Ndugu wanaharakati,
Kwa kifupi nadhani nami pia nitoe walau kero ambayo kwangu naona imekuwa ikinisumbua sana, pamoja na majibu ya WM, mimi naomba tujadili hoja yangu hii.
Wabunge wetu wakati wanapoomba sisi wananchi tuwachague, hupenda kutumia kauli kuwa wanaomba tuwatume Bungeni ili watutumike, kwa lugha hii, nadhani mwajiri wa Mbunge ni Mwananchi yaani mimi na wewe.
Sasa hoja yangu inakuja hivi, hivi wewe kama umeomba nafsi ya kazi ili utumikie Umma, kupitia Taasisi X au B, je wewe mwomba kazi unauwezo wa kujipangia mshahara na posho?
Hivi hawa wabunge ambao sisi wananchi tunawachagu inakuwaje wao wakiwa Bungeni wanajipangia mishahara na posho halafu ajira yao ya
kipindi cha Miaka mitano inapoisha, hurudi tena kwetu na kusema naomba ndugu wananchi mnitume Bungeni ili niweze kuwatumikia na sisi bila kuhoji mambo mhimu kama haya tunawarudisha tena Bungeni,
Unajua kwangu haiingii akilini kabisa, yapo mambo ambayo ukiyatazama utaona kabisa hayaingii akilini, leo Mbunge anapokea mamilioni ya shilingi, Madiwani nao wanapokea kiduchu tu, huku watendaji wa Kata na Vijiji wakiwa hawana ofisi kabisa, kuna sehemu moja nilimtembelea Afisa Mtendaji wa Kijiji nikakuta mbele ya Meza yake kuna kichuguu kikubwa nikamwuliza hivi kweli Bosi wako yaani Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya anaweza akdiriki kuja kukutembelea na akaingia katika ofisi hii akakaa na kutia sahihi kitabu cha wageni?
Hivi, leo, tumekuwa na pupa ya kuwachagua vijana ambao wametoka chuo Kikuu ati hao ndio wanaofaa kuwa wabunge, ( katika hili sina maana ya kupinga wasomi ati wasipewe nafasi) ila hapa najaribu
kujiuliza mnipe majibu kabisa, Kijana leo amemaliza chuo kikuu na kupta shahadaa yake ya kwanza, hicho kinakuwa kigezo kikubwa cha kupata ubunge wakati kijana huyu, kwanza akiingia Bungeni, laizma hesabu yake ya kwanza itakuwa kupigania maslahi ya posho na mishahara mikubwa ili alipe gharama zote ambazo wazazi wake walitumia katika kumsomesha yeye, pili atakuwa na hesbau za kuanza kujenga nyumba nzuri na kusaidia familia yake. Ndio maana Watanzania wengi wamekuwa na tabia ya kulalamika kuhusu hali ya maisha mara tu baada ya uchaguzi kumalizika, ikifika wakati wa upigaji kura tunakwenda likizo kimaamuzi.
Kwa ndugu zetu Waamerika, wao wana taratibu nzuri, elimu haiwi kigezo cha cha kwanza cha kupata madaraka, bali kwanza hujifunza huyu anayengombea madaraka tabia yake ilikuwa yanamna gani wakati alipokuwa yungali mtoto, alipokuwa pre-school, primary school na hata chuo Kikuu, iwapo itaonekana kwamba tabia na mwenendo wake
vilikuwa ovyo, basi kwa hali hiyo hawezi kufikiriwa hata kidogo, pia hali ya uwezo wa kiuchumi huangaliwa na mwisho ndipo elimu yake hufuata baada ya mchakato wa hayo yote mawili kuonekana kuwa amekidhi vigezo.
Pamoja na utamaduni tulionao kwamba tujenge taifa ambalo linalenga kuweka usawa kati ya wenye nacho na wasio nacho tuwe sawa nadhani hali hii ndio hupelekea kuwepo kwa ufisadi ambao hautaondoka kamwe.
Ndugu wanaharakati wenzangu, nadhani ipo haja kwamba katika siku zijazo na hata sasa, Waziri Mkuu ambaye ndiye Mkuu wa shughuri za Serikali Bungeni pamoja na waziri wa Uratibu Sera na Bunge, waweke utaratibu kuwa Kila Wabunge anapohitaji kuongezewa Posho na mishahara yao, basi iandaliwe White Paper ipitishwe kwa waajiri wao ambao ni sisi wapiga kura, na wanapiga kura ( wananchi) ndio watoe uamuzi wa ni kiasi gani ambaocho wabunge walipwe. Kwa kweli kwangu
naona wabunge wengi hawana uzalendo kabisa haswa unapoona mbunge analipwa mamilioni ya shilingi huku Polisi, Hospitali zetu, Walimu, watoto wa shule za msingi na hata Vyuo vikuu wakiwa katika mazingira mabaya na hata watoto wetu kuishia kukaa mavumbini katika karne hii, nawaapia hao wabunge siku ya mwisho Mungu atawaulizia kama waliwatendea haki wale waliowachagua, msijifuahishe kwa kutinga katika mashangingi mazuri mazuri mkadhani huo ndio mwisho siku ya Mungu inakuja mtajibu hata kama raia hawatachuku hatua.
Naomba Mwaka 2015, wananchi mchukue hatua na hasa katika kipindi hiki tunapoelekea kufanya mabadiliko makubwa ya katiba ya Nchi. Mbunge au Wabunge wasijipangie mishahara au posho. Vinginevyo nafasi ya Ubunge itakangazwe kama nafasi ya ajira.
Nawatakia mjadala mwema katika hili.
Asante
William Daudi Program Office TWSEDHRO Kigoma Tanzania
|