“ZIPO baadhi ya kampuni za migodi ya madini nchini zinafanya
kazi zake kwa kukiuka sheria za mazingira. Mafuta hayapaswi kumwagwa
eneo lisilokuwa limeandaliwa kitaalamu.”
Hiyo ni kauli ya Ofisa Mwandamizi wa Mazingira kutoka Timu ya
Uchunguzi ya Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC), Dk. Yohana Mtoni.
Dk. Mtoni ametoa kauli hiyo alipokutana na waandishi wa habari.
Akitoa ripoti ya ukaguzi uliofanywa na NEMC katika migodi tisa iliyopo
mikoa ya Kanda ya Ziwa, kuanzia Agosti 25, mwaka huu anasema imeonesha
kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira unaofanywa na baadhi ya kampuni za
migodi ya madini.
Dk. Mtoni anasema kupitia ripoti hiyo wamebaini ukiukwaji wa sheria za mazingira.
Anasema baadhi ya migodi hiyo inajihusisha na umwagaji ovyo wa mafuta
na kemikali pamoja na utunzaji mbovu wa dawa zenye kemikali.
Uchafuzi mwingine wa mazingira unaofanyika ni utupaji wa taka ngumu,
kushindwa kudhibiti majitaka yasiyosafishwa, mitaro inayotiririsha maji
ya kemikali kutoka kwenye mabwawa ya majitaka kutokujengwa kitaalamu ili
kuzuia kemikali kuingia ardhini na umwagaji ovyo wa maji yenye kemikali
bila kuzingatia usalama wa mazingira.
Kutokana na hali hiyo, NEMC imelazimika kuchukua hatua kali za
kisheria dhidi ya migodi saba mikubwa, kwa kuitoza faini ya sh milioni
450 kutokana na kukiuka sheria za mazingira.
Dk. Mtoni anaitaja migodi iliyobainika na uchafuzi wa mazingira
kinyume cha sheria za nchi ni North Mara-Nyamongo, GGM na Buzwagi.
Migodi mingine ni Bulyanhulu, El-Hillal, Tulawaka na mgodi wa Resolute.
Uongozi wa GGM umesema utafanya mazungumzo ya wazi baina yake na serikali na NEMC juu ya faini hiyo.
Sheria hizi zinakataza uchafuzi wa mazingira. Na zinaamuru mtu au
kampuni kukamatwa na kuamliwa kulipa faini ya fedha ama kuhukumiwa
kifungo jela.
Si hilo tu, Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 nayo inasema:
Udumishaji, usalama na matumizi sawa ya rasilimali kwa mahitaji ya
msingi ya sasa na ya vizazi vijavyo, bila kuharibu mazingira au
kuhatarisha afya na usalama.
“Kuzuia na kudhibiti uharibifu wa ardhi, maji, mimea na hewa ambayo
ndiyo husaidia mfumo wa uhai wetu, kuhifadhi na kuendeleza urithi wetu
na ule unaotengenezwa na binadamu, ikiwa ni pamoja na maisha ya viumbe
wa aina mbalimbali na vya pekee nchini Tanzania.”
Tangu mwaka 1997 serikali ilipotunga Sera hii ya Taifa ya Mazingira,
hatua mbalimbali zimechukuliwa na serikali, mashirika, taasisi na asasi
kuhusu udhibiti na utunzaji wa mazingira.
Ninapozungumzia uchafuzi wa mazingira katika maeneo yetu ya makazi na
sehemu za kazini, namaanisha kwamba tunaweka rehani maisha yetu na ya
vizaji vijavyo, iwapo kila mmoja wetu hataamua kutunza mazingira.
Katika kupambana na hali hii ovu, lazima serikali kupitia idara zake
za kudhibiti uchafuzi wa mazingira kama vile NEMC, LVEMP pamoja na Ofisi
ya Makamu wa Rais (Mazingira), itumie vema sheria zake kuwaadhibu watu
au kampuni yanayokiuka sheria za nchi.
Ubutu wa matumizi ya sheria za mazingira, ndicho chanzo ninachokiona
mimi kinachochea hali hii ya uchafuzi wa mazingira, maeneo mbalimbali ya
nchi yakiwamo maeneo ya migodini.
Hatua zilizochukuliwa na NEMC dhidi ya kampuni hizo za migodi zisiishie hapo.
Ofisa Mazingira kutoka NEMC, Paul Kalokola, anasisitiza: “Licha ya
kampuni hizo saba za migodi ya madini kuamliwa kulipa fedha, lakini ipo
migodi mitatu tumeipa muda wa miezi mitatu kuweka mfumo mzuri wa
utunzaji wa mazingira, la sivyo hatua kali zaidi za kisheria
tutazichukua.”
Anaitaja migodi hiyo kuwa ni GGM, Bulyanhulu na Buzwagi. Na kwamba
migodi hiyo itakuwa chini ya uangalizi wa muda huo na ikishindwa
kutekeleza maagizo ya NEMC lazima hatua za kisheria zaidi zichukuliwe
pasipo kuogopa ukubwa wa kampuni.
“NEMC na serikali kwa ujumla hatukubali hali hii, lazima tuchukue
hatua za kisheria kali sana kwa wachafuzi wa mazingira,” anasisitiza
Kalokola.
Ili Tanzania iweze kushinda vita hii ya uchafuzi wa mazingira lazima
uwepo usimamizi na utekelezwaji thabiti wa mikataba mbalimbali ya
kimataifa.
Katika mikataba hiyo, serikali yetu imeweka saini mikataba kadhaa ya mazingira na kuridhia makubaliano na nchi mbalimbali.
Kuna mapatano kwa ajili ya hifadhi, usimamizi na maendeleo ya
mazingira ya bahari na mwambao wa Afrika Mashariki, pamoja na itifaki
zinazohusika na mapatano hayo yaliyofikiwa Machi mosi 1996.
Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaohusu mfumo wa mabadiliko ya hali ya hewa ulisainiwa Aprili, 1996.
Makubaliano ya Vienna ya kuhifadhi tabaka la ozoni na makubaliano ya
Montreal juu ya vitu vinavyoharibu tabaka la ozoni yaliyosainiwa Aprili
7, 1993 na Aprili 16, 1993.
Mingine ni Mkataba wa Basley wa kudhibiti kusafirisha nje ya mipaka
dawa zenye hatari na jinsi ya kuyateketeza uliowekwa saini Aprili 7,
mwaka 1993; pamoja na makubaliano ya Bamako juu ya kuzuia kuingiza
Afrika na kudhibiti kusafirisha nje ya mipaka dawa zenye hatari katika
Afrika yaliyofikiwa Aprili 7, 1995.
Kwa mikataba hii ya kimataifa iliyoridhiwa na serikali iwapo watawala
watatekeleza vema wajibu wao, ikiwa ni pamoja na kuzichukulia hatua kali
za kisheria kampuni, taasisi, asasi, mashirika na watu binafsi
wanaochafua mazingira, hakika Tanzania itang’ara ulimwenguni kwa
kudhibiti uchafuzi huo wa mazingira.