LAANA:
Mara nyingi wapendwa tunaposoma habari ya laana tunaichukulia kama
jambo jepesi na kuona kuwa laana hizi ni kama hazipo ama hazitupati na
ndio maana watu tunaendelea kucheza na mambo ya Mungu. Lakini leo
nataka kukuonyesha kuwa laana hizi zipo na zinaonekana wazi wazi
katika maisha yetu. Mambo mengine yanaonekana kama ya kawaida katika
maisha yetu lakini kimsingi mambo hayo hayatakiwi kuwapata watu wa
Mungu. Hebu sasa tuangalie baadhi ya laana ambazo Mungu amesema. Nabii
Hagai anaanza kwa kusema, ”Basi sasa Bwana wa majeshi asema hivi,
zitafakarini njia zenu“ (Hagai 1:5) Maana mambo haya yanatokea kwenu;
soma mstari wa 6.
Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa lakini hamjazwi na vinywaji. Hii ni
hali ya kutotosheka na chakula maana unakuta mtu anakunywa na kula
lakini baada ya masaa kadhaa anakula na kunywa tena.
Jambo hili linaharibu bajeti yake kwa kujikuta ametumia hela nyingi
kwenye chakula bila sababu ya maana. Bwana anao uweza wa kuondoa hiyo
nguvu ya tamaa ya kula na kunywakunywa ovyo na kukufanya utosheke na
chakula kidogo na cha kawaida.
Mnajivika lakini hampati joto. Hii ni tamaa ya mavazi. Mtu anajikuta
hataki nguo au mtindo wa mavazi umpite japo hata kama uwezo wa kufanya
hivyo hana. Sisemi kwamba kuvaa ni vibaya lakini lazima tuwe na kiasi
na hasa wakati ambapo kipato chetu hakijafikia hatua ya kwenda na
fashion.Watu wengi bajeti zetu zimeathiriwa na tamaa ya mavazi.
Yeye apataye mshahara anaweka katika mifuko iliyotoboka toboka. Hii
ndio mbaya kuliko zote maana kuna wakati mtu unafanya kazi na kupata
mapato yako lakini baada ya siku mbili tatu pesa yote imekwisha na
wala ulichofanya cha maana hakionekani na wakati mwingine ni rahisi
kuona kuwa labda mtu amekuibia.
Mlitazamia vingi vikatoka vichache, tena mlipovileta nyumbani
vikapeperushwa. Kuna wakati mwingi tunafanya kazi na pengine ngumu
sana tukitazamia kupata kipato kikubwa lakini matokeo yake yanakuwa
madogo. Pengine tunafanya biashara lakini faida inatoka kidogo sana.
Pengine tunafanya kazi kwa bidii lakini mabosi wetu ndio kwanza
wanatudharau.
Mbingu zimezuiliwa zisitoe umande na nchi isitoe matunda. Hii inatokea
pale ambapo nguvu ya Bwana ya mbaraka inapokuwa haipo juu yako. Hivyo
hata kama utafanya biashara yaani utapanda mbegu (Mtaji) hutafanikiwa.
Kumbukumbu la Torati 28:15 – 68
* Mstari wa 21 – 22: Bwana atakuambatanisha na tauni
* Mstari wa 23: Mbingu zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba
na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma
* Mstari wa 24: Bwana atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na
mchanga
* Mstari wa 28: Bwana atakupiga kwa:
1. Wazimu
2. Upofu
3. Bumbuwazi la moyo
4. Utakwenda kwa kupapasa papasa
5. Hutafanikiwa katika njia zako
6. Utaonewa na kutekwa nyara
* Mstari wa 32: Wanao na binti zako watapewa taifa jingine
* Na macho yako yataangalia na kuzimia kwa kutamani mchana kutwa
* Hapatakuwa na kitu katika uwezo wako
* Mstari wa 33 Matunda ya nchi yako na taabu yako yote vitaliwa na
taifa usilolijua
* Mstari wa 37 – 40 Wewe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau
kati ya mataifa, mbegu nyingi utapanda shambani lakini utavuna haba
kwa kuwa nzige watazila.
* Mstari wa 43 Mgeni aliye katika nchi yako atazidi kupaa na wewe
kushuka
* Mstari wa 44 Yeye atakuwa kichwa na wewe mkia
* Mstari wa 48
* Mstari wa 49 - 51 Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali,
kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai, taifa usilolifahamu ulimi
wake, taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala
halipendelei kijana. Naye atakula uzao wa ngombe zako uzao wa nchi
yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa, wala hatakuachia nafaka ,wala
divai, wala mafuta, wala maongeo ya ngombe wako, wala mwana kondoo
wako mpaka utakapokwisha kuangamizwa
Yeremia 5:1– 9
Hebu sasa tuangalie maisha ya wapendwa wengi makanisani mwetu. Watu
wengi ndani ya makanisa ya watu tuliookoka tumetembea chini ya laana
hizi kwani ni kweli kwamba wapendwa wengi maisha yetu kwa ujumla wetu
ni duni sana. Laana ambayo imesemwa katika Kumbukumbu la Torati 28:28
ndio hasa imetawala ndani ya watu wa Mungu. Wengi tumepigwa na upofu
hatuoni chochote cha kutuendeleza katika maisha yetu. Wakati watu wa
mataifa wanaona mambo makubwa, wanavumbua miradi mikubwa, watu
waliookoka kwa sababu ya kutokwenda sawasawa tumejikuta kuwa hatuoni
chochote kile. Kwa ujumla, wapendwa, laana hizi zipo na zinatembea
ndani ya watu wa Mungu. Yatupasa kuamua kama alivyosema Joshua: Hakuna
jinsi ya kupona, njia pekee ni kujisalimisha kwa Bwana Mungu wetu.
