OFISI ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekiri uzembe
katika utendaji wake wa kila siku.
Hili limethibitishwa na Spika mwenyewe, Samuel Sitta, katika moja ya
habari za gazeti hili leo.
Uzembe huo umefanywa na sekretarieti ya Bunge hilo kwa kushindwa kumpa
barua rasmi ya kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge, Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA) kwa miezi mitano mfululizo.
Zitto, anatumikia adhabu hiyo tangu Agosti 14, mwaka huu, baada ya
kudaiwa na wabunge wenzake kuwa alilidanganya Bunge kuhusu utiaji
saini wa mkataba wa Buzwagi uliofanywa na Waziri wa Nishati na Madini,
Nazir Karamagi, jijini London Uingereza.
Kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa kumsimamisha, Zitto alilitaka Bunge
kuunda kamati teule ya kuchunguza suala hilo huku akisisitiza kuwa
mkataba huo ulisainiwa kinyume cha maagizo ya Rais Jakaya Kikwete
kusitisha utiaji saini wa mikataba mipya.
Wakati Rais Kikwete anaagiza hilo, pia alitangaza kwamba kwa sasa
serikali inadurusu mikataba ya madini iliyoingiwa awali.
Sote tunafahamu kuwa, adhabu iliyomkumba Zitto, ilitikisa nchi baada
ya kambi ya upinzani kulifikisha hili mbele ya wananchi, wakiamini wao
ndio wenye mamlaka ya kuchagua mchele na chuya.
Kwa maana hiyo basi, Sitta anakiri kuwa ndani ya Bunge tukufu kuna
uzembe ambao kwa namna moja ama nyingine ameshindwa kuutafutia tiba.
Tunasema ameshindwa kwa kuwa alikiri hadharani kwamba uzembe wa
sekretarieti umesababisha Zitto kutopewa barua rasmi kwa wakati,
kinyume cha taratibu za kiofisi.
Ikumbukwe kuwa ni zaidi ya miezi miwili sasa tangu kusimamishwa kwa
mbunge huyo.
Ni wazi kuwa adhabu hiyo inawanyima uwakilishi mzuri wapiga kura na
wananchi wa Kigoma Kaskazini, tofauti na matarajio yao.
Lakini, msingi wa maoni yetu ni namna ambavyo Bunge linavyoshindwa
kuwajibika kwa masuala ya msingi kama haya.
Inakuwaje ofisi nzito na moja ya mhimili wa utawala kushindwa kuandika
barua ya kikazi isiyozidi dakika 45, bila sababu za msingi kuelezwa.
Kwa vipi tuuamini utendaji wa watumishi hao ilhali barua ya kumjulisha
mhusika kuwa amesimamishwa kutokana na sababu ya kulidanganya Bunge
inashindikana kuandikwa kwa zaidi ya miezi miwili sasa?
Tunaamini kuwa Spika ana uwezo wa kumwajibisha yeyote anayeshindwa
kutimiza wajibu wake na kusababisha aibu ndani ya chombo hicho muhimu
cha kutunga, kurekebisha na kupitisha sheria za nchi.
Nini maana ya uzembe huu? Nani wa kuwajibika iwapo Spika anakiri
uzembe ndani ya Bunge huku akishindwa kubainisha hatua madhubuti
atakazochukua kuhusu hili?
Tunalazimika kutilia shaka utendaji wa Sekretarieti ya Bunge letu na
wote wanaohusika ndani yake.
Iwapo inashindikana kuandika barua, ni vipi katika masuala makubwa
yenye masilahi kwa taifa yanayoamuliwa na wabunge?
Katika hili tunashawishika kuamini kwamba, uzembe unaofanywa na chombo
kikubwa zaidi ndani ya Bunge unatokana na kufanya kazi kidugu,
kulindana, kujuana au pengine kuogopana.
Tunasema chombo kikubwa kwa sababu, baada ya wabunge kufanya maamuzi
ya jambo Fulani, kazi inabaki kwa sekretarieti kuliweka jambo lile
katika maandishi na kulifikisha linapohusika.
Maana ya uzembe huu ni kwamba, yapo mambo mengine ambayo
hayajatekelezwa kwa sababu za uzembe kama huu.
Tunafahamu uzembe kazini ni jambo linalorudisha nyuma maendeleo na
wakati mwingine husababisha rushwa na wanyonge kunyimwa haki zao.
Huu ni urasimu unaopigwa vita kila kukicha. Hivyo basi, tunamtaka
Spika kuliweka hili bayana, ili kuondoa ukakasi wa uzembe huu.
Udhaifu katika utendaji huondoa imani ya wananchi kwa viongozi wao na
kushusha heshima ya Bunge.