na Chris Mang'era
KAMPUNI ya kitalii ya Foxtrot Charlie Limited (FCL), ambayo imeomba
ardhi kwa ajili ya kujenga hoteli mbili za kitalii, imejitambulisha
rasmi kwa uongozi wa Wilaya ya Tarime.
Wiki tatu zilizopita, kampuni hiyo iliomba eneo la kujenga hoteli
mbili za kitalii katika Kijiji cha Gibaso, wilayani humu na ombi hilo
limeshakubaliwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCL, Tim Corfield, akiwa ameambatana na Ofisa
Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Gibaso, Titus Mwera, jana alifika ofisini
kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Stanley Kolimba, kujitambulisha.
Corfield na Mwera walimweleza Kolimba kuwa wakazi wa kijiji hicho
wameshapokea na kulikubali ombi la kuipatia kampuni hiyo eneo kwa
ajili ya ujenzi wa hoteli mbili za kitalii katika kijiji hicho kilicho
takriban kilometa sita magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
(SENAPA).
Kwa mujibu wa barua ya kuomba eneo hilo iliyosainiwa na Corfield,
kampuni hiyo yenye makao yake makuu mjini Arusha, inaomba kumilikishwa
ekari kadhaa za ardhi kijijini hapo, ili kujenga hoteli mbili kwa
ajili ya kuendesha biashara za kitalii, ukiwamo utalii wa picha kwa
kipindi cha miaka 90.
Corfield alisema iwapo kila kitu kitakwenda vizuri katika makubaliano
ya kumilikishwa ardhi hiyo, Kampuni ya FCL itaanza kujenga hoteli hizo
Januari mwakani na kwamba hoteli moja itakuwa na vitanda 20 na
nyingine vitanda 10.
Katika barua hiyo, ambayo gazeti hili lina nakala yake, mwekekezaji
huyo ametoa ahadi za kuwainua wakazi wa Kijiji cha Gibaso kielimu na
kiuchumi, kuipatia serikali ya kijiji ada ya sh 12,000 kwa kila
kitanda kilichotumiwa na mgeni kwa siku na ada ya ardhi isiyopungua sh
milioni 3 kwa mwaka kwa ajili ya maendeleo ya wakazi wa kijiji hicho.
FCL imeahidi pia kutoa mchango usiopungua sh milioni 1 kila mwaka ili
kuboresha elimu ya msingi, kugharimia mafunzo ya wanakijiji sita
katika fani za ufundi magari, useremala, uashi, uhunzi, udereva,
ukatibu na uongozaji watalii na kwamba baada ya mafunzo hayo
itawaajiri kwa kipindi cha miaka mitatu.
"Tutaanzisha mfuko wa mikopo kwa ajili ya biashara ndogondogo kwa
wanakijiji, akisisitiza kuwa mikopo hiyo italenga zaidi biashara za
gereji, asali, ushonaji, kilimo cha mboga na matunda, useremala na
maduka ya ushirika.
"Biashara hiyo ya hoteli itahitaji uwanja wa ndege ili kurahisisha
ufikaji wa wageni na ada ya sh 10,000 itatozwa kwa kila ndege
itakayotua, pia familia zitakazoathirika kutokana na ujenzi wa uwanja
huo zitalipwa fidia kwa kiwango kitakachokubaliwa na pande zote
husika," alisema Corfield.
Kwa upande wake, Kolimba alisema amefurahishwa na uwekezaji huo
akisema utasaidia kupunguza umasikini na hivyo kupunguza vitendo vya
uhalifu wilayani hapa.
Kolimba aliahidi kuitisha kikao cha wataalamu wa masuala ya uwekezaji
na utalii wa wilayani hapa ili kuzungumzia zaidi suala hilo, huku
akisisitiza kuwa hakuna kitakachoikwamisha kampuni hiyo kuwekeza
katika Kijiji cha Gibaso iwapo itafuata masharti ya uwekezaji wa
kitalii.