MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA
SHERIA,
MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, 2011
(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu
za Bunge, 2007)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 11 Machi 2011, Serikali ilichapisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika Gazeti la Serikali la tarehe hiyo.
Muswada huo ulipelekwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
kwa Hati ya Dharura. Hata hivyo, baada ya upinzani mkubwa dhidi ya Muswada huo
kujitokeza karibu nchi nzima, Bunge lililazimika kuondoa Hati ya Dharura na
hivyo kufanya Muswada kushughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida wa
kutunga sheria uliowekwa na kanuni za 80, 83 na 84 za Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano, 2007. Katika
kufanya hivyo, Bunge – kwa kupitia Spika - liliiagiza Serikali kufanya mambo
yafuatayo kwa mujibu wa Taarifa
Rasmi ya Majadiliano Katika Bunge (Hansard) ya Kikao cha Nane cha Mkutano wa
Tatu cha tarehe 15 Aprili 2011:
(a) “Muda zaidi utolewe kwa Kamati na wananchi
kuufikiria Muswada huu. Katika kufanikisha hili, “... iandae Muswada huu kwa
lugha ya Kiswahili ili wananchi wenyewe waweze kusoma yaliyomo kwenye Muswada
huo badala ya kupewa tafsiri tu na watu wengine;
(b) “Muswada uchapishwe kwenye magazeti na
kutangazwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari ili kutoa fursa ya kutosha kwa
wananchi wengi kuuelewa na kuutolea maoni;
(c) “Utangulizi wa Muswada huu uwekwe vizuri zaidi ili wananchi waelewe
madhumuni ya Muswada huu, kwani imeonekana wazi wananchi wengi wanadhani tayari
tumeanza kuandika Katiba, kumbe lengo la Muswada huu ni kutunga Sheria ya
Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni tu.” (uk. 31-32)
Mheshimiwa Spika,
Katika kutoa maagizo haya, Bunge lilisitiza kwamba “... Muswada huu uko ndani
ya Bunge, hauko serikalini.” (uk. 33) Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa kanuni
ya 84(1) ya Kanuni za Bunge, Muswada ulikwishasomwa kwa mara ya kwanza na
kupelekwa kwenye Kamati inayohusika kwa ajili ya kuanza kujadiliwa. Aidha, kwa
mujibu wa kanuni ya 84(2) Kamati ilikwishaanza kupokea maoni ya wadau “... kwa
lengo la kuisaidia katika uchambuzi wa Muswada huo.” Kazi iliyokuwa imebaki kwa
Kamati ilikuwa ni kutumia mamlaka yake chini ya kanuni ya 84(3) “... kufanya marekebisho
katika Muswada wa Sheria kwa kumshauri Waziri ... anayehusika na Muswada huo
kufanya mabadiliko....” Ni baada tu ya kupata ushauri wa Kamati kuhusu
mabadiliko ndio Serikali ingeweza kuleta Jedwali la Mabadiliko kwa lengo la
kufanya mabadiliko katika hatua hii kabla Muswada haujaletwa Bungeni kwa ajili
ya kusomwa mara ya pili na kwa mjadala wa Bunge zima.
Mheshimiwa Spika,
Hakuna hata moja ya maagizo haya ya Bunge ambalo limetekelezwa na Serikali.
Tafsiri ya Kiswahili ambayo imeletwa Bungeni – pamoja na kuonyesha imesainiwa
tarehe 8 Machi 2011 sawa na Muswada wa Zamani uliopigiwa kelele sana na
wananchi – ililetwa kwenye Kamati wiki mbili zilizopita, ikiwa ni wiki moja
baada ya Kamati kukataa kuujadili Muswada Mpya kwa vile ulifanyiwa mabadiliko
na Serikali bila kupata ushauri wa Kamati kama inavyotakiwa na kanuni ya 83(4)
ya Kanuni za Bunge. Badala ya kutekeleza maagizo ya Bunge, Serikali
imeleta Muswada wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ambao ulichapishwa katika Gazeti la
Serikali la tarehe 14 Oktoba 2011.
Muswada huu mpya una tofauti kubwa na za kimsingi na Muswada wa Zamani kama
nitakavyoonyesha hapa. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mabadiliko
makubwa na ya kimsingi yaliyofanywa kwenye Muswada wa Zamani yalihitaji na bado
yanahitaji mjadala wa kitaifa wa wananchi kama ambavyo wengi wamedai katika
mijadala inayoendelea nchi nzima. Aidha, Bunge hili tukufu lilihitaji, na bado
linahitaji, muda zaidi wa kuyatafakari mabadiliko haya makubwa na ya kimsingi
katika Muswada wa Zamani. Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaamini ni busara na ni sound
policy kwa Muswada huu Mpya kusomwa mara ya Kwanza ili kuruhusu
mjadala unaohitajika kufanyika.
TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, Muswada huu unapendekeza kuundwa kwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa mujibu wa Utangulizi wa Muswada,
itawajibika “... kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba (na)
kuainisha na kuchambua maoni ya wananchi....” Kwa mujibu wa ibara ya 5, Tume
hii itaundwa na Rais “kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na
kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar....” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 6(1), Rais
atateua wajumbe wa Tume “... kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa
Zanzibar....”
Ibara ya 6(2) inapendekeza kwamba “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa
kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Pendekezo
hili linarudia, kwa njia iliyojificha zaidi, msimamo wa ibara ya 6(2) ya
Muswada wa Zamani iliyokuwa imeweka wazi kwamba idadi ya wajumbe wa Tume
itakuwa sawa kwa sawa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano! Kama ilivyokuwa
kwa Muswada wa Zamani, ibara ya 7(2) ya Muswada inapendekeza kwamba “uteuzi wa
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti utafanyika kwa msingi kwamba iwapo Mwenyekiti
atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Makamu Mwenyekiti atakuwa mtu
anayetoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.”
Muundo wa Tume unakamilishwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na Katibu.
(ibara ya 13(1) Kwa mujibu wa ibara ya 13(2), Katibu huyo atateuliwa na Rais
“baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar.” Watendaji wengine wa Sekretarieti
watateuliwa na Waziri “kwa makubaliano na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya
Katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”
Muswada unapendekeza kumpa Rais - baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar -
mamlaka ya kutoa hadidu za rejea za Tume na muda wa kukamilisha na kuwasilisha
ripoti. (ibara ya 8(1) Na kama hali itahitaji kufanya hivyo, Rais – “kwa
makubaliano na Rais wa Zanzibar” – anaweza kuongeza muda usiozidi miezi mitatu
ili kuwezesha Tume kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(2) Hadidu za
rejea, kwa mujibu wa ibara ya 8(3), “... zitakuwa ni hati ya kisheria ambayo
Tume itaizingatia katika utekelezaji wa majukumu na utumiaji wa mamlaka yake
kwa mujibu wa Sheria hii.”
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 9(1) ya Muswada inaelezea kazi za Tume kuwa ni pamoja na:
(a) Kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi;
(b) Kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba
yanayohusu mamlaka ya watu, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na
utawala bora;
(c) Kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea; na
(d) Kuandaa na kuwasilisha ripoti.
Ijapokuwa haijaanishwa hivyo, ni wazi - kwa mujibu wa wa ibara ya 17(1)(d) na
(2) ya Muswada - kwamba moja ya kazi za Tume ni kuandaa Rasimu ya Muswada wa
Katiba mpya. Mapendekezo ya Muswada kuhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni
muhimu na yanazua maswali mengi yanayohitaji mjadala wa kitaifa na maamuzi ya
wananchi. Maeneo haya muhimu ni pamoja na nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
katika mchakato mzima wa kutengeneza Katiba Mpya.
MAMLAKA YA RAIS
Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge hili, kwa muda wote wa uhai wetu
kama taifa huru, mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa umejengwa juu ya nguzo
kuu ya Urais wa Kifalme (Imperial
Presidency). Hii inatokana na ukweli kwamba katika mfumo huu, Rais ana madaraka
makubwa sana ya kiutendaji na ya kiutungaji sheria. Vile vile Rais ana kivuli
kirefu cha kikatiba juu ya mahakama kwa kutumia mamlaka makubwa aliyonayo
katika uteuzi wa viongozi wote wa ngazi za juu za Mahakama. Urais wa Kifalme
ndio chanzo kikuu cha kukosekana kwa uwajibikaji katika ngazi zote za serikali
na ndio kichocheo kikubwa cha rushwa na ufisadi wa kutisha ambao umefanywa kuwa
ni sehemu ya kawaida ya maamuzi ya kiserikali. Sio vibaya, katika kuthibitisha
jambo hili, kurudia maneno ya ibara ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977: “... Rais atakuwa huru na hatalazimika
kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote....” Na kama alivyowahi kusema
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwenye mahojiano ya mwaka 1978 na Shirika la
Habari la Uingereza (BBC), kama Rais wa Tanzania alikuwa na mamlaka – kwa
mujibu wa Katiba na sheria za nchi yetu – ya kuwa dikteta!
