fyi
---------- Forwarded message ----------
From: Katulanda Frederick <
fkatu...@gmail.com>
Date: Sat, 9 Jun 2012 11:32:01 +0300
Subject: [Mabadiliko ] Mwongozo kwa wafugaji wa kuku wa kienyeji
To: mabadilikotanzania <
mabadilik...@googlegroups.com>
Somo langu ni dogo lakini naamini wapo watakaopata mafanikio makubwa sana.
Sasas kuwa makini zaidi. Unaweza kuanza kwa mtaji wa Mil.1 mpaka laki tano
au hata chini ya hapo. Mfano. Unaweza kutumia Tsh 250,000 kununua kuku 25
kwa bei ya Tsh 10,000 kwa kuku mmoja (kadirio la juu) Majogoo watakuwa 5
kwa uwiano wa 1:4 . Hii ina maana kuwa wakishaanza kutaga utakuwa na
vifaranga 20 x 10 = 200 Watunze vizuri. Wale vifaranga tunakadiria kuwa
makoo(majike) watakuwa 150 ambao ndani ya miezi 3 au zaidi nao wataanza
kutaga. Utakuwa na kuku 200 + 25 =225 ndani ya miezi 6. Miezi 6 inayofuata
225 - (majogoo 55) = 170 Hii ina maana kuwa 170 x 10= 1,700. Ndugu
mwanajamvi hayo niliyotoa ni makadirio ya chini sana hivyo mpaka mwisho wa
mwaka utakuwa na kuku zaidi ya 2000. Mwaka utakaofuata utakuwa na kuku
wangapi baada ya kuuza kuku 1,000. Mwaka 2. 750(majike) x 10 = 7500 (uza
wengine) 3000 x 10 = 30,000. Kutegemea na uwezo wako mpaka mwisho wa mwaka
wa pili utakuwa umefanikiwa sana. Kumbuka huu ni mwongozo tu, fanya utafiti
na ufuatilie zaidi huku ukiacha kando uzushi wa vitabu vya wasanii na DVD
zao pia. NB. Kumbuka kuku ninao wazungumzia hapa ni wale wa kawaida sio
wale mataahira (wa kisasa).Fuatilia zaidi kuhusu matibabu na matunzo
mengineyo.
MAELEZO ZAIDI
UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI
SEHEMU YA KWANZA
UTANGULIZI
Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kwa namna moja au
nyingine kutoa mchango wangu kwa mtindo huu. Huu ni kama mwongozo tu wa
nini utakabiliana nacho au unatakiwa kufanya katika zoezi zima la ufugaji
wa kuku wa kienyeji. Nimeamua kuuleta kwenu wana JF ili kwa mtu mwenye
malengo ya kufanikiwa kupitia ufugaji wa kuku ajue mlolongo mzima na
changamoto ambazo atakabiliana nazo.
A.KWA NINI KUKU WA KIENYEJI?
1. Wastahimilivu wa magonjwa lakini ni muhimu wakikingwa na magonjwa ya
kuku kama mdondo, ndui ya kuku n.k ili kuweza kuwaendeleza.
2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini.
3. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa na kulea vifaranga na ustahimilivu
wa mazingira magumu kama ukame, baridi n.k
4.Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko kuku wa kisasa.(PATA SUPU YA
KUKU WA KIENYEJI ILI UTHIBITISHE)
5. Wana uwezo wa kujilinda na maadui kama mwewe n.k . Pamoja na sifa hizi
ni muhimu muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri, wakawekwa kwenye mabanda
mazuri, wakapewa maji na chakula cha kutosha.
B.FAIDA ZA KUKU WA KIENYEJI.
Faida ni nyingi na zinafahamika lakini nitaeleza zile ambazo kwa wengine
huenda zikawa ni ngeni kwao.
- Mayai huweza kutumika kwa tiba. (Pata maelezo jinsi yai la kuku wa
kienyeji linavyoweza kutumika kwa tiba kutoka kwa wataalam wa tiba mbadala)
- Kiini cha njano cha yai kinaweza kutumika kutengenezea mafuta ya nywele
(shampoo)
- Manyoya yake yanaweza kutumika kama mapambo.
