Habari ambazo Mtaa kwa Mtaa imezinasa kutoka katika vyanzo vya
kuaminika na kwa waandishi wa habari wa kimataifa waliokuwa
wakifuatilia mkutano huo zinaeleza kwamba, wawakilishi wa vyama hivyo
waliofika hapa nchini kufuatilia mkutano huo wamekuwa wakisaka
mawakala ambao watasimamia shughuli za vyama vyao hapa nchini.
Kwa mujibu wa habari hizo, mashoga hao ambao walikuwa hapa nchini
wakiwakilisha vyama vyao, kwa lengo la kushinikiza kuendelea
kutambuliwa ndani ya Kanisa la Anglikana, wanafanya hivyo ili
kuanzisha shughuli za kijamii kama wanavyofanya katika mataifa kadhaa
yaliyoendelea duniani.
Vyanzo vya kuaminika vya habari vilivyo karibu na mashoga hao,
vinaeleza kwamba matawi hayo yanakusudiwa kuanza kufanya kazi Dar es
Salaam na visiwani Zanzibar.
Iwapo azima yao hiyo itafanikiwa, basi Tanzania inaweza ikaanza
kushuhudia kustawi kwa taasisi za kishoga ambazo zitakuwa zikipokea
ufadhili wa mamilioni ya fedha kutoka katika vyama tajiri vilivyoko
Ulaya na Marekani.
Habari za uhakika zilizoifikia Tanzania Daima kutoka kwa baadhi ya
washiriki wa mkutano mkuu wa Kanisa la Anglikana duniani uliomalizika
siku mbili zilizopita katika Hoteli ya White Sands, Dar es Salaam,
zimeeleza kuwa tayari viongozi wa mashoga hao wamekwisha kuteua
mawakala wao nchini.
Habari hizo zimeeleza kuwa mawakala hao ndio watakaokuwa wakipokea
pesa za misaada kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii hapa
nchini.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, kabla ya kuwapata mawakala hao, mitandao
ya mashoga hao awali ilitaka kuanza kuzituma fedha hizo kwa ajili ya
ujenzi wa shule na hospitali kupitia Kanisa la Anglikana, kabla wazo
hilo kuonekana kugonga mwamba.
Chanzo kimoja cha habari kinaeleza kuwa, mashoga tajiri wa Canada na
Marekani wamekuwa wakifungua mitandao ya namna hiyo katika nchi
mbalimbali duniani kwa malengo ya kuendeleza harakati za kutaka
kutambuliwa na kukubalika kimataifa.
Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kuwa kiongozi mmoja wa Kanisa la
Anglikana nchini, ameonekana akiwa miongoni mwa mawakala ambao ndio
watakaoendeleza harakati hizo hapa nchini.
"Wanataka kuleta pesa za msaada kama njia ya kufanikisha azima yao,
lakini kupitia katika kanisa, kitu ambacho kanisa linakipinga,"
kilieleza chanzo hicho.
Habari zaidi zinasema kuwa, hata hivyo viongozi kadhaa wa kanisa hilo
hapa nchini wamepinga vikali mipango yoyote ya kushirikiana na vyama
vyenye mrengo wa kishoga, kitendo wanachokielezea kuwa ni kulivuruga
kanisa.
Ushoga umekuwa ni ajenda kubwa inayoligawa Kanisa la Anglikana duniani
tangu mwaka 2004, baada ya Dayosisi moja nchini Marekani kumtawaza
Gene Robinson, ambaye ni shoga kuwa askofu.