Maombi

62 views
Skip to first unread message

Honorati Manang

unread,
Aug 3, 2011, 5:07:21 AM8/3/11
to iman...@googlegroups.com
Maombi ni neno ambalo limetumika sana katika Biblia. Mara nyingi
maombi yanafanyika makanisani, kwenye mikutano mbalimbali ya injili,
katika vikundi mbalimbali, na hata kwa mtu binafsi. Maombi yana
umuhimu mkubwa sana katika huduma. Na yakipata nafasi mafanikio
makubwa yanakuwepo. Maombi ya mtu binafsi nayo pia ni muhimu sana.
Mimi mwenyewe nimeona maombi yakifanya mambo mengi makubwa sana katika
maisha yangu.

Yote ambayo Mungu ameyafanya na anaendelea kuyafanya katika maisha
yangu hata sasa yamenifanya mimi binafsi kusikia msukumo mkubwa na wa
kipekee sana moyoni mwangu wa kutaka kujua zaidi na zaidi kuhusu
maombi. Hili ni jambo kubwa sana na linatufaa sisi sote ambalo Mungu
mwenyewe ameliweka ili tupate nafasi ya kuwasiliana naye. Mungu
ameiweka njia hii ya maombi ili apate kutusikiliza wakati
tunapozungumza naye.


Kwa hiyo kuomba ni njia pekee ya kutuunganisha na Mungu.

Yeye anayemtafuta Mungu wa kweli inampasa aanze uhusiano naye kwa
njia ya maombi na kwa njia hii ya kuomba uhusiano wetu na Mungu
unaanzishwa na kutunzwa.

Ni lazima tunyenyekee na kutii na kuonyesha heshima mbele za Mungu
wetu kwa kumshukuru na kumtukuza kwa ajili ya uweza wake na nguvu
zake.
Yoh: 15:14 "Ninyi mmekuwa rafiki zangu mkitenda niwaamuruyo." Mungu
anatuheshimu sana, tunapoyatenda yale aliyotuagiza. Anatuthamini kiasi
cha kutufanya sisi kuwa marafiki zake, hivyo tunaweza kushirikiana
naye na kuongea naye wakati wowote. Yeye kama rafiki yetu anapenda
sisi tuwe na furaha, amani na maisha ya ushindi. Mungu anapenda sisi
tuwe karibu naye kila wakati. Yak 4:8 "Mkaribieni Mungu naye
atawakaribia ninyi."

Hebu sasa tujifunze kwa undani mambo muhimu kuhusu maombi. Tuanze kwa
kujiuliza: Kwa nini inatupasa kuomba?

Inatupasa kuomba kwa sababu zifuatazo:


(1) Mungu mwenyewe ametuagiza tuombe.

Hakika Baba aliye na upendo anataka kushirikiana na watoto wake kwa
njia ya maombi. Ushirikiano wa kuwasiliana kati ya roho zetu na
Mungu. Anatuhimiza mara kwa mara kufanya hivyo. Na huu ni uamuzi wa
Mungu mtakatifu kwamba tunaukuza ufalme wake, ni uchaguzi wake muhimu
tunaoufanya kuliko kazi nyingine yoyote anatutumia, anatuongoza kuomba
vizuri.

1Tim:2:1-3 "Basi kabla ya mambo yote nataka dua, na sala, na maombezi
na shukurani, zifanyike kwa ajili ya watu wote, kwa ajili ya wafalme
na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika
utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri nalo linakubalika mbele za Mungu
Mwokozi wetu."


Kwa maneno hayo tunaona kwamba Mungu ameagiza. Tunaweza kusema kwamba
Mungu ametoa amri. Tukiangalia neno hili 'NATAKA' halina mjadala,
Yeye ndiye aliye juu ya vyote, ni wa kwanza kuliko vyote, Yeye anataka
maombi yafanyike. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kukosa kuomba ni
dhambi, ni kosa la kutokutii agizo la Mungu, kama Maandiko
matakatifu yanavyosema katika 1 Samweli 12 :23a

"Walakini mimi, hasha! Nisimtende BWANA dhambi kwa kuacha kuwaombea
ninyi." Dhambi hii ni mbaya na inaleta kizuizi. Hakuna jambo lolote
litakalofanyika tusipoomba yaani hakutakuwepo na maemdeleo yoyote.
Tusizuie makusudi ya Mungu anayotaka kuyatenda; tutambue kwamba Mungu
ni mwenye Busara kuliko sisi tulivyo, na tukubali kuwa makusudi yake
ni makubwa sana kuliko yetu.

