TAARIFA YA DKT. REGINALD A. MENGI MWENYEKITI MTENDAJI WA IPP LIMITED KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 20 DESEMBA 2013
Baada ya Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara ((TNBC) uliofanyika
tarehe 16 Desemba 2013, chini ya uenyekiti wa Mhe. Rais, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza hilo, sikutegemea kwamba Mhe. Profesa Muhongo
angeendeleza mashambulizi dhidi yangu kwa sababu katika mkutano huo
ambao ulikuwa na mafanikio makubwa tulifikia maamuzi ya kudumisha
ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi, kitu ambacho nimekuwa
nikipigania. Hivyo basi, kauli ambazo Mhe. Profesa Muhongo amezitoa
Bungeni tarehe 19 Desemba 2013, zimenishtua na kunisikitisha sana.
Ningependa kuwaeleza Watanzania wenzangu yafuatayo.
Profesa Muhongo ni muongo
Imefika wakati wa Watanzania kubaini kwamba Mhe. Profesa Muhongo ni mtu mwenye hulka ya kusema uongo. Kwa mfano:
1. Kwenye kongamano la tarehe 8 Desemba 2013, Mhe. Profesa Muhongo
alisema kwamba moja ya kazi yake, alipokuwa akifanya kazi kama
mwanasayansi huko nje, ilikuwa kutabiri umuhimu wa sayansi katika uchumi
wa dunia miaka 3,000 ijayo. Huu ni uongo wa mchana kweupe.
2. Mnamo Julai 2012 Mhe. Profesa Muhongo aliwaahidi Watanzania
kwamba hakutakuwa na mgawo wa umeme tena. Sote tunashuhudia mgao wa
umeme ukiendelea hadi sasa.
3. Mnamo mwezi Septemba 2012, Mhe. Profesa Muhongo alinukuliwa
akizungumzia mikataba ianayohusiana na vitalu vya gesi akisema kwamba
“baadhi ya mikataba ni ya ovyo, na inahitaji kuvunjwa” na “sitovumilia
mikataba ambayo haina maslahi kwa nchi na inawanufaisha wachache”. Baada
ya hapo, Mhe. Profesa Muhongo aliamrisha Bodi mpya ya TPDC kusitisha
ugawaji wa vitalu vya gesi uliopangwa kufanyika mwezi huo na kupitia
upya mikataba yote iliyokuwepo awali. Sasa zaidi ya mwaka umepita na
Mhe. Profesa Muhongo hajarekebisha mkataba hata mmoja.
Profesa Muhongo na takwimu zake za maeneo ya madini
1. Tarehe 8 Desemba 2013, alipokuwa anajibu swali la Mhe. Tundu
Lissu kuhusu ni nani anamiliki migodi ya Tanzania, Profesa Muhongo
alitoa takwimu za kuonyesha kwamba mimi ninamiliki eneo kubwa mara tatu
ya Dar es Salaam kupitia kampuni zangu tanzu.
2. Jumapili iliyopita mimi nilimjibu Mhe. Profesa Muhongo kwa
kumueleza kwamba takwimu zake kuhusu mimi ni za uongo, na vilevile hizo
alizotoa Bungeni pia ni za uongo na nilimweleza kwamba swali la Mhe.
Tundu Lissu lilikuwa ni “nani anamiliki maeneo ya migodi”.
3. Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa utafutaji madini (mineral
prospecting) ndiyo msingi wa maendeleo ya sekta ya madini kwa sababu
bila utafutaji hakuna ugunduzi na uendelezaji wa migodi hapa nchini.
Lakini kuanzia Julai mwaka jana Waziri Muhongo alipandisha tozo za
vitalu kwa asilimia kati ya 100 na 500. Matokeo yake Watanzania wengi
wanarudisha leseni zao na kasi ya ugunduzi wa migodi imepungua.