BARAKA
Baraka ni nguvu ya Mungu ya uwezeshaji wa Mungu katika maisha ya mtu.
Kweli sisi tuliookoka tunaposema habari ya baraka tunakuwa tunasema
habari ya Mungu kuachilia nguvu au uwezeshaji ndani ya maisha yetu.
Kumbukumbu la Torati 8:18 ”Bali wewe utamkumbuka Bwana Mungu wako
maana yeye ndiye akupaye nguvu ya kupata utajiri.“ Katika eneo hili
neno nguvu lina maana ya:
-ufahamu
-maono
-kibali
-uvumilivu
-bidii pamoja na mambo mengine ambayo yatakufanya wewe kupanda juu kwa
haraka ambayo Mungu ameikusudia.
Kila mtu aliyeokoka anatakiwa kuwa na nguvu hii kusudi aweze
kufanikiwa katika maisha yake. Panapokuwepo hii nguvu, maisha ya mtu
aliyeokoka katika hali yeyote lazima yatabadilika na kuwa mazuri zaidi
ya yalivyokuwa mwanzo. Hivyo kila mtu aliyeokoka yampasa kuitafuta na
kuhakikisha nguvu hii ipo kwake.
MFANO WA NGUVU (BARAKA)
* Yusufu alikuwa mtoto mdogo miaka 17 tu
* Alikuwa anafanya kazi ndogondogo za nyumbani,
* Alipenda kukaa na wazazi wake
* Yusufu alimcha Bwana naye alichukia dhambi na ndio maana
alipendwa na Mungu. (Mwanzo sura 39). Ndugu zake Yusufu walimchukia
sana Yusufu, nao wakamuuza, naye akaenda kuwa mtumwa.
YUSUFU KAMA MTUMWA
Katika hali ya kawaida Yusufu alikuwa kama watumwa wengine tu, lakini
kwa Yusufu ilikuwepo nguvu ya Mungu (uwezeshwaji wa Mungu). Mstari wa
2 ”Bwana akawa pamoja na Yusufu“ Uweza wa Bwana wa kustawisha ulikuwa
pamoja na Yusufu.
KAZI YA UWEZA HUU
Nguvu hii huleta ustadi wa kazi
Yusufu alipewa ustadi wa kazi, wakati wowote Yusufu alipopewa kazi
aliifanya kama bwana wake (Potifa) alivyotaka, na hivyo kuufurahisha
moyo wa bwana wake (Potifa). Mwanzo 39:3”bwana wake akaona ya kwamba
Bwana yu pamoja naye ,na ya kuwa Bwana anafanikisha mambo yote mkononi
mwake.“ Nguvu hii ni ya muhimu sana katika maisha yetu. Nguvu hii ni
ya muhimu katika biashara zetu na kazi za aina yoyote.Tutakapoweza
kufanya kazi au biashara kwa ustadi, na kwa akili ya KIMUNGU, basi jua
mafanikio ni makubwa sana.
Nguvu hii huleta kibali.
Mwanzo 39:4. ”Yusufu akaona neema machoni pake akamtumikia“ Kibali ni
jambo muhimu sana kwetu sisi ikiwa ni kazini ama kwenye biashara,
maana watu wakitupenda ndivyo watakavyokuja kwa wingi kwenye biashara
zetu, na mabosi wetu watatuwazia mema wakati wote. Tutakapoingia
sehemu yeyote na kusema neno au tendo basi tutaonekana sisi kwanza
Nguvu hii huleta bidii
Tunaona Yusufu alivyofanya na kumaliza kila kazi aliyokuwa amepangiwa
na hivyo bosi wake kuona ampe majukumu makubwa zaidi. Kama Yusufu
angekuwa stadi na ana kibali lakini kazi zinalala, bwana wake
asingempa majukumu makubwa.
Nguvu hii huleta uvumilivu
Wote tunafahamu maisha ya mtumwa, hutumwa hovyo, hupewa kazi nyingi,
tena ngumu, lakini Yusufu alivumilia akachapa kazi na watu wale
wakashangaa. Pamoja na mengine mengi nguvu ya Bwana ilimfanya Yusufu
kuonekana si mtu wa kawaida katika nyumba ya Potifa.