2 Nyakati 16: 9 "Kwa maana macho ya BWANA hukimbia–kimbia duniani
mwote ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao waliokamilika moyo
kuelekea kwake."


Lengo kubwa la Mungu ni kwamba anataka kuwa pamoja nasisi katika yote
tunayohangaika nayo kila siku. Anataka kutusaidia hata katika kazi
zetu za mikono. Hivyo anajitoa kabisa kwa ajili yetu akitaka
kushirikiana nasi katika mambo yote.


Bila shaka utazidi kujifunza kuwa maombi ni msingi mkuu wa kazi
nyingine zote katika ufalme wa Mungu, ndio maana Mungu hatulii anataka
watu waombe. Kama maandiko matakatifu yanavyosema katika kile kitabu
cha Mathayo 7:7 "Ombeni nanyi mtapewa tafuteni nanyi mtaona bisheni
nayi mtafunguliwa."

(a) Omba uweze Kupokea

(b) Tafuta uweze kupata.

(c) Bisha mlango uweze kufunguliwa


Isaya 55 "Mtafuteni BWANA maadamu anapatikana mwiteni maadamu yu
karibu."

Luka 18:1 "Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku
zote wala msikate

tamaa." Kufuatana na umuhimu uliopo katika kuomba hatupaswi kukata
tamaa.

Wafilipi 4:6 "Msijisumbue kwa neno lolote bali katika kila neno kwa
kusali pamoja na kushukuru na haja zenu na zijulikane na Mungu." Mungu
anajua kuwa kuna mambo yanayosumbua, hivyo basi Yeye anatukaribisha
kwake akisema yaleteni kwangu, hata mambo madogo madogo
nitawasaidia..


Sisi tunamhitaji Mungu kwa haja zote, tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, na
katika yeye tunaweza kuendelea vizuri, vinginevyo tunaweza kupotea
kabisa. Neno la Mungu linasema hivi katika Yohana 15:5-7 "Mimi ni
mzabibu nayi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa
sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Mtu
asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu
huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu,
na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi
mtatendewa."


Jinsi tunavyoendelea kuishi kwa kutambua na kutenda jambo hili zaidi
na zaidi, ndivyo tunavyozidi kumpatia Bwana heshima.

(2) Tunaomba kwa sababu mwili ni dhaifu

Dhiki na taabu zinatufundasha kumwomba Mungu, na kama ilivyo katika
maandiko matakatifu Mathayo 26:41 Neno linasema "Kesheni mwombe
msije mkaingia majaribuni roho i radhi lakini mwili ni dhaifu." Na
katika Zab;50:15 imeandikwa "Ukaniite siku ya mateso nitakuokoa na
wewe utanitukuza."

Tunapoomba tunatambua dhiki na taabu tulizonazo na mara nyingi
tunatambua kwamba hatuwezi. Na Mungu anaweza kuruhusu tupate dhiki
ili atuonyeshe udhaifu wetu na kutukumbusha kwamba msaada wa kweli
unapatikana kwake kwa hiyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi katika
dhiki. Hakuna vipingamizi vitakavyoweza kututisha, kwa maana matumaini
yetu hayapo katika nguvu zetu, bali yote tunayaweka mbele zake Mungu
kwa njia ya maombi. Neno la Mungu linasema hivi. Ayubu 33:29-30
"Tazama haya yote ni Mungu anayeyafanya mara mbili naam hata mara tatu
kwa mtu ili kurudisha roho yake itoke shimoni."

Lk:21:36 "Basi kesheni ninyi kila wakati mkiomba ili mpate kuokoka na
hayo yatakayotokea na kusimama mbele za Mwana wa Adamu."