4. Nia ya mtu inajionyesha siyo tu kwa yale anayosema lakini bali
pia kwa yale anayoacha kusema. Sasa kama kweli nia ya Mhe. Profesa
Muhongo ni nzuri, kwa nini hatoi takwimu zinazohusu gesi? Kwa mfano, kwa
nini hawaambii Watanzania kwamba:
a. Eneo ambalo limeshatolewa
kwa ajili ya mafuta na gesi lina ukubwa wa kilomita za mraba 243,000
ambalo ni sawa na karibu robo ya eneo la Tanzania nzima au mara 175 ya
eneo la mkoa wa Dar es Salaam au eneo la mikoa 9 ya Dar es Salaam,
Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Shinyanga na Kagera.
b. Kwa nini Mhe. Profesa Muhongo hataki kuwaambia Watanzania kwamba
hakuna hata mzawa mmoja anayemiliki kitalu cha kutafuta au kuchimba
mafuta na gesi?
c. Kwa nini Mhe Profesa Muhongo hataki kuweka wazi kwamba vitalu
vyote 27 vya gesi ambavyo vinaanzia katika mpaka wetu na Kenya hadi
mpaka wetu na Msumbiji, vimegawiwa kwa wageni? Je, kugawa vitalu vyote
vya gesi kwa wageni siyo hatari kwa mustakabali wa usalama wa taifa
letu?
d. Lakini cha muhimu ni kwamba Watanzania wafahamu kwamba gesi
ambayo imeshagunduliwa Tanzania inakadiriwa kuwa na thamani ya US$ 500
bilioni wakati dhahabu yote iliyokwishagunduliwa hadi sasa na bado
haijachimbwa inakadiriwa kuwa na thamani ya US$ 60 bilioni kwa bei ya
sasa ya dhahabu.
Kwanini Profesa Muhongo hawaambii Watanzania takwimu hizi?
Profesa Muhongo na kauli zake kwamba Watanzania hawawezi kushiriki katika mchakato wa mafuta na gesi
1. Mara nyingi tumesikia kauli za Mhe. Profesa Muhongo kwamba
Watanzania hatuwezi kufanya biashara ya mafuta na gesi kwa sababu
biashara hiyo inahitaji mtaji mkubwa na utaalamu, vitu ambavyo
Watanzania hawana. Mhe. Profesa Muhongo amewahi kusema kwamba Watanzania
ni wavivu wa kufikiri, wavivu wa kusoma na washamba sana katika masuala
ya uwekezaji na kwamba uwezo walionao Watanzania ni kuuza juisi au
soda. Huu ni uongo. Watanzania wanajua wanachokisema na gesi yetu ni
mtaji mkubwa sana.
2. Kwanza kabisa katika karne ya 21 utalaamu ni bidhaa ambayo mtu
asiye nayo anaweza kuinunua. Mhe. Profesa Muhongo anaweza asilifahamu
hili kwa sababu yeye mwenyewe hajawahi kufanya biashara katika maisha
yake – anayasoma masuala ya biashara kwenye makaratasi tu.
3. Namsihi Mhe. Profesa Muhongo akumbuke kwamba gesi ni mali ya
Watanzania na wana haki ya kuzaliwa ya kumiliki rasilimali yao ya gesi.
4. Mhe. Profesa Muhongo anataka Watanzania waamini kwamba kuna
mwekezaji wa nje anaweza kumiliki na kuendesha kitalu kwa fedha zake
yeye mwenyewe. Hii si kweli. Fedha zinazotumika ni za watu wengi
waliowekeza katika masoko ya hisa. Sisi pia tungehamasishwa na
kuwezeshwa, tunaweza kuunganisha nguvu zetu hivyo hivyo na kuwekeza
katika gesi yetu kwa kushirikiana na wageni. Mimi sipingi uwekezaji wa
wageni. Watanzania nao washirikishwe katika umilikaji. Mgeni aje
mwenyeji apone, siyo mgeni aje mwenyeji akose fursa ya kushiriki katika
umiliki wa uchumi wake.
Profesa Muhongo hana nia nzuri kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania katika gesi ?