Nguvu hii huatamia yale ambayo tunayafanya,
Mstari wa 5 ”…mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo
katika nyumba na katika shamba.“ Kusudi uweze kufanikiwa unatakiwa
kuwa na nguvu hii juu yako.Mungu wa Yusufu ndiye Mungu wetu; kama
alivyokuwa na Yusufu ndivyo atakavyokuwa na sisi pia. Jambo la
kukumbuka: palipo na mbaraka huu haijalishi wewe ni wa namna gani.
Katika sehemu zote mbili alizopitia Yusufu, ya utumwa na ufungwa
utaona mwisho wa Yusufu ni juu sana.
Hali uliyo nayo isikufanye kukata tamaa bali tafuta mbaraka wa Bwana
uwe maishani mwako. Kutokusoma, kutokuwa na mtaji, kutokuwa na refa,
sio sababu ya kukufanya wewe kutokufanikiwa maana wewe ni mtu ambaye
unawezeshwa na NGUVU maalum ya Mungu katika maisha yako. Nguvu hii
tunaiona tena katika maisha ya Yakobo nyumbani kwa Labani, Mwanzo
30:25-43
Yakobo hakuwa na mahari ya kukomboa wake zake na watoto wake kusudi
aweze kwenda kuishi mwenyewe, hivyo aliamua kufanya kazi nyumbani kwa
mkwe wake Labani. Lakini tunaona wazi tangu mwanzo wakati Yakobo
amefika kwa Labani. Labani hakuwa tajiri kama baada ya kukaa na
Yakobo. Utajiri wa Labani ulipatikana baada ya mtu mwenye nguvu ya
Baraka ya Mungu kushika mali zake. Mstari wa 27, ”…maana nimetambua
ya kwamba Bwana amenibariki kwa ajili yako“
Mstari wa 30. ”Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja…Bwana
akakubariki kila nilikokwenda“
Mtu wa Mungu ambaye nguvu ya Mungu ya ongezeko imo ndani yake
anapofanya jambo lazima hilo jambo lifanikiwe sana. Baada ya Yakobo
kuwa na wanyama wake na Labani kuwa na wanyama wake, nguvu ya Baraka
ya ongezeko ilikuwa juu ya wanyama wa Yakobo, hivyo basi Yakobo
aliongezeka sana mpaka ukoo wa Labani ukaanza kumuonea wivu. Mwanzo
30:43, ”Kwahiyo mtu huyo akazidi mno akawa na wanyama wengi na
wajakazi na watumwa na ngamia na punda.“ Mungu wa Yakobo ndiye Mungu
wetu.
Yesu anapofundisha habari ya nguvu hii anasema. ”…msisumbuke basi
mkisema,
(1)Tule nini, (2)Tunywe nini, (3)Tuvae nini?“ (Mathato 6:24-33).
Mstari wa 35, Maana watu wasio na Mungu, wasio na nguvu hii ya baraka
kutoka kwa Mungu hao ndio wanaosumbuka. Lakini sisi Baba yetu wa
mbinguni anajua kuwa tunataka hayo naye ataleta nguvu hiyo ya
kutuwezesha ili kutufanya tuwe nayo yote tunayoyahitaji. Mstari wa 33.
Hivyo basi utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na hiyo nguvu na yote
yatakuja.
Mwandishi wa Zaburi anasema katika Zaburi 1:1-3:
Heri, amebarikiwa, amepewa nguvu, atafanikiwa mtu yule, aitendaye
sheria ya Bwana. Mstari wa 3, kila alitendalo litafanikiwa.
Wapendwa yatupasa kwanza kuitafuta hiyo nguvu ndipo tutakapoona mambo
makubwa na ya ajabu yakitendeka maishani mwetu. Wana wa Mungu yatupasa
kuelewa kuwa (BARAKA) nguvu hii ya kutuwezesha ni roho kamili toka kwa
Mungu kama tunavyoona Mungu mwenyewe anamwambia Musa katika kitabu cha
Kutoka 31:3 - 4 Nimejaza Roho ya Mungu ndani yake. Roho hii ya Mungu
ambayo Mungu ameweka au anaweka ndani yetu inaleta mambo yafuatayo
- Hekima
- Maarifa
- Ujuzi wa mambo ya kazi za kila aina
Kutoka 35:31–35. Naye amejaza Roho ya Mungu katika
- Hekima
- Akili
- Ujuzi
- Kazi za ustadi
- Kuvumbua kazi za werevu
- Amejazwa akili za moyoni.
