---------- Forwarded message ----------
From:
Honorati Manang <hma...@gmail.com>Date: 2011/8/3
Subject: Tukio la Kutisha
To:
hma...@gmail.comJe una habari kuhusu tukio la kutisha linalokuja hivi karibuni?
DALILI ya mvua ni mawingu. Mtu mwenye busara aliyeanika nguo zake nje,
anapoona mawingu yametanda kila mahali, anajua kwamba mvua wakati
wowote inaweza kunyesha, hivyo anafanya haraka kwenda kuzianua nguo
hizo. Vivyo hivyo, Yesu Kristo anatuonya kwa msingi huohuo, kuzitambua
ishara za zamani hizi yaani dalili za nyakati hizi za mwisho, au za
mwisho wa dunia, na kuyajua yale yanayokuja ili tujiandae vema
kuyakabili. Biblia inasema katika MATHAYO 16:2-3, ”Akajibu akawaambia
kukiwa jioni, mwasema, kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni
nyekundu. Na asubuhi, mwasema, leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana
mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua
uso wa mbingu; lakini, je ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua?“
Sasa je, ni nini dalili za mwisho wa dunia?
Kilicho na mwanzo kina mwisho, na mwisho wa dunia uko karibu sana.
Dalili mbalimbali za mwisho wa dunia, zinatajwa katika Biblia, kwa
mfano katika MATHAYO 24:3-14; 1TIMOTHEO 4:1-5; 2 TIMOTHEO 3:1-5; na
UFUNUO WA YOHANA 22:6-7,10-12. Dalili zote zimetimia, na zinazidi kuwa
dhahiri mbele ya macho yetu. Moja kati ya dalili zinazotajwa ni
wachafu kuwa wachafu na maasi kuongezeka (UFUNUO 22:11; MATHAYO
24:12). Kabla ya maangamizo wakati wa Nuhu na pia wakati wa Sodoma na
Gomora, uchafu uliongezeka sana. Vivyo hivyo siku hizi, tukiona mambo
haya ya uchafu yanaongezeka, tujue hiyo ni dalili ya mwisho wa dunia.
Je, uchafu huu umeongezeka hivi leo? Jibu ni kwamba, ni kwa namna ya
kutisha.
Pamoja na sheria kali ya kujamiiana, ambayo inawafanya watu
wanaonajisi watoto wadogo, wabakaji na walawiti, kupewa adhabu ya
kifungo; bado vitendo hivi vinaongezeka kwa kasi kama vile watu
hawajali! Karibu kila siku tunasikia habari hizi katika vyombo vya
habari. Wengine wanaripotiwa kulawiti watoto wadogo waliowazaa
wenyewe! Wengine wanalawiti wazee wa miaka zaidi ya sabini! Wengine
wanawabaka mama zao! Mtu mmoja anaripotiwa kuwalawiti watoto wadogo
watano wa shule ya msingi, zamu kwa zamu! Sehemu mbalimbali duniani,
wanaume wanaoripotiwa kuwaacha wake zao kwa sababu hawataki
kulawitiwa, wameongezeka sana. Huko Marekani na Ulaya, ndoa za wanaume
kwa wanaume (mashoga) na wanawake kwa wanawake(wasagaji) zimekuwa ni
jambo la kawaida. Waziri Mkuu wa nchi moja kubwa Ulaya, anataka ushoga
uhalalishwe na Bunge la nchi yake. Maaskofu wa dhehebu moja kubwa la
Ukristo, hivi karibuni, walipiga kampeni ya kutaka ushoga uhalalishwe!
Wachafu watazidi kuwa wachafu!