Muswada unaendeleza kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika mchakato wa
upatikanaji wa Katiba Mpya. Mtu mwenye mamlaka ya kidikteta, kama Rais alivyo
kwa mujibu wa Katiba ya sasa, hawezi kusimamia upatikanaji wa katiba ya
kidemokrasia. Kwa kutumia mamlaka makubwa ya uteuzi wa Tume yanayopendekezwa na
Muswada huu, ni wazi Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha
CCM, atateua wajumbe anaowataka yeye na Rais Ali Mohamed Shein, Makamu wake na
pia Rais wa Zanzibar! Ni wazi vile vile kwamba watu watakaoteuliwa na Marais
hawa ni watu wasiokuwa tishio kwa status
quo kwa maana ya kupendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa
kikatiba na kiutawala na hivyo kuhatarisha maslahi ya CCM!
Mheshimiwa Spika,
Hali ni hiyo hiyo kwa Sekretarieti ya Tume ambayo ndio chombo cha kiutendaji na
moyo wa Tume yenyewe. Kama Katibu, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Tume ni
mteuliwa wa Rais na ni mtumishi wa Serikali; kama watendaji wengine wa Tume ni
watumishi wa serikali walioteuliwa wa Waziri ambaye naye ni mteuliwa wa Rais
baada ya kukubaliana na Waziri mwenzake wa Zanzibar; na kama watumishi wengine
wa Tume nao ni watumishi wa Serikali kama inavyopendekezwa na ibara ya 13 ya
Muswada Mpya, ni wazi, kwa hiyo, kwamba mapendekezo haya yote ya uteuzi wa
wajumbe, watendaji na watumishi wengine wa Tume yana lengo moja tu: kuhakikisha
kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na
Serikali yake na chama chake cha CCM.
Mheshimiwa Spika,
Badala ya mapendekezo haya ya Muswada Mpya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza utaratibu wa kidemokrasia zaidi katika uteuzi wa Tume. Kwanza,
badala ya Tume hiyo kuwa ‘Tume ya Rais’ kama inavyopendekezwa katika Muswada,
tunapendekeza iwe ‘Tume ya Vyama’ (multiparty
Commission) kwa maana moja kubwa: wajumbe wa Tume wateuliwe kufuatana na
mapendekezo na makubaliano ya vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni, vyama
vingine vilivyosajiliwa pamoja na mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na
za kidini. Hii haina maana kwamba wajumbe wa Tume hiyo hawatatakiwa kuwa na
sifa zilizoainishwa katika ibara ya 6(3) ya Muswada Mpya. La hasha! Wajumbe wa
Tume ya Vyama watatakiwa kuwa na sifa zozote za kitaaluma zinazotakiwa ili
kuwawezesha kufanya kazi ya kitaalamu kama inavyopendekezwa na Muswada
Mpya.
Pili, baada ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Vyama, inapendekezwa kwamba wajumbe
walioteuliwa kwa mashauriano na makubaliano kama tunavyopendekeza watatakiwa
wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Pendekezo hili litahakikisha
kwamba wajumbe wa Tume wanakuwa vetted na
chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi. Hili litajenga kuaminiana baina ya
Serikali, vyama vya siasa, mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za
kidini na litaipa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uhalali mkubwa wa kisiasa, kitu
ambacho ni muhimu katika mazingira ya sasa ya kisiasa.
Mheshimiwa Spika,
Tofauti pekee na muhimu kati ya pendekezo la Muswada Mpya na pendekezo letu
kuhusu mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ni locus ya uwajibikaji wao. Wajumbe wanaoteuliwa na Rais
wanakuwa na shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha Rais au chama chake.
Wajumbe wanaotokana na mapendekezo na makubaliano ya wadau wengi na wanaothibitishwa
na chombo cha uwakilishi cha wananchi kama tunavyopendekeza hawawezi kuwa na
shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha mmojawapo wa wadau hao. Faida
kubwa na ya wazi ya Tume ya Vyama ni kwamba matokeo ya kazi yake yana nafasi
kubwa zaidi ya kukubaliwa, kuheshimiwa na kutekelezwa na wadau mbali mbali
kuliko matokeo ya kazi ya Tume ya Rais. Kwa lugha nyingine, kazi ya Tume ya
Vyama itakuwa na uhalali wa kisiasa (political
legitimacy) mkubwa zaidi kuliko Tume ya Rais.
