Kijana ni mtu wa kike au wa kiume mwenye umri kati ya miaka 15 na 45.
Biblia inasema nini juu ya kijana?
Biblia imenena mambo mengi juu ya kijana, na baadhi ya hayo ni kuwa
fahari ya kijana ipo katika nguvu zake (Mithali 20:29). Kijana ana
nguvu nyingi, neno la Mungu linakaa ndani yake na kisha amemshinda
shetani(1Yohana 2:14b).
Yohana anawaandikia vijana akisema wana nguvu nyingi, pili neno la
Mungu linakaa ndani yao na kisha wamemshinda shetani. Nguvu yaweza
kuwa ya kiroho au ya kimwili, maana zote ni za muhimu na mara nyingine
hutegemeana katika utendaji.
Nguvu moja ikikosekana hujitokeza upungufu unaoweza kupelekea
uharibifu kama vile mtu kurudi nyuma kwa sababu ya majaribu. Nguvu ya
kimwili ya mtu wa Mungu ikitumika kwa mujibu wa uongozi wa Roho
Mtakatifu, yaweza kupelekea mtu kuwa na nguvu ya kiroho iletayo
ushindi juu ya hila na mitego ya yule mwovu.Hapa ina maana kuwa, kwa
mtu wa Mungu ukiwa na nguvu ya kimwili na unaongozwa na Roho wa Mungu
utamtumikia Mungu pasipo ulegevu, tofauti na mzee ambaye anaweza
kuhitaji kufanya jambo lakini nguvu ya kwenda kufanya hana, hilo nalo
Mhubiri aliliona na kumhamasisha kijana kutumika akiwa bado anazo
nguvu. Mhubiri12:1 ”Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako kabla
hazijaja siku zilizo mbaya…“ Yohana anawaandikia vijana akionyesha
sifa za aina ya vijana aliokuwa akiwalenga. Anatazamia kwamba kijana
akiitumia nguvu hiyo kama ilivyokusudiwa na Mungu, na kulisoma neno,
kuomba kwa bidii zake zote, matokeo yake atakuwa na hazina tele ya
neno ndani mwake, na kisha atamshinda shetani, maana anazo nguvu za
kiroho na za kimwili. Kijana wa aina hii hana hofu maana hata shetani
akija kwa sura gani au akitumia mazingira gani, haogopi maana silaha
alizo nazo (Neno) ni tishio kwa adui. Mungu anawatafuta vijana kama
hao wabebao silaha hiyo ya Bwana , nyakati zote, kila mahali na kwa
bidii. ”..Nimewaandikia ninyi vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno
la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu“(I Yohana
2:14b).
Biblia inasema kijana akilitii Neno la Mungu na kulifuata litasafisha
njia yake. Litamkamilisha kwa kiwango anachotaka Mungu, kwa makusudi
ya Mungu na kwa utukufu wa Mungu. Kwahiyo ili kijana aweze kuishi
maisha matakatifu, yenye ushindi tele na yanayomtukuza Mungu yampasa
kuisafisha njia yake kwa kutii, akilifuata neno la Mungu. Zab.119.9
”Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno
lako.“
Kijana, kufanikiwa kuisafisha njia yako kutategemeana na wewe mwenyewe
utakavyotumia nguvu zako. Yakupasa kuelekeza nguvu zako katika maombi,
kujisomea Neno la Mungu, hii ni pamoja na kulitafakari na kulitendea
kazi. Kwa kufanya hivyo utapata nafasi nzuri ya kumsikiliza Mungu na
kujua ni nini mpango na makusudi yake kwako. Kijana hupaswi kulala
usingizi tangu jioni hadi asubuhi na tangu January hadi Desemba, huo
ni msiba wa kutosha kwa kijana maana Biblia inasema mtu wa aina hiyo
atapata umaskini wa kumtosha. Si vema kijana kuzagaa, ukikutwa na adui
ukiwa umezagaa atakutumikisha katika matakwa yake. Ni muhimu sana
kijana kuwa na mikakati na kuiombea ili kupata uongozi wa Roho
Mtakatifu. Mungu anajali sana kijana kuwa na mkakati. Mfano mzuri ni
namna alivyomwandaa Yoshua kushika nafasi ya Musa. Awali ya yote
alimhakikishia uwepo wake pamoja na kijana huyo, na akamwahidi
kutomwacha wala kumpungukia kabisa: ”Hapatakuwa mtu yeyote atakayeweza
kusimama mbele yako siku zote za maisha yako…sitakupungukia wala
sitakuacha.“ (Yoshua 1. 5).
