. Hii ni
kwa sababu, kuzuia na/au kusitisha maandamano sio hatua pekee inayoweza
kuchukuliwa kisheria na Jeshi la Polisi la Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya
Vyama vya Siasa, kila chama ambacho kimesajiliwa ‘kina haki ya kupatiwa
ulinzi na msaada wa vyombo vya ulinzi kwa malengo ya kuwezesha mikutano yenye
amani na utulivu.’ Swali la kumuuliza Waziri Mkuu hapa ni kwamba kama
kweli kulikuwa na ‘taarifa za kiintelijensia’ za uwezekano wa
uvunjifu wa amani, kwa nini Jeshi la Polisi lililokuwa na taarifa hizo
halikutoa ulinzi wa kutosha kwa waandamanaji?
Mheshimiwa Spika,
Hata kama
maandamano na mkutano wetu wa hadhara yangekuwa yamepigwa marufuku kwa mujibu
wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa – kitu ambacho
hakikufanyika – bado CHADEMA ilikuwa na uhalali wa kuendelea na
maandamano hayo na kufanya mkutano kama ilivyopangwa. Hii ni kwa sababu Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inatambua na kulinda uhuru wa wananchi ‘kukutana na watu wengine kwa
hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa
ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani….’ Aidha, kwa mujibu ibara
ya 64(5) ya Katiba, “… Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika
Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka mashrti
yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo
nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba, itakuwa batili.” Hii ina maana
kwamba hata kama Sheria ya Jeshi la Polisi na
Sheria ya Vyama vya Siasa inaruhusu Jeshi la Polisi kukataza na/au kusitisha
maandamano, Sheria hizo zitakuwa ni batili kwa kiasi cha ukiukwaji wao wa
masharti ya ibara ya 20(1) ya Katiba inayotoa uhuru wa kufanya maandamano ya
amani na mikutano ya hadhara.
4. UONGO WA NNE
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa
nne aliousema Waziri Mkuu unahusu sababu ya kusitishwa kwa maandamano ya amani
ya tarehe 5 Januari 2011. Kwa mujibu wa Hansard, Waziri Mkuu alitamka:
“Sasa mkaamua kufanya maandamano yale bila kujali kabisa kwamba utaratibu
uliokuwa wamekubaliana mmeukiuka wenyewe. Mheshimiwa Spika, sasa kilichotokea
pale ni namna ya kuzuia hayo maandamano....” Kauli hii ya Waziri Mkuu ni ya
uongo kwa sababu inapingana moja kwa moja na taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi
iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe 13 Januari 2011.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, “Jeshi la Polisi lilichukua hatua ya kuwaamuru
waandamanaji kusitisha maandamano hayo mara moja baada ya kuona kwamba yataleta
uvunjifu wa amani kutokana na jazba ya waandamanaji hao.” Wakati Waziri
Mkuu – ambaye hakuwepo Arusha - anadai Bungeni kwamba maandamano
yalisitishwa kwa sababu yalikiuka utaratibu, Jeshi la Polisi – lililokuwa
na mamia ya askari polisi kwenye eneo la tukio – linasema kwenye taarifa
rasmi kwamba maandamano hayo yalisitishwa kwa sababu ya jazba ya waandamanaji!.
Taarifa ya IGP kama kielelezo “D”
5. UONGO WA TANO
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa
tano wa Waziri Mkuu unahusu kauli yake juu ya umbali kati ya Kituo Kikuu cha
Polisi cha Arusha na mahali walipouawa waandamanaji watatu na wengine wengi
kujeruhiwa. Kwa mujibu wa Hansard, Waziri Mkuu alitamka yafuatayo kuhusu jambo
hili: “Mpaka mmekaribia mita 50 muweze kuingia kituo cha Polisi. Police
was left with no option kwa kujua tu kwamba kama
mkiingia hatujui litakalotokea ni kitu gani. Katika purukushani ile, masikini
wale marehemu wale watatu wakapoteza maisha.”