Dalili nyingine ya mwisho wa dunia, inatajwa katika Biblia, ingawa
haiko wazi sana katika tafsiri ya Kiswahili. Katika Biblia ya
Kiingereza ya tafsiri ya King James Version(KJV) katika MATHAYO 24:7,
tunasoma, …. ”…and there shall be famines and pestilences…..“
"Pestilences,“ ni magonjwa mabaya ya kuambukiza yasiyokuwa na dawa au
tiba. Leo tunaishi nyakati za kuwepo kwa Ukimwi, ugonjwa mbaya wa
kuambukiza usio na tiba. Hii ni dalili ya mwisho wa dunia. Vivyo
hivyo, dalili nyingine inatajwa katika MATHAYO 24:14, ”Tena habari
njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa
mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.“
Kwa kutumia teknolojia ya kisasa, Injili inahubiriwa kwa kasi ya
kutisha. Kwa mfano kwa kutumia ”satellite“, Mwinjilisti mmoja
anayeitwa Billy Graham, tarehe 14 April 1996, alihubiri Injili na nchi
zote ulimwenguni walisikia Injili kwa wakati huohuo, wakati yeye akiwa
Marekani. Hatusemi kwamba mwisho wa dunia utakuwa leo au kesho. Siku
ile wala saa, hakuna aijuaye, lakini yote haya ni mawingu ambayo ni
dalili ya mvua! Maana yake ni kwamba, tuko ukingoni kabisa na wakati
wowote ule mwisho wa dunia unakuja!
Mwisho wa dunia utakuwaje? Mfululizo wa matukio ya mwisho wa dunia,
utatanguliwa na tukio la kutisha litakalotokea ulimwenguni wakati
wowote kuanzia sasa, maana dalili za mwisho huu tumekwisha kuona
kwamba zinatimia machoni petu hivi sasa. Tukio hili , linaitwa
”Kunyakuliwa kwa watu waliookoka“, na linaelezwa katika 1
WATHESALONIKE 4:15-17, "Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana,
kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana,
hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana
mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko na sauti ya
malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo
watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tutanyakuliwa pamoja nao
katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na
Bwana milele…“
Kunyakuliwa, ni tendo la kuchukuliwa kwa kitu ghafla, kwa kasi kubwa
na kuondolewa pale kilipokuwa; katika hali ya kuwaacha watu wamepigwa
butwaa, kwa jinsi wasivyoweza kukipata kitu hicho tena. Watu
waliookoka, muda si mrefu ujao, watanyakuliwa kwa jinsi hii na Yesu
Kristo. Yesu anakuja kufanya kazi hii, haraka wala hatakawia
(WAEBRANIA 10:37). Siku ya kunyakuliwa kwa watu waliookoka, sehemu
nyingine dunia itakuwa usiku, sehemu nyingine mchana, maana majira
duniani yanatofautiana. Jua likitua sehemu moja ya dunia, linachomoza
sehemu nyingine ya dunia.
Wakati wa kunyakuliwa kwa watu waliookoka, ikiwa ni mchana, watu wote
waliokufa tangu zamani za kale wakiwa wameokoka na wakawa wamekwenda
mbinguni, watafufuliwa na kutokea duniani tena. Kila mmoja atawaona.
Watakuwepo watu wengi kwa ghafla, mitaani kila mahali, waliokufa
zamani wakiwa wameokoka. Hata kama kwenye makaburi ya zamani, siku
hizi kuna Jengo la ofisi, watatokea humo humo ofisini. Dakika moja
kufumba na kufumbua, watu waliookoka ambao wako hai duniani nao
wataungana pamoja nao, na wote watabadilishwa miili yao na kupewa
miili ya utukufu wa milele, isiyoharibika. Biblia inasema katika
1WAKORINTHO 15:52-53, ”Kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa
parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, wafu watafufuliwa, wasiwe
na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae
kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.“
Katika wale watakaokuwako duniani, watatwaliwa wale waliookoka tu na
kuishi katika utakatifu mpaka mwisho. Watakuwepo wawili wakilima
kondeni au shambani, mmoja ameokoka na mwingine hajaokoka, ni mwenye
dhambi. Aliyeokoka atatwaliwa, ambaye hajaokoka ataachwa. Ikiwa ni
katika basi, treni au eropleni; dereva au rubani ameokoka, atatwaliwa,
na wenye dhambi watabaki. Tunasoma katika MATHAYO 24:40-41, ”Wakati
ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;
wanawake wawili watakuwa wakisaga, mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.“
Ikiwa itakuwa usiku, na katika familia fulani mume hajaokoka, mke
ameokoka, watoto wakubwa hawajaokoka, na wako watoto wadogo wasiojua
mema na mabaya; mume huyo mlevi anayempiga vita mkewe kwa sababu
ameokoka, ataamka asubuhi na kushangaa kuona mkewe kitandani na watoto
wadogo hawapo. Atawauliza watoto wakubwa, Mama yenu yuko wapi?“
watajibu, ”hatujui“. Atatoka nje kwenda kuuliza, na kila mahali
itaripotiwa Polisi, kwamba wako watu waliotoweka usiku, pamoja na
watoto wote wadogo. Katika kituo cha Polisi pia, kutakuwepo na polisi
waliotwaliwa. Baada ya uchunguzi duniani kote, waandishi wa habari
ambao hawajaokoka, walioachwa, watatoa ripoti katika magazeti,
”Mamilioni ya watu kote duniani wameripotiwa kutoweka usiku wa jana.
