Waliopania kumshitaki Dk. Slaa waendelea kujiandaa?

4 views
Skip to first unread message

mcha...@googlemail.com

unread,
Oct 9, 2007, 10:22:29 AM10/9/07
to KULIKONI TANZANIA

Waliopania kumshitaki Dk. Slaa waendelea kujiandaa?

na Happiness Katabazi


HADI jana hakuna hata mmoja miongoni mwa watu waliotajwa wakituhumiwa
kuwa ni mafisadi, aliyekuwa ametekeleza azima ya kumfungulia mashitaka
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa.

Watu hao, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Katibu
Mkuu katika Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, na Patrick Rutabanzibwa,
walishatangaza azima yao ya kumfungulia Dk. Slaa mashitaka kwa madai
kuwa alikuwa amewakashifu kwa kuwatuhumu kuwa ni mafisadi.

Akihutubia umati uliofurika katika mkutano wa hadhara katika viwanja
vya Mwembeyanga, Dk. Slaa alitoa orodha ya watu 11 aliowatuhumu kuwa
ni mafisadi na wabadhirifu wa mali ya umma.

Uchunguzi uliofanywa na 'Tanzania Daima' kuanzia Septemba 18 hadi jana
katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu na mahakama za wilaya jijini hapa, umegundua
kwamba hakuna hata mmoja aliyekwishatekeleza azma hiyo.

Siku chache baada ya Dk. Slaa kutaja majina hayo, baadhi ya watuhumiwa
hao walikana tuhuma hizo na kusema ni za uongo na kuahidi kumfungulia
kiongozi huyo kesi ya kashfa kwani amewachafulia majina.

Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM),
alishasema wazi kuwa hatomshitaki Dk Slaa, wakati Waziri wa
Miundombinu, Andrew Chenge, alisema kwamba tuhuma hizo ni utumbo mtupu
na hakusema atamfikisha mahamakani.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari, Karamagi alisema kuwa
atafungua kesi hiyo katika kipindi kisichozidi saa 48, lakini ni zaidi
ya wiki sasa na bado hajatekeleza azma yake.

Alipoulizwa na gazeti hili wiki iliyopita, alisema bado dhamira yake
ipo pale pale na alikuwa anajiandaa kufungua kesi hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliliambia gazeti hili kuwa suala hilo ni
gumu kutokana na mtego uliowekwa na Dk Slaa, ambaye hajaweka bayana
aina ya ushahidi alionao dhidi ya watu anaowatuhumu.

"Hata wao waliotuhumiwa wana hofu kuwa iwapo suala hili litafikishwa
mahakamani, kuna uwezekano wa mambo mengine mengi kufichuka na kuzidi
kuwagandamiza," alisema mwanasheria mmoja ambaye hakupanda jina lake
litajwe gazetini.

Hata hivyo, wakili mwingine, Robert Rugemalila, alisema kitendo cha
watuhumiwa hao kushindwa kwenda mahakamani hadi sasa kinaleta hisia
kwa wananchi kuwa huenda tuhuma zilizotolewa na Dk. Slaa zina ukweli
ndani yake.

"Hawa wana uwezo wa kifedha wa kuweka wanasheria wazuri wa kuendesha
kesi zao...sasa ni kitu gani kinachowakwamisha hadi kumfikisha
mahakamani Dk.Slaa wanayesema amewachafulia majina yao?

"Haiingii akili kabisa mtu akuvunjie heshima na kukuchafulia jina
mbele ya jamii halafu ukae kimya na ushindwe kumpeleka mahakamani, kwa
hili serikali na watuhumiwa hao wanawahaada wananchi," alisema
Rugemalila.

mcha...@googlemail.com

unread,
Oct 10, 2007, 2:25:25 PM10/10/07
to KULIKONI TANZANIA
Waziri aliyetuhumiwa ufisadi adai fidia ya Sh10bilioni
Na Muhibu Said

WAZIRI wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ametoa siku mbili kwa
Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama
hicho, Tundu Lissu, wamwombe radhi na kumlipa Sh10 bilioni zikiwa ni
fidia ya kuchafuliwa jina kwa kuhusishwa na ufisadi.

