CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake viko katika wakati mgumu,
vikipita katika tanuri la malalamiko dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa
maadili na hususan kukithiri kwa rushwa.
Kama ilivyo jadi yake ya miaka ya hivi karibuni, chama hicho tayari
safari hii tena kimejikuta kikipita katika kipindi kigumu kabisa cha
uhai wake wa miaka 30 tangu kianzishwe, na mtu wa mwisho kupigilia
msumari wa lawama ni kada wake wa siku nyingi, Joseph Butiku.
Kwa hakika, kile ambacho Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipata
kukielezea kuwa moja kati ya nyufa zinazoliandama taifa, yaani rushwa,
imeonekana kukiandamana chama hicho kwa namna ya ajabu.
Kukithiri kwa vitendo vya waziwazi vya rushwa katika uchaguzi wa chama
hicho ambavyo vilianza kujijenga taratibu ndani ya CCM na
kujidhihirisha kila nyakati za uchaguzi, safari hii dalili zinaonyesha
hali inazidi kuzotora na pengine kufikia hatua ya kukatisha tamaa.
Jambo baya zaidi ni kwamba, hivi sasa imefikia wakati baadhi ya makada
maarufu wa chama hicho, wakiwamo mawaziri nao wameingia katika orodha
ya wana CCM wanaoeleza waziwazi kulalamikia hali hiyo ya kukatisha
tamaa.
Kiongozi wa kwanza kueleza malalamiko yake hayo kabla ya kina Butiku
katika siku za hivi karibuni alikuwa ni Waziri wa Mipango, Uwezeshaji
na Uchumi, Dk. Juma Ngasongwa, ambaye alikuwa akigombea ujumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kupitia Mkoa wa Morogoro na kuanguka.
Baada ya Ngasongwa kutoa kauli hiyo, siku chache baadaye, Katibu Mkuu
wa zamani wa chama hicho, Philip Mangula na sasa Waziri wa Mambo ya
Ndani, Joseph Mungai, wote walisikika wakitoa matamshi hayo hayo ya
kulalamikia mwenendo wa rushwa katika chaguzi za chama hicho.
Malalamiko hayo ya makada maarufu wa CCM yanakuja wakati tayari
wanachama kadhaa na viongozi wa chama hicho katika maeneo mbalimbali
ya nchi hii wakiwa chini ya mkono wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Taarifa ya Kamati Kuu ya CCM iliyokutana miezi kadhaa iliyopita
ilieleza kuwa, kuingia kwa Takukuru katika kukabiliana na tatizo la
rushwa ndani ya chama hicho, kulikuja kwa maelekezo ya Mwenyekiti wa
Taifa wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa taarifa nyingine za uhakika kutoka ndani ya chama hicho,
uamuzi huo wa Kikwete kuishirikisha taasisi ya dola kukabiliana na
rushwa ndani ya chama tawala, ilipokewa kwa hisia tofauti na makada na
viongozi wengine kadhaa ndani ya chama hicho.
Ingawa gazeti hili liliipongeza Kamati Kuu ya CCM wakati huo kwa
uamuzi wake huo wa kukabiliana na rushwa, uamuzi wa Kikwete kuamua
kuwaita Takukuru kuingia ndani ya chama hicho kwa upande mwingine
ulionyesha kushindwa kwa mbinu zote za kichama za kukabiliana na
tatizo la ufisadi ndani yake.
Kwa maelezo yoyote yale, hali hiyo ya mambo inaonyesha jambo moja
kwamba, taifa limeingia katika kipindi kigumu kabisa tangu baada ya
uhuru, kwani kuvamiwa kwa rushwa ndani ya CCM na kwa hakika
serikalini, kunaweza kukawa kielelezo cha kutokomea kwa haki katika
maeneo mbalimbali.
Hivyo basi, tunapenda kuwaasa viongozi wakuu wa CCM na wale wa
serikali kuyachukulia matukio yote haya ya karibuni kwa tahadhari
kubwa na kuyapa uzito unaostahili ili kuliepusha taifa katika balaa
baya zaidi siku zijazo.
Tunaamini kwa dhati kabisa kwamba, iwapo viongozi wetu watayaangalia
kwa undani malalamiko ya kina Butiku, Ngasongwa, Mangula, Mungai na
wengine wengi, na kuyachukulia hatua zinazopaswa, basi watakuwa
wamelinusuru taifa hili ambalo kimsingi limeanza kuzama katika bahari
yenye kina kirefu.
h.sep