Kwa mara
nyingine tena kauli ya Waziri Mkuu Bungeni inapingana na kauli ya Jeshi la
Polisi. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jeshi hilo,
“walipokaribia kituo Kikuu cha Polisi cha Kati umbali wa kama mita 50 huku wakirusha mawe, chupa, fimbo, nondo,
mapanga na visu, amri halali na tahadhari za msingi zilizotolewa kuwataka
watawanyike mara moja. Wafuasi hao walikaidi amri na kuzidi kukaribia kituo kwa
lengo la kutimiza azma yao
ya kukivamia.” Hapa maana ni kwamba waandamanaji walishapita huo umbali
wa mita 50! Baada ya hapo, kufuatana na taarifa ya Jeshi la Polisi, hatua
zifuatazo zilichukuliwa:
(i) Hatua ya kwanza, yalipigwa mabomu ya machozi, onyo ambalo lilipuuzwa na
wakaendelea kusonga mbele;
(ii) Hatua ya pili, zilitumika risasi za baridi na mabomu ya vishindo bado
walikaidi na kuzidi kukaribia kituo cha Polisi;
(iii) Hatua ya tatu, zilipigwa risasi juu za onyo bado wakaendelea kusonga
mbele.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya
hatua zote hizo kushindikana kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi,
“kilichofuatia ni mapambano ya ana kwa ana kati ya askari na waandamanaji
waliokuwa wakisonga mbele kuvamia kituo. Katika mazingira hayo risasi za moto
ililazimika kutumika. Matokeo ya tafrani hiyo, watu 14 walijeruhiwa na
kufikishwa hospitalini ambapo watatu kati yao
walifariki dunia wakipatiwa matibabu.”
Mheshimiwa Spika,
Kama ni kweli hatua zote zilizoelezwa hapo juu
zilichukuliwa na Jeshi la Polisi basi ni wazi kwamba watu waliouawa au
kujeruhiwa waliuawa au kujeruhiwa kwenye uzio au mlango wa Kituo Kikuu cha
Polisi mjini Arusha! Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kama
ilivyo kwa kauli ya Waziri Mkuu, taarifa ya Jeshi la Polisi vile vile ni ya
uongo mtupu. Kwa ushahidi wa picha za video tulio nao, marehemu mmoja aliuawa
kwenye eneo la Mianzini ambalo liko zaidi ya kilometa tatu kutoka Kituo Kikuu
cha Polisi cha Arusha. Aidha, marehemu wa pili alipigiwa risasi katika eneo la
Kaloleni ambalo nalo liko zaidi ya kilometa moja kutoka kituo hicho. Ushahidi
wa video unaungwa mkono na ushahidi wa watu walioshuhudia mauaji hayo wenyewe.
6. UONGO WA SITA
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa
sita wa Waziri Mkuu unatokana na kauli yake kwamba “... kama Mheshimiwa
Mbowe na chama chako mngeliamua kushirikiana na Serikali hii mkafanya ule
mkutano kama tulivyokubaliana haya yote
yasingetokea.” Ukweli ni kwamba mkutano wenyewe uliohutubiwa na Dr. Wilbrod Slaa
na Mheshimiwa Philemon Ndesamburo ulishambuliwa kwa mabomu ya machozi na maji
ya kuwashawasha na kutawanywa kabla ya makundi ya watu kurudi kwenye mkutano na Dr. Slaa na
Mheshimiwa Ndesamburo kuendelea kuhutubia!
Aidha,
ushahidi wa maandishi kati ya CHADEMA na Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha
unaonyesha wazi kwamba CHADEMA walikubaliana na matakwa ya Jeshi la Polisi kwa
kuchagua njia moja ya maandamano. Hata viongozi waliokamatwa wakati wa
maandamano hayo walikamatiwa kati ya eneo la Sanawari na Mianzini wakiandamana
kwa kutumia moja ya njia zilizopendekezwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya! Na gari
iliyokuwa imewabeba Mheshimiwa Lucy Owenya na mke wa Dr. Slaa ilishambuliwa na
kuvunjwa vioo na Mheshimiwa Owenya na Mama Slaa kuumizwa na askari polisi
katika eneo la Sanawari Mataa wakati wakiwa katika njia ya maandamano
iliyopendekezwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba,
waliovunja makubaliano juu ya maandamano na mkutano wa hadhara walikuwa ni
Kamanda wa Polisi wa Mkoa ACP Thobias Andengenye na Inspekta Jenerali wa Polisi
Saidi Mwema walioamua kuingilia maamuzi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha
na kuyapiga marufuku maandamano hayo.
7. UONGO WA SABA
Mheshimiwa Spika,
Katika jibu
lake kwa swali la Mheshimiwa Martha Umbulla,
Waziri Mkuu alidai kwamba mkutano wa Baraza la Madiwani wa kumchagua Meya,
Naibu Meya na Wenyeviti wa Kamati ulianza “wajumbe wote 31
wakiwepo....” Hii ni kauli ya uongo. Kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya Kanuni
za Kudumu za Mikutano na Shughuli za Halmashauri ya Manispaa ya Arusha za 2003,
“kila mjumbe anayehudhuria mkutano wa Halmashauri au Kamati yoyote ya
Halmashauri ambamo yeye ni mjumbe ataweka sahihi yake kwenye Rejesta ya
mahudhurio inayotunzwa na Mkurugenzi kwa ajili hiyo.” Kwa kufuatana na
orodha ya mahudhurio ya mkutano wa tarehe 17 Desemba, walikuwepo madiwani 16
wote wakiwa madiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM)!