Hata hivyo, kumbukumbu za notisi ya kusudio la kufungua mashtaka
iliyoandikwa na mawakili wa Kampuni ya FK Law Chambers ya jijini Dar
es Salaam wanaomwakilisha Waziri Karamagi, zinaonyesha kuwa muda ambao
waziri huyo ametaka aombwe radhi na Dk Slaa na Lissu ulishapita tangu
Septemba 26, wakati ule wa kulipwa kiasi hicho cha fedha uliisha
Oktoba Mosi, mwaka huu.

Notisi hiyo yenye Kumbukumbu Na. FK/CF/NMK/DN/, iliyosainiwa na
mwanasheria wa kampuni hiyo, Joseph Ndazi, iliandikwa Septemba 24,
mwaka huu na kumtaka Dk Slaa na Lissu kuomba radhi kwa maandishi ndani
ya siku mbili na kumlipa kiasi hicho cha fedha ndani ya siku saba,
kuanzia tarehe ya notisi hiyo.

Mbali na kuwataka kutekeleza mambo hayo, mawakili hao wamewataka Dk
Slaa na Lissu katika notisi hiyo, kukiri kwamba tuhuma walizozitoa
dhidi ya mteja wao hazikuwa sahihi na hazikuwa na ukweli wowote na
wakiri hivyo kwa kuchapisha kwenye magazeti yenye mtandao mkubwa wa
usambazaji.

Pia watoe ahadi ya maandishi kwenye magazeti kwamba, wataacha mara
moja kuchapisha taarifa zenye maneno yasiyokuwa ya kweli au yenye
kashfa dhidi ya Karamagi, familia na washirika wake na walipe Sh10
bilioni kwake, au kupitia kwa mawakili wake, kama fidia ya madhara
yote waliyomsababishia mteja wao.

Vilevile, mawakili hao wamemtaka Dk Slaa na Lissu wamlipe Karamagi
gharama zote ambazo tayari ameshaingia na anazotazamia kuingia
kuhusiana na suala hilo.

"Kwa vile (Dk Slaa na Lissu) wamezungumza mambo yanayohusu jinai dhidi
ya mteja wetu ambayo si sahihi na ya kweli, mteja wetu anayo haki ya
kufungua malalamiko ya jinai dhidi yao katika vyombo vinavyohusika,"
ilieleza sehemu ya notisi hiyo ambayo nakala yake ilipelekwa kwa
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Mawakili hao wamedai kuwa kutokana na Dk Slaa na Lissu kutaja
hadharani tuhuma hizo dhidi yake (Karamagi), wamemsababishia madhara
mbalimbali, ikiwamo kudhoofisha heshima yake ya kitaaluma na nafasi
yake ya kisiasa kwa viongozi wa serikali ya Tanzania na wa kisiasa,
maafisa wa ngazi za juu wa serikali, marafiki, washirika wake na jamii
kwa ujumla.

Wamedai pia wamesababisha aonekane vibaya kwa washirika wake wa ndani
na nje ya nchi ambao sasa wanamkwepa.

"Kutokana na madhara waliyomsababishia mteja wetu, katika muda
usiozidi siku mbili, kuanzia Septemba 24, wamwandikie barua ya
kumwomba msamaha, pia wamwandikie barua ya kukiri kwamba tuhuma
walizozitoa dhidi ya mteja wetu hazikuwa sahihi na hazikuwa na ukweli
wowote na wakiri hivyo kwa kuchapisha kwenye magazeti yenye mtandao
mkubwa wa usambazaji.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake juzi, Lissu alisema notisi hiyo
aliipata juzi na kusema kuwa: "Kwa vile nimeiona leo (Oktoba 9, 2007)
na barua yenyewe ni ya Septemba 24 ni wazi nimeshachelewa sana
kutekeleza yale ambayo huyu bwana (Karamagi) anadai niyafanye. Na
mpaka sasa hivi sijaletewa hati yoyote ya madai".

Walipoulizwa na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, wanasheria wa FK
Law Chambers, kila mmoja alimtupia mpira mwenzake na mwisho suala hilo
wakalirudisha kwa Karamagi wakimtaka mwandishi amuulize iwapo kuna
hatua zozote ambazo zimekwishachukuliwa tangu wawaandikie notisi hiyo
Dk Slaa na Lissu.