Roho hii itakapokuwapo juu yako nataka kukwambia huwezi kuwa masikini
lazima neno la Mungu litimie kwako lile linalosema ”Na watu wote
watakuita mbarikiwa“ Nguvu hii au Roho hii kamili toka kwa Bwana
haitolewi kwa upendeleo bali ni kwa kila mtu aliyeokoka na kukubali
kutembea katika njia za Bwana. Kumbukumbu la Torati 28:1-2 Bwana
anaweka msimamo jinsi ya kupokea nguvu hii ya muhimu kwenye maisha
yetu; anasema ”Itakuwa utakapoisikia sauti ya Bwna, Mungu wako, kwa
bidii, kutunza kufanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana
Mungu wako atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya dunia na Baraka hizi
zote zitakujilia na kukupata“
Hebu tutazame mambo yafuatayo:
1. Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana Mungu wako
2. Kwa bidii
3. Kutunza kufanya maagizo yake yote
Matokeo:
Ndipo baraka (Nguvu) hizi zote zitakujilia na kukupata Isaya 1 :19
”Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi.“ Warumi 2:10 ”Bali
utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema…“
(Mambo ya Walawi 26:3 – 13, Kumbukumbu la Torati 8:12 – 15). Pamoja na
maandiko mengine mengi utaona ya kuwa siri kubwa ya kupata mbaraka au
nguvu hii ni kutenda sheria ya Bwana. Hapo juu tumeona mambo matatu
muhimu ambayo Mungu anataka kwetu.
1. Kusikia sauti ya Bwana, kinyume sana na tulivyozoea watu wengi
tunapokuwa na pilika ya kutafuta pesa tuna kosa muda wa kuja kanisani
kwenye mafundisho na hata tukirudi nyumbani tumechoka hatuwezi kusoma
Neno. Lakini kumbe kama tunataka kuendelea yatupasa kujitahidi sana
kusoma Neno na kuhudhuria mafundisho. Ndani ya Neno utaona wazi wazi
yale ambayo Mungu anataka tufanye na yale ambayo Mungu hataki tufanye.
2. Kwa bidii, tunaona tena wazi pale ambapo tunatafuta pesa, watu
wengi tunaweka bidii sana kwenye pesa , lakini sharti la Bwana
linasema tulitafute Neno kwa bidii sana.
3. Kutenda sawasawa, tunapaswa kutenda sawaswa na yale ambayo Mungu
ametuagiza kutenda
Tutakapokuwa tumefanya mambo hayo tutaona wazi wazi nguvu ya Bwana ya
mbaraka ikiwa juu yetu .
Maombi.
Hatuwezi kuwa na kiu na bidii ya kusoma Neno pamoja na kutenda
sawasawa kama tutakuwa sio waombaji. Maombi ndio njia pekee ya
kutupatia nguvu za kuweza kuyatenda hayo. Kwa kifupi kabisa niseme
hivi nguvu ya Mungu ndani ya maisha yetu italetwa na mambo makuu
matatu
- Kusoma neno kwa bidii
- Kutenda sawa sawa na neno
- Kuomba kwa bidii
Baada ya kuona mambo ambayo yatatupata tutakapokuwa chini ya laana ama
tutakapokuwa chini ya mbaraka wa Mungu tutazame sasa neno MTAJI.
MTAJI
Wana wa Mungu tunapoongelea mtaji, watu wengi wanafikiri tunataka
kuzungumzia pesa na wanakuwa wapo sawa kabisa. Lakini leo nataka
kukupa jambo la msingi kwetu sisi watu wa Mungu.
Kwetu sisi watu wa Mungu mtaji wetu wa kwanza ni kuhakikisha nguvu ya
Mungu ya mbaraka (baraka) ipo kwetu.
Nguvu hii inapokuwepo kwetu swala la pesa sio tatizo.
Tunajifunza neno hili kwa Yakobo katika kitabu cha Mwanzo 29 na 30.
tunaona wazi wakati Yakobo anakwenda kuoa hakuwa na pesa ya kulipa
mahari hivyo alilazimika kulipa mahari ya nguvu zake na hivyo
alitumika miaka kumi na nne ili kupata wake wote wawili.
Katika miaka yote kumi na nne Yakobo aligundua kuwa nguvu ya Bwana ya
mbaraka ilikuwa juu yake na ndio maana Labani alipomwambia kwamba sasa
nitakulipa mshahara aligoma. Alijua kwamba mshahara ungezuia nguvu ya
Bwana ya kumuongeza na kumkuza. Mwanzo 30:30 ”Maana mali yako ilikuwa
haba kabla sijaja, nayo imezidi kuwa nyingi. Bwana akakubariki kila
nilikokweda…“ Kwa maana nyingine Yakobo anamwambia Labani ”Nguvu ya
Bwana iliyo juu yangu ndio imekuongeza kiasi hiki ulichonacho, sasa
wewe utanilipa nini cha kutosha?“
Mstari wa 31, ”Akamwuliza, Nikulipe nini? Yakobo akasema USINIPE
KITU“.
Yakobo akijua kuwa nguvu ya mbaraka ya Bwana ipo juu yake alitaka mali
kidogo toka kwa Labani na Labani bila kufahamu hilo alikubali kwa
urahisi kabisa. Soma mstari wa 32-33 .
Katika mstari wa 43, Biblia inasema, ”Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno,
akawa na wanyama wengi…“ Utajiri tayari.
Wapendwa, nguvu ya Mungu ya mbaraka inapokuwapo upande wetu chochote
kile kinachotuzunguka ni mtaji tosha.