Uchunguzi umeonyesha kwamba waliotoweka ni walokole ambao wamekuwa
wakidhaniwa kuwa wamechanganyikiwa au ”kupotea.“ Taarifa zaidi
zinaeleza kwamba watoto wadogo wote pia wametoweka. Taarifa za
uchunguzi zinaonyesha kwamba waliotoweka wamenyakuliwa kwenda kumlaki
Yesu mawinguni kama walokole walivyokuwa wakihubiri!“
Hawa watakaotwaliwa, wataungana na wale waliofufuliwa, na kisha wote
kwa pamoja; watavutwa kama kwa sumaku, kwa mvuto utakaotoka kwa Yesu
atakayekuwa mawinguni. Yeye hataonekana kwa wale watakaokuwako
duniani. Wenye dhambi nao watajaribu kupaa, haitawezekana. Itakuwa
kama kuku na ndege wanaposhitushwa na kishindo. Ndege hupaa angani,
lakini kuku akijaribu kupaa huishia kwenye kichanja cha kuanikia
vyombo! Sumaku itawavuta waliookoka tu, kama jinsi sumaku inavyovuta
vyuma tu na kuacha mchanga au udongo! Baada ya wenye dhambi kuachwa,
ndipo kitakapokuwapo kilio na kusaga meno hapa duniani. Itafuata dhiki
kubwa ya miaka saba, ambayo namna yake haijawahi kutokea. Biblia
inasema katika MATHAYO 24:21, ”Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki
kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata
sasa, wala haitakuwapo kamwe.“ Wenye dhambi watateswa kwa namna ya
kutisha. Watu watatamani kufa kutokana na mateso na maumivu, lakini
mauti itakuwa imeondolewa (UFUNUO 9:2-6). Wataiambia milima na miamba,
tuangukieni, watamwomba Mungu awahurumie, huruma na uvumilivu wake
utakuwa umekoma (UFUNUO 6:15-17; ISAYA 26:16-18). Wale walionyakuliwa
huko juu watakuwa katika karamu ya Arusi ya Mwanakondoo baada ya
kupewa kila mtu taji zake (UFUNUO 19:5-9; 2WAKORINTHO 5:8-10).
Mpendwa msomaji, parapanda inaweza kulia usiku wa leo. Je, utakuwa
kundi lipi? Utanyakuliwa au utaachwa? Ikiwa wewe ni mwenye dhambi,
hujaokoka, utaachwa kwa hakika. Hata hivyo, bado una nafasi ya kutubu
dhambi zako. Ukifanya hivyo huku ukimaanisha moyoni kuziacha dhambi
zote, utasamehewa sasa hivi, na hivyo kuokoka. Na sasa hivi
utahesabiwa kuwa miongoni mwa wale watakaonyakuliwa (MITHALI 28:13;
LUKA 1:77). Je uko tayari kutubu, na kuokoka? Najua uko tayari. Basi
fuatisha sala hii fupi kwa dhati kutoka moyoni:
”Mungu wangu, asante kwa kunipa ujumbe huu kabla tukio hili
halijatokea. Natubu dhambi zangu zote nikimaanisha kuziacha. Yesu
Kristo naomba unisamehe dhambi zangu zote na kuniokoa. Naamini sasa
kwamba umeniokoa, katika Jina la Yesu. Amen.“
Tayari umeokoka. Ili uutunze wokovu wako mpaka wakati wa Kunyakuliwa,
hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu
(ZABURI 119:11).
MUNGU AKUBARIKI!!!