Bwana wetu Yesu yeye mwenyewe alikuwa kielelezo katika kuomba, aliomba
maombi ya dua pamoja na kulia sana. Yeye alilia machozi ingawa alikuwa
ni mwana wa Mungu. Sisi ni zaidi tunahitaji na kutegemea maombi,
tuziangalie nafsi zetu sisi wenyewe kisha tujiulize: "Mimi ni nani?
Kama Yesu aliomba kwa nini mimi na wewe tusiombe?" Waebrania 5:7
"Yeye,siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na
kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi,
akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu."

(3) Tunaomba kwa sababu adui ana nguvu na vita ni vikali.

Kwa kuwa maombi ndiyo kiini cha maisha yetu, tunatakiwa kuomba ili
kuizima mishale ya shetani. Adui huyu anafahamu sana jinsi maombi
yalivyo na faida kwetu. Kwa sababu hii anatushambulia tunapoomba.
Hivyo tunashindana na adui ambaye ana nguvu. Kwa hiyo tukishindana
naye kwa nguvu zetu binafsi ni bure kabisa. Lakini tunaweza kumshinda
adui shetani kwa njia ya maombi. Neno la Mungu linasema katika
Waefeso 6:11-12 "Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga
hila za shetani, kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na
nyama;bali ni juu ya falme na mamlaka, juu wa wakuu wa giza hili, juu
ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho." Ukiendelea
kusoma mstari wa 18 Neno la Mungu linasema "kwa sala zote na maombi
mkisali kila wakati katika roho mkikesha kwa jambo hilo na kudumu
katika kuwaombea watakatifu."

Luka 10:19 "Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu
zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru." Njia pekee ya
kuzishinda nguvu za yule adui ni maombi.


Maombi yana nguvu kubwa ya kuzishinda nguvu za yule adui. Ndio sababu
tunaona vizuizi mbalimbali vinavyowekwa mbele yetu kila siku ili
tusiombe. Lakini kwa kadiri tunavyojifunza kuomba kwa Roho, ndivyo
tunavyoweza kuona kuwa maombi ni kazi inayowezekana kwetu sisi
tunaomwamini Mungu katika ulimwengu huu.

1 Petro5: 8 "Mwe na kiasi na kukesha; kwa maana mshtaki wenu Ibilisi,
kama simba angurumaye,huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi
mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani."

Ushindi mkubwa juu ya adui yetu haupatikani kwa mapanga, mikuki wala
baruti bali unapatikana kwa njia ya maombi. Mfano wa Daudi juu ya
Mfilisti. 1Samweli17:45-47 "Ndipo Daudi akamwambia yule mfilisti, wewe
umenijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe
Kwa Jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli
uliowatukana." 1Sam 17:37 "Daudi akasema Bwana aliyeniokoa na makucha
ya simba na makucha ya dubu ataniokoa na makucha ya mfilisti huyu."


Tunatakiwa tuwe na ujasiri kama Daudi kwa kuyaangalia matendo makuu ya
Mungu aliyotutendea wakati uliopita hadi sasa na tuone kwamba hata
hayo tunayoona ni magumu tunaweza kuyashinda kwa Jina la Bwana.


Tena Mungu anasema hivi katika Kumbukumbu la Torati 20:1
"Utakapokwenda vitani kupigana na adui yako, na kuona farasi, na
magari, na watu wengi kuliko wewe usiogope kwa kuwa Bwana Mungu wako,
yu pamoja nawe."


Hata Yesu aliona kwamba ni muhimu katika ulimwengu huu tulindwe na
yule mwovu na majaribu yake. Ndio maana alituombea ombi hili: Yohana
17:15 ‘’Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na
yule mwovu." Na katika 2 Wathesalonike 3:3 tunasoma kuwa "Lakini
Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu.’’

Vile vile katika 1Yohana 5:18 imeandikwa ‘’Twajua yakuwa kila mtu
aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi bali yeye aliyezaliwa na Mungu
hujilinda, wala yule mwovu hamgusi." Maombi yanatuwezesha kujilinda
mwovu asituguse.

Ushirika wetu na Mungu ukiwa mzuri hatuna haja ya kuogopa, haijalishi
ya kwamba sisi tupo katika hali gani. Tukiliita jina lake kwa mamlaka
tuliyopewa ya kumkemea adui kwa Jina la Yesu, hakuna jambo lolote
litakalotudhuru, tutaziangusha ngome zote za adui.