Katika hali hii tuliyonayo yatupasa kutafuta nguvu ya Mungu ya mbaraka
kwanza kabla ya mtaji wa pesa. ”Tafuteni ufalme wa Mungu kwanza na
haki yake yote mengine yote mtazidishiwa“ Yesu anaendelea kusema
”Msisumbuke kama mataifa.“ Kwa maneno haya sisemi tusitafute pesa,
pesa tutafute lakini yatupasa kujua kuwa pesa sio msingi wa maendeleo
kwetu sisi tuliookoka. Kwetu sisi kitu cha kwanza ni kibali cha Mungu
katika maisha yetu. Ni nguvu ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku.
Neno la Mungu linasema katika Kumbukumbu la Torati kwamba Mungu ndiye
atupaye nguvu za kupata utajiri. ”Bali utamkumbuka Bwana Mungu wako,
maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri…“(Kumb 8:18).
Hatua ya pili ni pesa
Baada ya nguvu ya Mungu kuwepo kwetu nasi tukaanza na chochote kidogo
kilichopo, hata kama ni kibaya, au cha fedheha, tutaona Bwana
anatufanikisha, na yale mapato yanayoingia ndio unakuwa mtaji wetu
mzuri wa kuanzia.
Fedha yoyote tunayopata yatupasa kuitenga au kuiweka katika makundi
matano muhimu. Yaani fedha kwa ajili ya:
* Zaka (Fungu la kumi)
* Sadaka (Dhabihu)
* Mtaji
* Akiba
* Chakula.
Mtaji lazima uongezeke kila wakati tunapohesabu faida. Kwa maana hiyo
basi tunapokuwa tayari tumepata faida yatupasa kutenga kiasi cha fedha
yetu na kuiweka kwenye mtaji. Kwa mfano: Nilianza biashara bila kitu
pale Kamanga Feri; nilianza nikiwa mpiga debe tu. Samaki zinapoletwa,
mimi nachukua toroli na kuanza kuuza huku mwenye samaki hizo amekaa
tu. Chochote nachopata kwa siku au kwa wiki lazima nitenge sehemu
kidogo ya mtaji. Ikiwa makubaliano yetu ni kuwa kila samaki nitakaye
muuza yeye atanipa shilingi 100 basi nikiuza samaki 50 ninapata
shilingi 5,000 kwa siku. Kwa wiki shilingi 5,000 x 6 = 30,000.. Kwa
mwezi 30,000.00 x 4 = shilingi 120,000.
Kwahiyo hizo shilingi 120,000 zinapaswa kugawanywa katika yale mambo
matano muhimu (zaka, sadaka, mtaji, akiba na chakula).
Nguvu ya Mungu inapokuwepo, kiasi kidogo tu cha pesa chatosha kuwa
mtaji wa kutuletea mambo makubwa. Mtaji mkubwa wa pesa ni kitu cha
muhimu sana lakini kisiwe kizuizi kwetu sisi kuanza kufanya yale
ambayo tunakusudia kufanya katika maisha yetu.
Yakobo akijua kuwa anayo nguvu ya Mungu ya mbaraka maishani mwake
anamwambia Labani, sitaki unilipe pesa ”nipe lile kundi dogo la
wanyama wenye marakaraka hao ndio utakuwa mshahara wangu.“ Labani bila
kujua hilo anamkubalia Yakobo. Na Yakobo mwenye nguvu ya Mungu anaanza
na yale machache na mwisho wake tunaona Yakobo anakuwa tajiri.
Hivyo nakushauri wewe uliyekata tamaa na maisha, hapo ulipo na kipato
ulichonacho chatosha kukufanya wewe kuwa tajiri sana sana.
Tunapokuwa tumeanza kupata pesa yatupasa kujua kuwa kilichotuwezesha
ni nguvu ya mbaraka maishani mwetu na sio ujanja wetu, hivyo ni
lazima tuhakikishe kuwa tunaitunza hiyo nguvu ya Mungu ya mbaraka
maishani mwetu. Na ili kutunza hiyo nguvu maishani mwetu yatupasa
kufanya mambo yafuatayo.
1. KUTOA ZAKA
(i) Zaka ni sehemu ya kumi (10%) ya mapato yako yote, ambayo Neno
linasema ni mali ya Bwana. Mambo ya Walawi 27: 30 ”tena zaka yote ya
nchi kama ni mbegu ya nchi au kama ni matunda ya nchi ni ya Bwana, ni
takatifu kwa Bwana.“
(ii) Zaka itolewe wapi?