Fuga kuku upate faida kwa kuzingatia:
Chanjo ya mdondo kila baada ya miezi mitatu na chanjo ya ndui mara mbili
kwa mwaka
Zuia viroboto, utitiri na minyoo.
Chagua mayai bora kwa ajili ya kuatamiza
Panga kuuza kuku kwa makundi uongeze kipato
Kula mayai na kuku kadri uzalishaji unavyoongezeka.
Kipato unachokipata utenge pia na kiasi kwa ajili ya uendelezaji wa kuku
C:MAPUNGUFU
Yako mapungufu mengi yanayofahamika lakini hapa naomba niweke lile la
muhimu zaidi. MAGONJWA kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku
kutokana na kutokuzingatia kuchanja kuku kwa wakati.
D: KABILA ZA KUKU WA KIENYEJI
Kuna maelezo ya kusisimua sana kuhusu makabila ya kuku wa kienyeji, hata
hivyo kuna ugumu kidogo kuweza kuyachanganua makabila hayo kutokana na
muingiliano mkubwa wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Hata
hivyo kuku hawa wana tofauti za kimaumbile zinazosaidia kwa kiasi fulani
kutambua uwepo wa baadhi ya makabila ya kuku. Kabila hizi pia zinahusishwa
kwa kiasi kikubwa na eneo kuku wanakotoka. Baadhi ya kuku wa kienyeji
wanaweza kutambuliwa kwa maumbile yao Mfano:
a. Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni
b. Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale wenye manyoya yaliyosimama.
c. Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi kichwani.
d. Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani
Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha kuku kuwa na aina ya maumbile
mchanganyiko. Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na alama ya kishingo,
Njachama, Kibwenzi au Kibutu.
Hivyo kabila za kuku zifuatazo zinaweza kutambuliwa kama ndiyo kabila za
kuku wa kienyeji kulingana na maumbile yao na maeneo wanakotoka.
(i) KUCHI
Ni kuku warefu kwa umbo na wenye kusimama mgongo ukiwa wima. Wana manyoya
machache mwilinini na hasa kifuani, vilemba vyao ni vidogo. Majogoo huwa na
wastani wa uzito wa Kg. 2.5 na mitetea kg 1.5 mayai ya kuchi yana uzito wa
wastani wa gm 45. Kuku hawa hupatikana kwa wingi maeneo ya Mwanza,
Shinyanga, Tabora na Zanzibar.
(ii) CHING'WEKWE
Kuku hawa ambao jina lao ni gumu kidogo kwa mtu asiyekuwa na meno kulitamka
wana sifa zifuatazo.
Majogoo wana wastani wa kg 1.6, Mitetea wastani kg 1.2, mayai wastani wa gm
37. Kuku hawa wenye umbo dogo hupatikana zaidi maeneo ya CHAKWALE mkoani
Morogoro na pia sehemu za umasaini. Kuku hawa hutaga mayai mengi sana
kuliko aina nyingine ya kuku wa kienyeji waliopo Tanzania, kwa hiyo wanafaa
sana kwa biashara ya mayai.
(iii)UMBO LA KATI
Majogoo wana uzito wa wastani wa kg. 1.9, Mitetea kg. 1.1, Kuku hawa ndio
hasa wanaoitwa wa kienyeji(wa kawaida) Wana rangi tofauti. Utafiti
umeonyesha kuwa kuku hawa hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya
kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa mdondo (Castle desease)
Muhimu - Mfugaji akifanya uchaguzi kutoka kwenye aina hii ya kuku na kutoa
matunzo mazuri kwa hao kuku waliochaguliwa, Hakika anaweza kupata kuku
walio bora na wenye uzito wa kutosha pia kutaga mayai mengi na makubwa.
(iv) SINGAMAGAZI
Ni aina ya kuku wakubwa wa kienyeji wanaopatikana zaidi TABORA, kuku hawa
wana utambulisho maalum kutokana na rangi zao. Majogoo huwa na rangi ya
moto na mitetea huwa na rangi ya nyuki. Uzito - Majogoo uzito wa wastani wa
kg 2.9, mitetea wastani wa kilo 2 mayai gramu 56.
