Mbinu zilizobuniwa na wafanyabiashara hao ni pamoja na kuweka bidhaa
kwenye mifuko ya rambo na mikoba na kuziuza ofisini, katika baa na
kumbi mbalimbali za starehe.
Nyingine zinazotumiwa na mama lishe ni kuweka vyakula kwenye ndoo na
kuviuza katika vituo vya mabasi na daladala, ofisini na katika baadhi
ya maeneo yasiyoruhusiwa. Mbinu hizo zinaonekana kuwapiga chenga
mgambo wa Jiji zaidi ya 100, waliotapakaa katika maeneo mbalimbali ya
jiji kwa lengo la kudhibiti wafanyabiashara hao kutorejea katika
maeneo hayo baada ya kutimuliwa mwaka jana.
Baadhi ya wafanyabiashara hao walisema kuwa waliamua kubuni mbinu hizo
waweze kupata wateja wakidai kuwa maeneo waliyohamishiwa hayafikiwi na
wateja kwa urahisi na hivyo kuwakosesha mapato.
Walisema kuwa maeneo ya Kiloleli, Buzuruga na Nyegezi walikohamishiwa
hayafikiwi na wateja kutokana na kukosa huduma muhimu za jamii kama
vile maji, umeme na barabara hasa katika eneokama la Kiloleli.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Emmanuel Kalobelo, alisema hakuwa
na taarifa hizo za wamachinga kubuni mbinu mpya na aliahidi
kuwashughulikia mara moja.
Kalobelo alitoa mwito kwa wakuu wa taasisi na idara mbalimbali za
Serikali jijini hapa, kuzuia uuzaji wa bidhaa na vyakula unaofanywa
holela na wamachinga na mama lishe hao akisema kuwa watazifanya ofisi
na taasisi hizo kutumika kinyume na majukumu yake ya kuhudumia
wananchi.
"Niwaombe basi wakuu wetu wa idara waunge mkono juhudi za Serikali na
halmashauri kwa kutorutubisha biashara za wamachinga na mama lishe
kwenye ofisi za Serikali. Ni bora wakawafuata kwenye maeneo
yaliyotengwa kisheria," alisema