Hesabu 18: 21 ”Na wana wa Lawi nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa
urithi wao badala ya huo utumishi wautumikao, maana ni utumishi wa
hema ya kukutania.“
Hesabu 18:24 ”Kwakuwa zaka ya wana wa Israeli waisongezayo kuwa zaka
ya kuinuliwa kwa Bwana n mewapa Walawi kuwa urithi wao …“
Kumbukumbu 18: 1-5. Mstari wa 1 ”makuhani Walawi kabila yote ya Lawi
wasiwe na fungu wala urithi pamoja na Israeli watakula sadaka za
Bwana...“ Zaka ni kwa ajili ya MAKUHANI WALAWI. Maana wao hawakupewa
urithi (mashamba wala ajira) bali Bwana ndiye urithi wao kwa hiyo zaka
unatoa kanisani kwako unapopata malisho ya kiroho na anakula Mchungaji
wako yule anayeilea roho yako na atumikaye mbele ya madhabahu ya Bwana
kwa ajili ya roho yako.
(iii) Sababu ya kutoa zaka.
Malaki 3 : 10-12
(a) Ufanye chakula kiwemo kwa wingi nyumbani mwa Bwana. Zaka
hutolewa kwa Bwana lakini anayekula ni Mchungaji wako, pale unapopokea
malisho. Kama tulivyoona watumishi wa Mungu hawana urithi, Bwana ndiye
urithi wao, hivyo chakula kinapokuwepo tele nyumbani mwa Bwana
unamfanya Mchungaji wako kutulia na kutafuta malisho ya kutosha
kwaajili ya Kanisa. Nehemia 13: 10-12 mstari wa 10 ”Tena nikaona ya
kwamba Walawi hawakupewa sehemu zao, basi wamekimbia, Walawi na
waimbaji, waliofanya kazi kila mtu shambani kwake.“ Unapoacha kutoa
zaka unasababisha mchungaji wako badala ya kutafuta malisho kwa ajili
ya kondoo, atafute kazi ya kumpatia chakula na kwa hiyo kanisa
litakosa malisho bora na hasira ya Bwana kuwaka juu ya kanisa
(b) Zaka huonyesha ni kiasi gani mtu anamcha Bwana kwa mapato yake.
Kumbukumbu 14: 22- 23, Mithali 3:9 ”Mheshimu Bwana kwa mali yako na
kwa malimbuko ya mazao yako yote.“
(c) Unapotoa zaka unasababisha Bwana kufungua madirisha ya mbingu
tayari kumwaga baraka tele Malaki 3:10d ”…mjue kama sitawafungulia
madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka hata isiwepo nafasi ya
kutosha au la ..“
(d) Unapotoa zaka pia Bwana anawafukuza maadui wafuatao: Malaki 3: 11
(i) Alaye
(ii) Aharibuye mazao yenu
(iii) Apukutishaye mazao yenu kabla ya wakati
Toa zaka usifanye nyumba ya Mungu kuachwa na Walawi (makuhani) hata
wasipoiacha Mungu hashindwi kuwalisha au kuwahudumia, bali laana
itakuwa juu yako wewe. Kumbukumbu 28:23 ”… na mbingu zako zilizo juu
ya kichwa chako zitakuwa shaba na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma“
Soma pia Hagai 1:4–11. Hayo ni matokeo ya kudharau nyumba ya Bwana.
2. KUTOA SADAKA
Sadaka ni kiasi cha mali zetu ambacho mtu anatoa kwa Mungu kwa hiari
yake mwenyewe
kulingana na vile ambavyo mwenyewe amependa au amemthamanisha Mungu
wake. Paulo ameifananisha sadaka na mbegu, inapotolewa ni sawasawa na
kupanda mbegu ndani ya shamba.
2 Wakorintho 9;1-14. Hivyo chukua moyoni mwako picha hii kwamba kutoa
ni kupanda na sadaka yako ni mbegu inayopandwa ndani ya shamba. Katika
mstari wa 6 Neno la Mungu linasema, ”Apandaye haba atavuna haba,
apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.“ Ukarimu ni nini? Ni moyo wa
kumwaga kwa wingi, pasipo kuzuilia. Mithali 11;24-25 ”Kuna atawanyaye,
lakini huongezewa zaidi, kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea
uhitaji. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshae atanyweshwa
mwenyewe.“ Mithali 19:17 ”Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye
atamlipa kwa tendo lake jema“
Hivyo sharti la kwanza tunapokwenda kupanda mbegu zetu yatupasa kujua
kuwa lazima tupande kwa wingi, mwenye kipimo kimoja apande kwa wingi
katika kipimo alicho nacho, mwenye vipimo kumi apande kwa wingi kwenye
vipimo vyake kumi, mwenye vipimo ishirini, hamsini, mia kila mmoja
lazima apande kwa wingi. Kumbuka hatupandi kwa kutazamana, bali kila
mmoja anapanda kwa kadiri ya kipimo alichonacho na katika kipimo
ulicho nacho panda kwa wingi.
2 Wakorinto 9;7 ”Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake,
si kwa huzuni wala si kwa lazima, maana Mungu humpenda yeye atoaye
kwa moyo wa ukunjufu.“
Sharti la pili juu ya sadaka yetu, ni lazima iwe kwa moyo wa kupenda,
hiyari ya moyo, ndiyo tabia yetu kutoka ndani. Ukweli kama tunataka
kufanikiwa na kuona nguvu ya mbaraka inatukalia yatupasa kujijengea
tabia hii maishani mwetu, kufurahi na kushangilia wakati wa kutoa,
maana tunajua kutoa ni kupanda mbegu.