1. Katika kongamano lilofanyika tarehe 8 Desemba 2013 Mhe. Profesa
Muhongo alisema Watanzania wenye uwezo wa kifedha wazipeleke TPDC tarehe
10 Desemba 2013 na watapewa vitalu vya gesi. Vilevile alisema kwamba
baada ya tarehe hiyo, hoja ya suala la wazawa kumiliki vitalu
litafungwa. Watu waliokuwepo kwenye hilo kongamano walipigwa butwaa kwa
sababu Profesa Muhongo alishanukuliwa akisema kwamba kwenye uongozi wake
wazawa hawatapewa vitalu vya gesi na kwamba “suala la vitalu halina
mambo ya uzawa”.
2. Kwa kuzingatia kwamba maagizo ya Mhe. Profesa Muhongo yalikuwa ni
batilii (huwezi kutangaza zabuni kwenye kongamano) wafanyabiashara wa
Tanzania walimpuuza na hakuna hata mmoja aliyejitokeza. Lakini kikubwa
zaidi ni kwamba haya mazingaombwe ya Mhe. Profesa Muhongo yalitufumbua
macho Watanzania kung’amua kwamba kumbe kazi ya TPDC ni kupokea maagizo
tu na anayegawa vitalu vya gesi ni Profesa Muhongo mwenyewe.
3. Nimekuwa nikirudia mara kwa mara kwamba mtaji sio tu fedha hata rasilimali kama gesi ni mtaji.
Hitimisho
1. Ningependa kutofautiana na Mhe. Profesa Muhongo na kusema kwamba
adui wa maendeleo ya Watanzania siyo Watanzania wenyewe kama alivyosema
ila ni Watanzania wachache sana wenye kauli za dharau za kutuambia
kwamba Watanzania hatuwezi.
2. Katika suala la gesi mimi sipiganii mambo yangu binafsi, kwa
sababu mimi nimeshafanikiwa kibiashara. Ninachopigania ni Watanzania
wenzangu nao wapate fursa. Naomba nieleweke kwamba ninaposema Watanzania
nina maana kuanzia yule mfanyabiashara mdogo wa sekta isyo rasmi,
mfanyabiashara wa kati na wafanyabiashara wakubwa. Nataka kuwepo sera
ambayo itahakikisha kwamba wanawezeshwa na siyo kusema tu kwamba
hawawezi. Nafanya hivyo kwa sababu ninaamini kwamba utajiri uliobarikiwa
ni ule uliopatikana kwa njia halali na unatumika kusaidia wanaohitaji
msaada.
3. Ni wazi kwamba Mhe. Profesa Muhongo anachuki binafsi na mimi. Hii
ni utashi wake, siyo lazima anipende na mimi siyo lazima nimpende.
Lakini suala la gesi ni kubwa mno kuliko mahusiano kati ya Mhe. Profesa
Muhongo na mimi – linagusa kila Mtanzania wa leo na wa vizazi vijavyo.
Kwahiyo napenda kumsihi ndugu yangu Mhe. Profesa Muhongo aache
kuchanganya chuki zake binafsi kwenye suala la gesi.
Dr. Reginald Mengi
Dar es Salaam
Disemba 20, 2013
________________________________________________________________________
Eliaza Mmbaga (ELLY),
Bachelor In Tourism Management, Diploma in Tourism & Travel Agency Mgmt and Licensed Mt Tour Guide,
Expedition Tour Guide/Leader & Tour Organizer at Milimani Adventure & Safaris East Africa,
P. O. Box 14510,
ARUSHA - TANZANIA.
EAST - AFRICA.
Skype:
elly.mmbaga
Proud Member Of:
Tanzania Association of Tour Operators (TATO)
Working hours:
Mon through Friday: 08:30hrs - 17:00hrs
Saturday: 09:00hrs - 12:30hrs
EAST AFRICAN TIME: GMT + 3
...................................................
Conserve Nature and Culture!!
--------------------------------------