(iiv) MBEYA
Kuku hawa wanapatikana Ileje mkoani mbeya. Asili hasa ya kuku hawa ni
kutoka nchi ya jirani ya Malawi na si wa kienyeji asilia bali wana damu ya
kuku wa Kizungu "Black Australop". Majogoo Kg 3 mitetea kg 2 mayai gram 49
(iiiv)PEMBA
Hupatikana zaidi Pemba. Majogoo Kg.1.5 Mitetea Kg 1 mayai wastani gm 42
(xi) UNGUJA.
Majogoo Kg 1.6,mitetea kg 1.2 mayai gm 42. Kuku hawa wa Unguja na Pemba
wanashabihiana sana na Kuchi isipokuwa hawa ni wadogo.
SEHEMU YA PILI
1. MIFUMO YA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI.
A. MFUMO HURIA
Katika mfumo huu kuku huachiwa wakitembea toka asubuhi wakijitafutia
chakula na maji na kufungiwa kwenye vibanda visivyo rasmi wakati wa usiku.
Huu ni mfumo rahisi lakini si nzuri kwa mfugaji wa kuku wengi kwani
atahitaji eneo kubwa la ardhi.
FAIDA.
Mfumo huu una faida za gharama ndogo za uendeshaji kiujumla.
HASARA
Uwezekano mkubwa wa kuku kuliwa na vicheche, kuibiwa mitaani n.k
Kuku huweza kutaga popote na kusababisha upotevu mkubwa wa mayai.
Ni rahisi kuku kuambukizwa magonjwa
Utagaji unakuwa si nzuri kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Uwekaji kumbukumbu si nzuri.
Ni vigumu kugundua kuku wagonjwa hivyo kusababisha ugumu katika utoaji wa
tiba.
UTUMIAJI NZURI WA MFUMO HUU
Kuku wajengewe banda kwa ajili ya kulala nyakati za usiku na liwasaidie
wakati mwingine wowote hali ya hewa inapokuwa si nzuri.
Kuku wapatiwe chakula cha ziada na maji.
Kuku waandaliwe kwa viota vya kutagia.
Kuku 100 ni vizuri wakitumia eneo la ardhi la ekari 1.
B.MFUMO NUSU HURIA
Huu ni mfumo ambao kuku hujengewa banda rasmi na banda hilo huzungushiwa
uzio/ wigo. Mfumo huu ni ghari kiasi ukilinganisha na mfumo huria lakini
huweza kumpatia mfugaji faida haraka sana.
FAIDA
Sehemu ndogo ya kufugia hutumika kuliko ufugaji huria, utunzaji wa kuku ni
rahisi ukilinganisha na mfumo huria, Ni rahisi kutibu magonjwa ya mlipuka
kama mdondo (Newcastle desease), Upotevu wa kuku na mayai ni mdogo sana
ukilinganisha na mfumo huria.
C. MFUMO WA NDANI
Kuku hujengewa banda rasmi na hufugwa wakiwa ndani. Mfumo huu kuku huwekwa
kwenye mabanda ambayo sakafu hufunikwa kwa matandiko ya makapi ya mpunga,
takataka za mbao(randa), maganda ya karanga au majani makavu yaliyokatwa
katwa.
FAIDA
Mfumo huu unahitaji eneo dogo la kufugia, uangalizi mzuri na rahisi wa
kuku, Joto litokanalo na matandiko lina uwezo wa kuua vimelea vya maradhi,
kuku wanakingwa na hali ya hewa mbaya na maadui wengine.
HASARA
Uwezekano wa kuku kudonoana ni mkubw na pia Gharama za ujenzi wa mabanda
UTUMIAJI MZURI WA MFUMO HUU.
1. Matandiko yageuzwe kila siku
2. Kila mara matandiko yawe makavu kwa kuwa na madirisha yanayopitisha hewa
ya kutosha, ambayo yatatoa unyevunyevu hewa chafu ikiwemo ammonia.