(4) Tunaomba ili tuishi maisha ya utakatifu.

Wakati tunapokosa au tunapomkosea Mungu kwa kutenda dhambi, kwanza
kabisa tunapaswa kujua kwamba Mungu anatuona, na anajua nini
tumefanya, hatuwezi kujificha mbele za Mungu. Hivyo kwa sababu Yeye
anatupenda na anataka kutusamehe, anataka tuungame dhambi zetu.
Hapendi tuendelee kubaki katika hali ya dhambi. Kwa hiyo hatupaswi
kukaa kimya ikiwa tumekosea. Tunatakiwa tunyenyekee na kujieleza kwa
kusema wazi mbele zake yale tuliyotenda. Katika kitabu cha Yeremia
8:6 Neno la Mungu linasema: "Nalisikiliza nikasikia, lakini walisema
yasiyo sawa; hapana mtu aliyetubia maovu yake, akisema, nimefanya
nini?..."

Na katika Yohana 1:9 imeandikwa: "Tukiziungama dhambi zetu yeye ni
mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na
udhalimu wote."

Maombi hutusaidia ili tuweze kutakaswa, tuweze kusafishwa. Hivyo
inatupasa kuungama na kutubu dhambi zetu. Tunatakiwa tujue kwamba
tukikaa katika dhambi hatutahesabiwa haki mbele za Mungu. Mungu
anataka kutusaidia tushinde dhambi na kuishi maisha ya utakatifu. Yak:
5:16a "Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate
kuponywa."

2 Nyakati 7:14 "Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu,
watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuacha njia zao
mbaya; basi nitasikia kutoka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na
kuiponya nchi yao."

(5) Maombi husababisha nguvu za Mungu zifanye kazi.

Mambo makubwa sana yanayofanyika hapa duniani Mungu ameyafanya
yategemee maombi ya watoto wake, kama ilivyoandikwa katika 1Wafalme:
18:36-39 "Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii
akakaribia, akasema Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa
Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli,
na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na yakuwa nimefanya mambo yote kwa
neno lako. Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa
wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.
Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na
kuni, na mawe , na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika
mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema BWANA
ndiye Mungu BWANA ndiye Mungu."


Kama Eliya asingechukua hatua ya kuomba, Mungu asingetenda jambo
lolote lakini tunaona maombi ya Eliya yaliweza kumgusa Mungu hata
akaweza kuziachilia nguvu zake, (ndipo moto wa BWANA ukashuka) mambo
yaliyotendeka ni makubwa sana na watu wote wakamtukuza Mungu. Na
jambo hili limekuwa ukumbusho mbele za Mungu na katika kizazi hiki
pia.

Katika 2 Wafalme 6:17-18 imeandikwa hivi: "Elisha akaomba, akasema,
Ee BWANA nakusihi, umfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua
macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa
kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote. Na
walipotelemka Elisha akamwomba BWANA, akasema, uwapige nakusihi watu
hawa kwa upofu akawapiga upofu sawasawa na neno la Elisha."


Elisha aliomba mbele za Mungu na Mungu akatenda. Kwa sababu hiyo
waliweza kuwateka maadui zao na kuwafikisha mbele za mfalme wa Israeli
pasipo wao kujua. Bila shaka jambo hili lilikuwa kubwa sana ambalo
Mungu alilitenda kupitia maombi ya Elisha.

Mara kwa mara tunahimizwa tuombe kwa ajili kazi ya Mungu, Mungu
abadilishe mioyo ya watu waweze kutubu. Sisi sote tunajua kwamba Mungu
ana uwezo mkubwa sana. Ni kwa nini basi tunatakiwa tuombe ili Yeye
aitimize kazi yake? Swali hili ni gumu hatuwezi kulijibu kama
inavyotakiwa. Lakini kwa kifupi ni kwamba huo ni utaratibu wake ambao
ameupanga kwamba inatupasa kuomba ili Mungu aweze kutimiza kazi yake.