Mambo manne ya kutazama
(1) Kusudi la moyo
(2) Sio kwa huzuni
(3) Sio kwa lazima
(4) Kwa moyo wa ukunjufu
Mungu anapoyaona mambo hayo ndani yamaisha yetu.
(i) Unapanda kwa wingi
(ii) Unalo kusudi la kupanda wakati wowote unapoona shamba
(iii) Hupandi kwa huzuni
(iv) Hupandi kwa lazima,
(v) Unapanda kwa moyo wa ukunjufu.
Kwa ujumla Bwana anapoona hayo ndiyo maisha yako kutoka ndani anafanya
yafuatayo;
(a) Anakujaza kila neema kwa wingi. Neema ni Nguvu/uweza unaomfanya
mtu kuweza kufanya jambo ambalo alikuwa hawezi kulifanya.
(b) Unakuwa na riziki za kila namna. Anamwaga Roho ya Mungu ndani yako
kusudi uongezeke na kuwa na riziki za kila namna.
(c) Upate kuzidi sana katika kila tendo jema, anakuzidishia ili na
wewe uzidi sana katika kutenda mema. 2 Wakorintho 9; 10 ”Na yeye
ampaye mbegu mwenye kupanda,na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za
kupanda na kuzizidisha, naye ataongeza mazao ya haki yenu.“
Tunapopewa kipato katika hali yoyote ile, yatupasa tujue katika kipato
hicho, kuna mambo mawili,
(i) Kuna mbegu ya kupanda na
(ii) Kuna mkate wa kula.
Tutakapotambua haya basi, yatupasa kujua mambo yafuatayo yanatokea:
Atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha. Pili, ataongeza mazao ya haki
yenu. Matokeo ya kupanda mbegu ni Bwana kuzizidisha na kuongeza mazao
yako. Katika mstari wa 11 imeandikwa, ”mkitajirishwa katika vitu
vyote.“ Yaani matokeo ya kupanda mbegu ni watu wa Mungu kutajirishwa
kila upande katika vitu vyote. Sadaka, Dhabihu, mbegu ni vitu vya
muhimu sana kwa mtu uliyeokoka ambaye unataka kufanikiwa na
kuongezeka. Tunapokuwa tumetoa sadaka au dhabihu kwa moyo wa kupenda
na kwa wingi Bwana atatuongeza kwa
* kutumwagia Roho yake juu yetu.(Ujuzi na ustadi mkubwa wa
kuyafanya yale tunayoenda nayo)
* Kuongeza ufahamu (Maono makubwa)
* Kibali
3. MAOMBI
Kwa sababu adui yetu shetani anajua kuwa hawezi kutushinda tunapokuwa
na Bwana, anajaribu kutufanya tuache kufanya mapenzi ya Mungu maishani
mwetu.
Wapendwa sio rahisi wala sio jambo la mchezo mtu kutoa fungu la kumi,
ni pale tu mtu anapokua na nguvu ya Mungu ya kumuwezesha maishani
mwake ndipo mambo mengine yanaonekana kuwa rahisi.
Sio rahisi kutoa ili kuwasaidia wajane na yatima, na kupeleka injili,
pasipo mtu kuwa na nguvu ya Mungu maishani mwake. Na nguvu hii ya
Mungu tunaipata kwenye maombi. Pasipo maombi hatuwezi kupata nguvu ya
Mungu ya kutusaidia kutenda mema.
Kwa kifupi unaposikia sadaka na fungu la kumi jua kuwa ni NGUVU ya
Mungu katika utu wetu wa ndani ndiyo inayotuwezesha kutenda hayo.
Pia watu wengi wameshindwa kufanya mambo makubwa katika maisha yao
kwasababu ya kushindwa kwenye vita na roho za upinzani. Wapendwa, zipo
roho za upinzani sana katika maisha yetu hasa tunapokuwa tunakwenda
kwenye mambo yatakayomletea Bwana utukufu. Zipo roho za kukatisha
tamaa, kuvunja moyo, kuzuia, zote hizi kiboko yake ni maombi makali.
Maana maombi hushusha nguvu za Mungu, huvunja mapingu, huvunja kuta.
Hivyo pamoja na kufanya biashara kama watu wa Mungu yatupasa kujua
kuwa maombi ni ya muhimu sana sana.
4. KUFANYA KAZI KWA BIDII
Wapendwa kama tulivyoona Bwana amekuwa akiwabariki wale ambao wamekuwa
wakifanya kazi kwa bidii, maana tunaona Mungu analeta nguvu ya
kutuwezesha, na sio kumwaga baraka kama mvua.