Kwa Waziri
Mkuu kusimama na kuliambia Bunge kwamba wajumbe wote 31 wa Halmashauri ya Jiji
la Arusha walikuwepo tarehe 17 Desemba 2010 wakati Rejesta ya mahudhurio
inaonyesha kwamba ni wajumbe 16 tu ndio walioweka sahihi zao kwenye Rejesta
hiyo ni uongo wa wazi. Angalia Kielelezo “E”
Mheshimiwa Spika,
Waziri Mkuu
alitoa kauli ya uongo tena pale aliposema kwamba mgombea wa CCM alishinda kura
za meya “walikuwa wanashindana mmoja wa CHADEMA, mmoja wa CCM.” Kwa
mujibu wa orodha ya mahudhurio ya mkutano wa tarehe 18 Desemba 2010 uliomchagua
Meya, waliokuwepo ni madiwani 17 ambao kati yao, 16 walikuwa wa CCM na mmoja
alitoka chama cha TLP. Hakukuwepo na mjumbe hata mmoja wa CHADEMA. Na hii
haishangazi kwa sababu ratiba ya mkutano huo inaonyesha kwamba siku ya tarehe
18 Desemba 2010 ilitakiwa kuwa siku ya mafunzo ya Madiwani yaliyokuwa yafanyike
Olasiti Garden. Madiwani wa CHADEMA ambao
hawakuwepo kwenye mkutano wa tarehe 17 Desemba wasingeweza kujua kwamba ratiba
ya mafunzo ilikuwa imebadilishwa na kuwa ratiba ya uchaguzi wa Meya! Ratiba ya
shughuli za tarehe 18.12.2010 kielelezo “F”
8. UONGO WA NANE
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa
nane wa Waziri Mkuu ni kauli yake kwamba “... utaratibu uliofuatwa
ulikuwa sahihi kabisa, haukukosewa kitu chochote. Meya ni halali kabisa,
alipatikana kihalali kabisa.” Huu ni uongo mtupu. Chini ya kanuni ya 8(3)
ya Kanuni za Halmashauri, “akidi katika mkutano wa kawaida wa mwaka na
mkutano wa kwanza wa Halmashauri itakuwa theluthi mbili ya wajumbe wote wa
Halmashauri.” Kwa kusoma kanuni ya 8(3) pamoja na kanuni ya 9, ni wazi
kwamba Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri wanatakiwa kuchaguliwa na
mkutano wa kwanza wa Halmashauri. Ili kukidhi
matakwa ya kanuni hizi, mkutano wa uchaguzi wa Meya na Makamu Meya wa Arusha
ulipaswa kuwa si chini ya wajumbe 21 ambao ni theluthi mbili ya wajumbe wote wa
Halmashauri hiyo. Kwa maana hiyo, mkutano wa tarehe 18 Desemba haukuwa mkutano
halali na viongozi wa Halmashauri waliochaguliwa na mkutano huo hawawezi kuwa
halali!
9. UONGO WA TISA
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa
tisa aliousema Waziri Mkuu Bungeni uko kwenye kauli ifuatayo: “Mheshimiwa
Spika, yaani hata kwa hesabu tu za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza hakuna
namna ambavyo kwa hali ilivyokuwa kwamba mna CHADEMA wajumbe 14, una CCM 16
utashindaje?” Hapa Waziri Mkuu alitaka kuaminisha Bunge kwamba hata kama wajumbe wa CHADEMA wangehudhuria kwenye mkutano huo
bado wasingeshinda kwa sababu wajumbe wa CCM walikuwa wengi zaidi ya wajumbe wa
CHADEMA. Lakini kwenye hotuba hiyo hiyo Waziri Mkuu alitoa kauli ifuatayo
kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri hiyo ya Arusha:
“Wakaingia awamu ya pili ya kumtafuta Naibu Meya, wakapiga kura, Mjumbe
wa kutoka TLP akashinda, CCM alishindwa hakupata kura hata moja, CHADEMA
hawakupata kura hata moja...”!
Mheshimiwa Spika,
Kwa akili
za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza kama iliwezekana kwa mgombea wa TLP
ambaye yuko peke yake katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kupata kura za
wajumbe wote wa CCM na kumshinda mgombea wa CCM ambaye – kwa kauli ya
Waziri Mkuu – hakupata kura hata moja, je, ingeshindikanaje kwa mgombea
wa CHADEMA yenye wajumbe 14 kushinda? Swali ni muhimu hasa hasa kwa vile chini
ya kanuni ya 9(1) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Arusha inasema
kwamba kura ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu wake itakuwa ni ya siri! Na kama inavyofahamika, katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ni mgombea wa CHADEMA ndiye aliyeshinda pamoja na
kwamba CCM ina wajumbe wengi zaidi katika Halmashauri hiyo!