Mungu ameona ni vyema kabisa sisi tushiriki kufanya kazi pamoja na
Yeye na hili jambo ni zuri na linapendeza sana kwamba Mungu
ametukubali na kututhamini. Na katika jambo hili ni muhimu sisi tuweze
kutambua kwamba wokovu wetu umetoka kwa Mungu, na yakwamba sisi
tumeupata kwa njia ya neema tu ya Mungu. Hivyo tukumbuke kwamba wapo
watu waliofunga na kuomba kwa ajili yetu na neema hii ya wokovu
ikatufikia. Hivyo basi ni wajibu wetu sisi pia kuomba kwa ajili ya
ndugu zetu marafiki zetu, wafanyakazi wenzetu na hata nchi yetu na
watu wote Ulimwenguni ili Mungu aweze kuitimiza kazi yake ya
kuwaokoa.

Tunaweza pia kumwomba Mungu kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya watu
wengine; wafunguliwe katika vifungo mbalimbali, wamjue Mungu wa kweli,
wasamehewe dhambi na kutakaswa na damu ya Yesu, watoke katika laana za
aina mbalimbali, waponywe maradhi mbalimbali n.k. Tunapoomba miujiza
mbalimbali inaweza pia kutendeka.

(5) Maombi yanatusaidia kupata mahitaji yetu.

Maombi yanayohusu mahitaji yanapaswa kupelekwa mbele za Mungu bila
mashaka. Yah 15:5 "Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa
ndani yenu ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa."

Tunaweza kuomba na kupata kile tunachokihitaji. Hii ni ahadi ya ajabu
sana kutoka kwa Mungu lakini kumbuka kwamba ahadi hii hufanya kazi tu
endapo sisi tutakaaa ndani yake.

Katika 2 Wafalme 6:1-7 tunasoma "Kisha wana wa manabii wakamwambia
Elisha, angalia basi, mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu. Basi
twende mpaka Yordani, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili
tujifanyie mahali pa kukaa. Akajibu haya nendeni. Mmoja wao akasema
uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako. Akajibu,
nitakwenda. Basi akaenda pamoja nao. Na walipofika Yordani, wakakata
miti. Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka
kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu kwani
kiliazimiwa kile. Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha
mahali . Akakata kijiti , akakitupa palepale, chuma kikaelea. Akasema,
kiokote. Basi akanyoosha mkono akakakitwaa."

Tunaposema kwamba maombi yanatusaidia kupata mahitaji yetu, hiyo
inamaanisha mahitaji yetu yote tunayoyahitaji katika maisha haya ya
sasa. Mungu atatutimizia mahitaji yetu yote tukiomba.

Mungu anaheshimu sana maombi ya watoto wake. Ameyafanya kuwa na harufu
nzuri sana ya manukato na kuyathamini kiasi cha kuyaweka katika vyombo
vya dhahabu na kuyapokea kwa muziki kama ilivyoandikwa katika Neno la
Mungu Ufunuo:5:8-10 "Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai
wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana –
Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa
manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya
wakisema wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri
zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa
kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na
makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi."

Ndugu yangu kwa maneno haya unaweza kuona jinsi ambavyo upo umuhimu
mkubwa sana wa maombi. Kwahiyo tusiyafanye maombi kuwa kama desturi
fulani au taratibu fulani, wala tusilichukulie jambo hili kama ni
jambo la kawaida au uzoefu fulani. Tumheshimu Mungu na kutii maagizo
yake. Maana Yeye anatuheshimu sisi na ametupa nafasi hii ya pekee
kabisa ya kwamba tuweze kuzungumza naye wakati wowote ule
tunapoendelea kuishi hapa duniani. Maombi yote tunayoyaomba yatajibiwa
na pia yataendelea kudumu kama kumbukumbu mbele za Mungu.

Kwa sababu hiyo anza sasa kwa bidii kuwaombea ndugu zako, wazazi wako,
watoto wako na nchi yako.

Hata saa yako ya mwisho atakapoamua Yeye mwenyewe kukuchukua kwenda
kwake mbinguni, yale maombi uliyoyaomba wakati ukiwa hai Mungu
ataendelea kuyajibu sawa sawa na jinsi ulivyoomba. Maombi yako
yatafanya kazi ya Mungu iendelee kutendeka na yatakuwa ndio urithi
wako uliouacha hapa duniani.

Na Mwl. Josephine Kapaya

Reply all
Reply to author
Forward
0 new messages