Neno la Mungu linasema katika Zaburi 1-3 ”…Na kila atendalo
litafanikiwa“ Tunapokuwa tunafanya jambo ndipo Mungu analeta
uwezeshaji katika yale ambayo tunayafanya. Kumbukumbu la Torati 28:8
”Na mambo yote utakayotia mkono wako“ yatafanikiwa. Mstari wa 12 ”Na
kubariki kazi ya mkono wako.“ Yatupasa kufanya kazi kwa mikono yetu
ndipo tutaona nguvu ya mbaraka inakuwa pamoja nasi na kutufanikisha
Jambo tunalotakiwa kujua ni kuwa tunapofanya kazi yatupasa kufanya
kazi kwa bidii pasipo ulegevu wala kujionea huruma. Tunaona hata
Yusufu pamoja na nguvu ya Mungu kuwa juu yake lakini alifanya kazi
kwa uwezo wake wote. Mwanzo 39 Biblia inasema Yusufu alipewa kazi zote
za nyumbani na shambani na alifanya akamaliza. Kuna maandiko mengi
yanayotuonyesha kuwa mtu mwenye bidii atafanikiwa sana. Mithali 10:4;
Mithali 12:24; Mithali 13:4; 1 Wafalme 11:28; Mithali 22:29; Mithali
6:6-11.
Wapendwa wengi tunakosa bidii katika mambo yetu na ndio maana
hatufanikiwi.
Jambo jingine la muhimu ni kutochagua kazi. Yatupasa kuwa tayari
kufanya kazi yoyote huku tukijua kuwa ndio mwanzo wa mbaraka wetu
Katika kitabu cha Ruthu tunaona wazi wakati Ruthu alipokuwa na shida
alikwenda kufanya kazi ya chini kabisa lakini mwisho wa Ruthu ulikuwa
wa ajabu sana.
Ruthu 2:3a Neno la Mungu linaonyesha Ruthu aliamua kwenda kondeni
kuokota masazo nyuma ya wavunaji. Ruthu 2 3b Neno la Mungu linasema
”Bahati ikamfikia“Bahati ya Ruthu haikumkuta nyumbani wala kwenye
mkesha wala amefunga mlimani, bahati ilimkuta kwenye shughuli.
Ruthu 2:5 Mwenye shamba aliyekuwa tajiri alimwona akampenda
Ruthu 2:8-18 Ruthu akapata kibali mbele ya mwenye shamba na mambo
mengine mazuri yakaendelea mpaka maisha ya Ruthu yakawa mazuri sana
Wapendwa tusibweteke, tufanye kazi kama watu tunaoamini kwamba Mungu
anatupenda na kutuwazia mema.
5. KUWA NA MIPANGO (MALENGO)
Watu wengi tuliookoka huwa hatuna mipango (malengo). Mtu anafanya vitu
kutokana na msisimko au ameona mtu fulani amefanya au amefanikiwa ama
amesikia ushuhuda kwa juu juu kuhusu mtu fulani. Basi anaanza na yeye
kuingia pasipo mipango au kujua misingi na njia alizopitia mpaka
kufikia hapo alipo. Mara zote unapotaka jambo lolote kubwa au nzuri ni
lazima ulipangie mipango na uiheshimu mipango ile na kuitendea kazi
kwa gharama yoyote ile. Yeremia 29:11 ”Maana nayajua mawazo
ninayowawazia ninyi, asema Bwana…“ Mungu wetu ni Mungu wa mipango na
tunapohitaji baraka ni lazima tuwe na mipango juu ya baraka hizo.
Maana hata wokovu wetu Mungu aliupangia mipango tangu mwanadamu
alipokosa pale bustanini Edeni. Mwanzo 3: 15.
Kuna mipango ya maendeleo ya aina mbili
1. Mipango ya muda mfupi
2. Mipango ya muda mrefu
Mipango ya muda mfupi:
Hii ni mipango ambayo wengi tunaikimbia kwa sababu haina utukufu kwa
maana waweza kujikuta unafanya kazi au shughuli za hovyo kitu ambacho
wengi hatutaki. Lakini kwa ntu aliyeokoka ambaye anajua kuwa Bwana ni
nguvu zake yeye anakuwa tayari kwa lolote.
Mipangi hii mara nyingi ni mizuri sana kwani ina mambo yafuatayo
1. Haihitaji mtaji kubwa
2. Haihitaji elimu kubwa
3. Haihitaji kujulikana sana
4. Mara nyingi hutumika kama kianzio kwa ajili ya mambo makubwa
Mambo muhimu ya kuzingatia wakati umo ndani ya mipango hii
1. Uvumilivu mkubwa
2. Lengo lako la mbele
3. Kujituma sana
4. Katumia gharama kidogo kadiri utakavyoweza – Kwani mara nyingi
mapato yake huwa kidogo sana
5. Maombi na kusoma Neno (kuhakikisha Bwana yuko pamoja na wewe)
Mipango ya muda mrefu:
Mipangi hii ni mizuri sana kwani huzaa mambo makubwa katika maisha
yetu. Mipango hii inataka mambo yafuatayo
1. Mtaji wa kutosha
2. Elimu ya kutosha juu ya shughuli unayokwenda kufanya
3. Usimamizi wa kutosha
4. Maombi makubwa na kusoma Neno