4. Mita mraba moja hutosha kuku 5 hadi 8.
UTATUZI WA KUKABILIANA NA VIKWAZO KATIKA UFUGAJI.
Mambo ya kuzingatia:
Mabanda bora - Fuatilia kwa wataalamu wa mifugo walio karibu nawe.
Sifa za banda bora (Waone wataalam wa mifugo)
Kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi
Kuwa makini na aina ya mitetea na majogoo unatakiwa kuchagua ili kuwa na
kizazi bora.
UTAGAJI WA MAYAI
Kwa kawaida kuku huanza kutetea(Kutoa mlio wa ishara ya kutaga)
anapofikisha miezi sita hadi minane. Hivyo ni vyema viota viandaliwe mapema
wakiwa na umri wa miezi mitano. Kuku anapoanza kutaga akifikisha mayai
matatu mfugaji anashauriwa kuondoa kila yai linalozidi hayo matatu kila
siku linapotagwa na kuliweka alama ya tarehe au namba kwa kutumia penseli
ili kumfanya kuku aendelee kutaga kwa lengo la kufikisha mayai 15 mpaka 20.
Mayai yanayoondolewa yawekwe kwenye chombo kikavu kinachopitisha hewa ni
vizuri pia kuweka mchanga ndani ya chombo hicho.
Hakikisha ya fuatayo.
Sehemu iliyochongoka iwe chini na pana iwe juu.
Hifadhi sehemu yenye hewa ya kutosha na isiyohifadhi joto
Mayai yasikae kwenye hifadhi hiyo zaidi ya wiki mbili toka siku ya kuanza
kutagwa.
UATAMIAJI WA MAYAI NA UANGUAJI WA VIFARANGA
Uatamiaji na uanguaji wa kubuni - Mfumo huu hutumia mashine za kutotoleshea
vifaranga (Incubators) hutumika kuangua mayai mengi kati ya 50 hadi 500 kwa
wakati mmoja Mashine zinazotumika kutotoleshea vifaranga wa kisasa zinaweza
kutumika pia kutotoleshea wa kienyeji.
Uatamiaji na uanguaji wa asili
KUCHAGUA MAYAI YA KUANGUA.
Hili nalo ni muhimu kuzingatia. Ni vizuri kuchagua mayai ya kuatamia ili
mayai yasiyofaa yaweze kuuzwa au kutumiwa nyumbani kwa chakula. Mayai ya
kuatamia yawe na sifa zifuatazo
Yasiwe na uchafu yawe masafi
Yasiwe na nyufa
Yatokane na kuku aliyepandwa na jogoo
Yasiwe madogo wala makubwa bali yawe na ukubwa wa wastani kulingana na
umbile la kuku.
Yasiwe mviringo kama mpira pia yasiwe na ncha kali sana.
Yasiwe yamekaa muda mrefu zaidi ya wiki mbili toka yalipotagwa
Yasiwe yaliyohifadhiwa kwenye sehemu yenye joto.
KUMTAYARISHA KUKU WA KUATAMIA
Pamoja na matayarisho hayo zingatia kumuwekea mayai yasiyozidi 15 pia ni
vizuri yasipungue 12. Kuku wanaotazamiwa kuatamia ni lazima wachunguzwe kwa
makini kabla ya kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana chawa, utitiri n.k.
Kuwepo kwa wadudu hao huwafanya kuku wakose raha na kutotulia kwenye viota
vyao. Hali hii husababisha kuanguliwa kwa Vifaranga wachache.
Sasa unatakiwa kufanya yafuatayo:-
Nyunyiza dawa ya kuua wadudu ndani ya kiota
Pia mnyunyuzie dawa kuku anayetarajia kuatamia
Weka mayai kwenye kiota huku mikono yako ikiwa imepakwa jivu ili kuepuka
kuwa na harufu kwani kuku anaweza kuyasusa.
Ni vizuri kuifanya kazi hii ya kumuandaa kuku anayetaka kuatamia wakati wa
usiku. Pia ifahamike kuwa kwa kawaida kuku huatamia mayai yake siku 21.