Hapa Mungu anamhakikishia Yoshua kuwa, hata kutokee tatizo kubwa kiasi
gani, hata vitisho viwe vikubwa namna gani, hata ainuke nani,
asingeweza kuzuia wala kukwamisha kusudi la Mungu katika huduma
aliyokuwa anakabidhiwa na Mungu, ya kuwafikisha Waisraeli nchi ya
Kanaani. Hali kadhalika wewe kijana, yumkini bado unawategemea wazazi
au ndugu, lakini kwakuwa umeokoka labda wamekutenga, hawataki kukupa
huduma, hata masomoni unatishiwa kufukuzwa kwasababu huna karo;
yumkini umeoa au umeolewa na huyo mume au mkeo anakutesa kwa ajili ya
wokovu; kazini unanyanyaswa na mkubwa wako wa kazi au wafanyakazi
wenzio, halikadhalika kwenye biashara zako wanakutesa kwa njia
mbalimbali. Katika hali yoyote ile, jambo la muhimu uwe na uhakika
kwamba Mungu yupo pamoja na wewe na kwamba hatakuacha wala
hatakupungukia. Hivyo usikate tamaa, azimia kutomwacha Mungu kabisa,
simama katika haki na ahadi za Mungu, utaona ushindi mkubwa.
Baada ya Mungu kutoa uhakika juu ya uwepo wake kwa kijana huyo Yoshua,
alimpa mikakati ya namna atakavyoweza kufikia lengo ambalo lilikuwa
kuwafikisha Waisraeli katika nchi ya ahadi, Kanaani. Mikakati hiyo ni
kama ifuatavyo:
1. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi….
Mungu hapendezwi na uvivu, alitaka Yoshua awe hodari tu na ushujaa
mwingi na siyo mtu wa kujihurumia hurumia bali awe mwepesi wa kwenda
anakotakiwa, kutekeleza majukumu ambayo Mungu angempa inavyotakiwa,
kwa wakati unaotakiwa, na pasipo hofu. Huo ndiyo ushujaa.
2. ...uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa
mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume au wa kushoto.(Yosh.
1.7).
Mungu anamwambia Yoshua, aangalie kutenda sawasawa na sheria yote
aliyokuwa ameamriwa na Musa mtumishi wake Mungu. Swala kuu hapa ni
utii wa neno la Mungu. Kwamba kijana hatarajiwi kuwa msikilizaji tu wa
Neno la Mungu na kuendelea na maisha ya kidunia. Kijana anahitajika
kuwa msikiaji na mtendaji/mtekelezaji wa maagizo ya Mungu ndani ya
Neno.
Mungu anasisitiza katika mstari wa nane kuhusu kutafakari Neno. Mungu
alimtaka Yoshua, kuhakikisha siku zote za maisha yake anafanya Neno la
Mungu kuwa sehemu ya maisha yake. Alimtaka akiwaza awaze (atafakari)
Neno mchana na usiku, maongezi yake yawe na msingi katika Neno. Kuhusu
kutendea kazi Neno, Mungu alimwambia Yoshua aangalie kutenda sawasawa
na maneno yote yaliyoandikwa humo (ndani ya torati/Neno.
”Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari
maneno yake mchana na usiku upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno
yote yaliyoandikwa humo…."(Yoshua 1:8).
Kwa maana hiyo, iwe usiku iwe mchana kijana saa zote unatakiwa
kutafakari neno la Mungu siyo kuwaza shida, taabu na masumbufu ya
dunia hii. Kulitafakari Neno huja baada ya kulisoma, Daudi alisema:
”Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi“ (Zab.
119.11).
Alilisoma na kisha akalihifadhi moyoni. Neno hilo katika hazina ya
moyoni, likawa mshauri, mwongozo na faraja wakati wa majaribu, mapito
au mateso. Na kwa kulitamka likafanyika fimbo ya kumwangamiza adui, na
kufungua milango ya baraka iliyofungwa na adui na pia likatumika hata
kubadilisha mazingira kama Ezekia alivyotamka uhai kwa mifupa,
ikainuka ikiwa hai na kuwa kikundi kikubwa cha watu.
Ili uwe na maisha yenye mwelekeo wa ki-Mungu na ya mfano, epuka kabisa
kuwaza mambo mapotofu, epuka mazungumzo mafu yasiyo na uhai wa ki-
Mungu maana yatakuharibu wewe pamoja na wakusikilizao, pia matendo
yoyote yaliyo kinyume na Neno la Mungu epukana nayo. Mungu alijua kuwa
kijana huyu Yoshua asiposisitiziwa na Mungu mwenyewe, asipoishi kwa
Neno ambalo ndiyo lishe bora ya roho yake, angeharibikiwa, na hapo
kusudi la Mungu la ukombozi wa wana wa Israel lingeyumba. Hali
kadhalika wewe usipoishi kwa kulitii Neno na kufanya kama
linavyokuagiza, adui atayumbisha mpango wa Mungu katika maisha yako,
matokeo yake ni kuchanganyikiwa, kukata tamaa na hata kufa kabisa
kiroho. Lakini ukisimama pasipo kujali mazingira yanayokuzunguuka,
Mungu anao mpango mzuri sana na maisha yako na ndiyo maana amekuokoa
(amekuita). Yumkini wewe ndiye wa kwanza kumpa Yesu maisha yako katika
familia au ukoo wako. Mungu anategemea kukutumia wewe kulifikisha
kundi hilo nchi ya ahadi kama alivyomtumia Yoshua. Zoezi hilo
litafanikiwa iwapo utakuwa hodari tu na mwenye ushujaa mwingi, na
kutenda sawasawa na Neno kama linavyoletwa kwako na Roho Mtakatifu
mwenyewe kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujumbe huu
unaousoma sasa.