10. UONGO WA KUMI
Mheshimiwa Spika,
Waziri Mkuu
aliulizwa swali la nyongeza na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kama
Serikali iko tayari kuunda tume ya uchunguzi ya kimahakama kutafuta ukweli wa
matukio ya Arusha na “... vile vile kuchukua hatua kwa wale
wanaohusika.” Swali hilo liliulizwa pia na
Mheshimiwa Martha J. Umbulla aliyetaka kujua kama Serikali itachukua hatua
kuwaadhibu CHADEMA kwa kile alichokiita kuhusika na vurugu za Arusha “...
ili tukio kama hilo
lisirudie katika chaguzi za nchi yetu?” Waziri Mkuu alijibu: “Mimi
nadhani hili ... wala si suala pengine la kusema ichukue hatua dhidi ya CHADEMA
hapana.” Waziri Mkuu alitilia mkazo kwamba Serikali haina mpango wa
kuwachukulia hatua CHADEMA kwa kusema: “Nataka niwaombe sana,
hili hatuwezi kama Serikali tukasema
tutaichukulia hatua CHADEMA....”. Angalia hansard ya tarehe 10-02-2011
kielelezo “G”
Mheshimiwa Spika,
Watanzania
wawili na raia wa nchi jirani na yenye uhusiano mzuri na nchi yetu waliuawa
wakati wa vurugu za Arusha. Watu wengine wengi walijeruhiwa kwa kupigwa risasi,
mabomu, virungu na mabuti ya polisi. Kama taarifa za Jeshi la Polisi na kauli
ya Waziri Mkuu ni za kweli, vurugu hizo zilihusisha pia mashambulizi na
uharibifu wa mali za Serikali kama vile vituo vya Polisi na mali za watu
binafsi na za vyama vya siasa hususan CCM. Aidha, kama
kauli ya Jeshi la Polisi nay a Waziri Mkuu ni za kuaminiwa, madhara yote haya
yalitokana na uchochezi uliofanywa na viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA na
ambao wametajwa kwa majina.
Mheshimiwa Spika,
Kama yote haya ni ya kweli na sio porojo za kisiasa,
Watanzania wanapaswa kuambiwa ni kwa nini Serikali hii haiko tayari
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika na matukio haya? Kwa nini
Serikali imeamua kwamba ni busara kuwafungulia mashtaka ya kosa dogo la kufanya
maandamano kinyume cha sheria badala ya kuwashtaki kwa makosa makubwa kama kusababisha mauaji, au uchochezi, au kujaribu
kuchoma majengo moto au makosa ya aina hiyo ambayo yana adhabu kubwa zaidi ya
kosa waliloshtakiwa nalo? Kukataa kuchukua hatua stahili kuna tafsiri moja tu:
CHADEMA hawakuhusika katika vurugu za Arusha na kwa hiyo kauli ya Waziri Mkuu
Bungeni ni ya uongo na yenye lengo la kulidanganya Bunge!
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Kanuni ya
63(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, inasema “… ni
marufuku kabisa kusema uongo Bungeni na kwa sababu hiyo, Mbunge yeyote
anapokuwa akisema Bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au
maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli na
siyo jambo la kubuni au la kubahatisha tu.” Hii pia ni msingi wa kanuni
ya 64(1)(a) ya Kanuni za Bunge.
Kama nilivyothibitisha katika maelezo haya, Waziri
Mkuu amesema uongo na/au kutoa taarifa ambazo hazina ukweli Bungeni. Kanuni ya
63(5) inaelekeza cha kufanya inapothibitika kuwa Mbunge amesema uongo Bungeni:
“Spika au Mbunge mwingine yeyote, baada ya kutoa maelezo mafupi ya ushahidi
unaotilia mashaka ya dhahiri kuhusu ukweli wa kauli au usemi au maelezo juu ya
jambo au suala ambalo Mbunge amelisema Bungeni, anaweza kumdai Mbunge huyo atoe
uthibitisho wa ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake na kama atashindwa
kufanya hivyo, afute kauli au usemi au maelezo yake hayo.” Naomba
kuchukua nafasi hii kumtaka Waziri Mkuu atoe uthibitisho wa ukweli wa kauli au
usemi au maelezo yake Bungeni siku ya tarehe 10 Februari 2011 na kama atashindwa kufanya hivyo, afute kauli au usemi au
maelezo yake hayo na kutubu kwa Mungu!
Mheshimiwa
Spika, naomba kuwasilisha!
Godbless
Jonathan Lema
Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini
Josh Nassari
Scholarship Program Director
The Foundation For Tomorrow
P. O. Box 119
Duluti-Arusha.
www.thefoundationfortomorrow.org
+255 784 225 758
Men anpil chay pa lou. (Haitian proverb)
Many hands make the load lighter.