PIA JIFUNZE MBINU ZA KUATAMIA MAYAI MENGI KWA NJIA ZA ASILI
Iwapo una kuku wengi wanaotaga kwa wakati mmoja ni vema ukawafanya
wakaatamia na kutotoa pamoja.
Unachotakiwa kufanya ni kuchagua mayai ya kuatamia ukianzia na yai la
mwisho kutaga.
Unaweza kuwaandaa kuku wako zaidi ya mmoja ili waanze kuatamia kwa pamoja
na kupata vifaranga vingi kwa mara moja kuku wa kwanza anapoanza kuatamia.
Mwekee mayai viza au ya kuku wa kisasa kwani kuku huatamia hadi mayai
yanapoanguliwa hivyo ukimuwekea mayai yasiyo na mbegu atakaa hapo muda
mrefu hadi vifaranga watoke.
UTEKELEZAJI WAKE
Kuku anapotaga kila siku weka alama ya namba au tarehe kulinganisha na siku
anayotaga
Yanapofika mayai matatu yaondoe na muwekee mayai viza au ya kisasa huku
ukiendelea kuweka alama mayai yanayotagwa kila siku.
Mara kuku anapoanza kuatamia muongezee mayai ya uongo yafikie 8 hadi 10
Fanya hivyo kwa kila kuku anayetaga hadi utakapoweza kupata idadi
itakayoweza kukupatia vifaranga wengi kwa wakati mmoja.
Wawekee kuku wote mayai siku moja kwa kuondoa mayai ya uongo na kuwawekea
mayai ya ukweli wakati wa usiku.
MUHIMU
Mayai ya kuatamia yasishikwe kwa mkono ulio wazi na wala yasipate harufu za
mafuta ya taa, manukato n.k.
JIFUNZE PIA KUTAMBUA MAYAI YALIYO NA MBEGU NA YALE YASUYO NA MBEGU.
Mfugaji anaweza kutambua mayai yaliyo na mbegu na yale yasiyo na mbegu siku
ya saba baada ya kuanza kuatamia iwapo atapima mayai kwa kutumia box
lililotengenezwa maalum pamoja na tochi yenye mwanga mkali ndani ya chumba
chenye kiza. Hii itamuwezesha mfugaji ayatumie mayai yasiyo na mbegu kwa
chakula cha familia au kuyauza.
TAMBUA VYAKULA NA UZALISHAJI WA KUKU - Sitalielezea hili naomba ufuatilie
mwenyewe.
JIFUNZE MBINU ZA KUZALISHA KUKU WENGI KWA MUDA MFUPI
Zoezi hili linawezekana iwapo uleaji wa vifaranga kwa njia ya kubuni
utatumika. Kuku mmoja anaweza kutotoa zaidi ya mara saba kwa mwaka.
Taz.
Hesabu ya uzalishaji wa kuku wengi kwa mwaka kwa kutumia mtetea mmoja tu.
Mpaka mwisho wa mwaka unaweza kuwa na idadi ya vifaranga 252 kwa kadirio la
vifaranga 8 kila mzao. Hivyo kama una kuku 10 wanaotunzwa vizuri utakuwa
umezalisha jumla ya vifaranga 2520.
Fuatilia kwa wataalamu wa mifugo ili ufundishwe zaidi kuhusu mbinu hiyo ya
kuzalisha kuku wengi.
ULEAJI WA VIFARANGA
NJIA YA KUBUNI
NJIA YA ASILI
Njia zote mbili zinafahamika kama huzifahamu tafadhali fuatilia kwa
mtaalamu aliye karibu nawe.
MAGONJWA NA WADUDU WANAOSHAMBULIA KUKU WA KIENYEJI NA JINSI YA KUKINGA.
A. MAGONJWA.
Ugonjwa hatari - Mdondo/ Kideri (Newcastle desease) Hapo nyuma dawa ya
kukinga ugonjwa huu ilikuwepo lakini ilikuwa inahitaji kuhifadhiwa kwenye
hali ya ubaridi (Friji) Hali hiyo ilisababisha iwe ngumu kutumika vijijini
kwa dawa hiyo. Hivi sasa kumepatikana chanjoa ambayo inastahimili joto
ambayo inaweza kutumika hata vijijini.
