Yanga watawaweza realmadrid

1 view
Skip to first unread message

Fusha

unread,
Feb 20, 2007, 8:25:16 AM2/20/07
to Mtaa Kwa Mtaa
KLABU ya Yanga, inakusudia kuzungumza na serikali kupitia Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), kuangalia uwezekano wa kuinunua moja ya mechi
za Real Madrid kama mchango wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kamati ya mpito ya klabu
hiyo, Yanga imeamua kufanya hivyo ukiwa ni mchango wake katika
maendeleo ya soka nchini, kwani Yanga ni sehemu ya maendeleo hayo.

"Uongozi wa Yanga, utawasiliana na serikali kupitia Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), kuona uwezekano wa Yanga kama mchango wake kwa kununua
mechi moja wakati wa ziara ya Real Madrid," ilisema taarifa hiyo.

Aidha, katika taarifa hiyo iliyotiwa saini na Francis Kifukwe, Yusuf
Mzimba na Kibo Merinyo, mkakati wa klabu hiyo, ni kuona Yanga
inang'ara kisoka.

"Katika kipindi hiki tutajitahidi kuhakikisha Yanga inakuwa tishio
katika michuano mbalimbali iliyo mbele yetu ya kitaifa na kimataifa,"
ilisema taarifa hiyo.

Viongozi hao pia wametoa shukrani kwa wanachama wa klabu hiyo kwa kuwa
watulivu kwa kipindi cha mchakato wa kusaka suluhu ya kumaliza mgogoro
wa klabu hiyo.

"Tunawaomba wanachama wote wawe watulivu na kuendeleza hali ya umoja
na mshikamano katika kipindi hiki cha mpito katika kuelekea uchaguzi
mkuu," ilisisitiza taarifa hiyo ya pamoja.

Sambamba na hilo, kamati hiyo imempongeza mfadhili wa klabu hiyo,
Yusuf Manji, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanachama wa
klabu hiyo wanakuwa kitu kimoja.

"Ni ukweli usiopingika kuwa, mazuri yote haya ndani ya Yanga, ni
juhudi za Yusuf Manji. Tumefika hapa tulipo sasa kwa jitihada kubwa za
mfadhili wetu Manji," ilisema kamati hiyo.

Aidha, kamati hiyo ya mpito, ilitoa shukurani kubwa kwa kamati maalumu
iliyokuwa ikiratibu rasimu hiyo ya muafaka na uuzwaji wa hisa kwa kazi
kubwa hadi kufanikisha suala hilo.

Waliokuwamo kwenye kamati hiyo ni Lucas Kisasa, George 'Castro'
Mpondela na Ismail Idriss. Katika rasimu hiyo, imekubaliwa kuwa
wanachama wote wana haki sawa.

Kuhusu hisa, viongozi hao wamesema baada ya kukamilika mchakato wa
hisa za klabu hiyo, zitakuwa zikiuzwa kupitia Benki ya CRDB.

Taarifa hiyo, imekuja siku moja tangu makundi matatu ya klabu hiyo
yaliyokuwa yakivutana, kwa nyakati tofauti juzi kupitisha rasimu ya
kumaliza mgogoro na suala la uuzwaji wa hisa.

Makundi hayo ni Kampuni, Asili na Academia, ambayo Juni 22 mwaka jana,
yalifikia muafaka ambao kwa sasa uko katika utekelezwaji wake.

Rasimu hiyo inakwenda kuzika mgogoro wa kikatiba ulioisumbua klabu
hiyo kwa zaidi ya miaka saba, kwa kila kundi kudai ndilo lenye haki
kuliko jingine.

Reply all
Reply to author
Forward
0 new messages