Ndazi alikiri kusaini notisi hiyo, lakini akakataa kuzungumzia suala
hilo na kumtaka mwandishi awasiliane na mwanasheria mwenzake wa
kampuni hiyo, Profesa Luoga.

Hata hivyo, Profesa Luoga alitoa udhuru kwamba, muda mrefu hayuko
ofisini, hivyo, hafahamu kinachoendelea na kumtaka mwandishi
awasiliane na mwenzao aliyemtaja kwa jina moja la Danka, akisema
kwamba ndiye anayeshughulikia suala hilo.

Danka alipoulizwa alikataa badala yake alimtaka mwandishi akamuulize
Waziri Karamagi kwa kuwa ndiye mhusika mkuu wa suala hilo.

Naye Waziri Karamagi alipoulizwa alikataa kuzungumzia suala hilo,
akisema kwamba yeye si mwanasheria na kusema kwamba wanaopaswa
kuulizwa suala hilo ni wanasheria wanaoshughulikia suala hilo.

"Waulize wao wenyewe, mimi siyo lawyer (mwanasheria), wao ndio
wanaojua" alisema Karamagi ambaye alipoelezwa na mwandishi kuwa
wanasheria hao ndio walioelekeza aulizwe yeye, alimtaka awaambie
wanasheria hao kuwa wamweleze kinachoendelea.

Kwa upande wake, Dk Slaa, ametoa msimamo akisema hawezi kuomba radhi
wala kulipa fidia na kuwataka watuhumiwa kwenda mahakamani.

Akizungumza juzi usiku kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika
(VoA), Dk Slaa alisema hawezi kufanya hivyo na kwamba ni vema
watuhumiwa waende mahakamani.

Dk Slaa alifafanua kwamba, kabla ya kuibua tuhuma hizo walikaa
wakazifanyia kazi kwa kina na mapana na kusisitiza kwamba wana
ushahidi.

"Kabla ya kuibua tuhuma hizi, nilikaa na wenzangu tukazifanyia kazi
kwa kina, sasa kama kuna watu wamekwenda mahakamani ni vizuri, suala
sijui la kuomba radhi, hilo kamwe siwezi kulifanya," alisisitiza
msimamo wake.

Alisema kama ni kuomba radhi yeye anaweza kufanya hivyo kwa wananchi
tu, lakini si mtu ambaye anajua ana tuhuma ambazo zina ushahidi.

"Kama ni kuomba radhi labda kwa wananchi tu, lakini siwezi kumwomba
radhi mtu ambaye najua ana tuhuma," alisema.

Dk Slaa akitoa msimamo huo wa kupinga kuomba radhi kwa Karamagi,
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Gray Mgonja, naye amezidi kumng'ang'ania
akisema mawakili wake wako katika hatua za kukamilisha taratibu kuona
namna ya kufungua kesi hiyo.

Mgonja aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kwamba, kamwe
hawezi kubadili msimamo huo na kwamba lazima amburuze Dk Slaa
mahakamani.

Alisema mawakili wake wanapaswa kupitia kwa kina tuhuma hizo, ili
waone namna watakavyoweza kufungua kesi itakayokuwa na mafanikio.

Mgonja alipoulizwa vipi mawakili hao wanachukua muda mrefu wakati yeye
ana uhakika tuhuma hizo ni za uongo, alijibu: "Mimi ndiyo nina uhakika
ni tuhuma za uongo, lakini wao wanapaswa kujiridhisha kwa kupitia kwa
makini tuhuma zenyewe".

Alipoulizwa tena kuhusu ushauri wa Jaji Mark Bomani, kutaka tuhuma
hizo ziishie nje ya mahakama, alisema: "Huo ni ushauri, hata upande wa
kwanza (yaani wa Dk Slaa), aliutoa kwamba zilikuwa ni za jumla mno,
nimeupokea lakini msimamo wangu uko pale pale".

Dk Slaa ambaye yuko Marekani alitoa msimamo wake wa kwamba watuhumiwa
wanapaswa kuendelea na kesi mahakamani, leo usiku Dk Slaa anatarajiwa
kufanya mahojiano maalumu katika kipindi maalum cha Sauti ya Amerika
ambayo yatatangazwa moja kwa moja.

Reply all
Reply to author
Forward
0 new messages