Pamoja na mdondo yapo pia magonjwa yanayoshambulia kuku hapa nchini
Ndui ya kuku(Fowl pox)
Mafua ya kuku(Infectious coryza)
Homa ya matumbo (Cocciodiosis)
Minyoo na wadudu kama viroboto, chawa, utitiri na kupe wa kuku.
DALILI ZA KUKU MGONJWA.
Huzubaa
Hali chakula/maji vizuri
Hujitenga na wenzake
Hujikunyata au kuinama
Hutetemeka
Hutembea kwa shida
Utagaji wa mayai hupungua au hukoma kabisa
MAGONJWA YA KUKU HUSABABISHWA NA NINI?
Yako mambo mengi yanayosababisha lakini matunzo hafifu pia huchangia.
ATHARI ZA MAGONJWA.
Hili liko wazi
Maelezo haya ya magonjwa ni mengi hivyo tuwe wafuatiliaji kwa wataalam.
MATIBABU
KIDERI - Sifahamu tiba ya kitaalam ya ugonjwa huu kama kuna ambaye
anafahamu tunaomba atufahamishe lakini ziko dawa za asili na za kitaalam
ambazo zinafaa zaidi kwa chanjo.
Ugonjwa huu unaweza kuukinga kwa kuwapa kuku chanjo ya Mdondo. Pia
usichanganye kuku wako na kuku ambao huna taarifa zao za chanjo.
KUMBUKA
Mdondo au kideri ni ugonjwa tishio ambao huweza kuua kuku wote
Mdondo ukitokea vifo huwa vingi pia kuku hupumua kwa taabu, hupooza na
wengine huzunguka na huzungusha vichwa.
Mdondo unaweza kuzuilika kwa chanjo kila baada ya miezi 3
NDUI YA KUKU
HOMA YA MATUMBO (Fowly typhoid)
MAFUA YA KUKU(Infectious coryzya)
KUHARISHA DAMU(Coccidiosis)
Minyoo na wadudu wanaoshambulia kuku kama viroboto n.k
Kwa magonjwa na wadudu tuliowataja hapo juu please wasiliana na mtaalamu wa
mifugo aliye karibu nawe Kwani siwezi kueleza kila kitu hapa wataalamu
tunao naamini watatusaidia.
TIBA ZA ASILI
Kuna madawa ya asili ambayo hutokana na mimea ambayo hukinga kuku.
BAADHI YA MIMEA INAYOTIBU NA KUKINGA MARADHI YA KUKU.
MWAROBAINI - Typhoid, kuhara, kideri, kifua na vidonda
ALOEVERA - Typhoid, kuhara, kideri, kifua na vidonda,ngozi na Cholera.
Tutaelekezana zaidi namna ya kuandaa dawa hii.
Hapa nataka niorodheshe baadhi ya madawa ya asili ambayo yanasaidia kutibu
na kukinga kuku.
Mwarobaini, Aloevera, Mtakalang'onyo(Euphorbia),Mbar ika, mlonge,
Ndulele/dungurusi/tura/ndura, Majani ya mpapai, Mwembe, Minyaa na Pilipili
kichaa.
NAWASHUKURU PIA NAOMBA MWENYE MCHANGO ZAIDI AENDELEE KUONGEZEA TUSIWE
WACHOYO WA MAARIFA KIDOGO GAWANA NA MWENZIO
Chanzo:
jamiiforums.com: Last edited by GAZETI; 4th December 2011 at 18:04.
--
'Walk The Talk'
Frederick M. Katulanda
Cell:
+255 784 642620,
Alternative:
+255 754 642620
E-mail:
fkatu...@yahoo.com
--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la ‘Mabadiliko’.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii:
mabadilik...@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda;
mabadilikotanza...@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
This years motto: ‘WALK THE TALK’
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
--
"For hope is but the DREAM of those that wake"
LOVE, HOPE AND FAITH!