Pendekezo hili linawahusu Katibu, watendaji na watumishi wengine wa Tume vile
vile. Kutokana na uzoefu uliotokana na historia yetu na mfumo wetu wa kiutawala
na kikatiba, watumishi wa serikali wamekuwa hawana uhuru wa kufanya maamuzi kwa
kuzingatia utashi wao na uadilifu wa kitaaluma bali hufanya maamuzi kwa
kuzingatia matakwa ya mabosi wao wa kisiasa. Hii ni kwa sababu, kisheria na
hata kivitendo, watendaji na watumishi karibu wote wa umma hujiona wanawajibika
kwa mamlaka zao za uteuzi, yaani Rais na/au Waziri. Aidha, watendaji na
watumishi hawa wanawajibika kinidhamu kwa mamlaka zinazoongozwa na watendaji wa
Serikali ambao nao ni wateuliwa wa Rais na kwa hiyo wanakuwa na woga wa kufanya
maamuzi yanayoweza kuhatarisha maslahi ya kisiasa ya Rais na chama
tawala.
Kwa sababu hizo, ni muhimu kwa watendaji na watumishi wote wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba wawe huru dhidi ya mashinikizo yoyote ya kisiasa kutoka
kwa Rais na Serikali yake na chama chake. Ili Tume iwe na mamlaka na uhuru
unaohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake na ili isiingiliwe kweli
na mtu au mamlaka yoyote kama inavyosema ibara ya 10 ya Muswada, inabidi
mamlaka ya uteuzi yaondolewe katika mikono ya Rais na/au Waziri ambaye ni mdau
mmojawapo tu wa wadau wengi wa mchakato wa Katiba Mpya. Na namna ya pili ya
kuhakikisha uhuru huu unakuwepo ni kuweka utaratibu wa kuwapata watendaji na
watumishi hawa nje kabisa ya utumishi wa serikali kwa kuweka masharti ya
kuwataka waombe kazi, kufanyiwa usaili na kuteuliwa na jopo la wataalamu walio
huru.
Mheshimiwa Spika,
Namna ya tatu ya kuhakikisha uhuru wa Tume katika kutekeleza majukumu yake ni
kuhakikisha wajumbe wake wanapatiwa ulinzi wa ajira zao (security of tenure) sawa na wanaopatiwa majaji wa Mahakama ya
Tanzania ili kuzuia uwezekano wa wajumbe kuondolewa kwa sababu zisizotokana na
utendaji wao wa kitaaluma au ukosefu wa maadili. Kwa maana hiyo, mapendekezo ya
ibara ya 10 Muswada Mpya juu ya uhuru wa Tume hayatoshelezi hata kidogo. Hii ni
kwa sababu ibara ya 12 ya Muswada Mpya, ambayo inazungumzia ukomo wa ujumbe wa
Tume, haijaweka utaratibu wowote wa namna ya kushughulikia nidhamu ya wajumbe
pale kunapokuwepo tuhuma za ukiukaji wa Kanuni za Maadili zinazopendekezwa
katika ibara ya 12(2) na Jedwali la
Pili la Muswada. Kutokuweka utaratibu huu kuna hatari kubwa kwani,
kisheria, mamlaka ya uteuzi huwa ndio mamlaka ya nidhamu pale ambapo sheria
haijaweka utaratibu tofauti wa nidhamu. Hii ina maana kwamba bila kuweka
utaratibu wa kisheria wa nidhamu ya wajumbe wa Tume, Rais ndiye atakuwa na
uwezo wa kuwaondoa madarakani kwa sababu yeye ndiye aliyewateua!
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo letu la tatu linahusu hadidu za rejea. Hapa kuna hoja za aina mbili.
Kwanza, sambamba na pendekezo la kutompa Rais madaraka ya uteuzi wa wajumbe wa
Tume, Rais asipewe mamlaka ya kutoa hadidu za rejea kwa Tume. Pili, kwa vile – kama
inavyopendekezwa katika Muswada Mpya – hadidu za rejea ni hati ya kisheria
inayotakiwa kuzingatiwa na Tume katika utekelezaji wa majukumu yake, ni muhimu
hati hii iwekwe wazi katika sheria yenyewe badala ya kubakia kuwa siri ya Rais.
Watanzania lazima wajue Tume inapewa majukumu gani ya kisheria. Aidha, wajumbe
wa Tume wenyewe lazima wafahamu wanapewa majukumu gani ya kisheria na wafahamu
kwamba wanatakiwa kufuata matakwa ya sheria na sio maelekezo ya mtu mmoja hata
kama ni Rais wa Kifalme. Hii itasaidia uwajibikaji wa Tume kwa wananchi kwani
itakuwa rahisi kupima matokeo ya kazi ya Tume kwa hadidu za rejea zilizowekwa
wazi katika sheria.
Ukweli ni kwamba badala ya kumsubiri Rais kutoa hadidu za rejea, tayari ibara
za 9 na 16 za Muswada Mpya zimeshafanya hivyo kwa kuainisha kazi za Tume,
mipaka ya Tume katika utekelezaji wa kazi hizo na utaratibu wa namna ya
kuzifanya. Kwa ajili hiyo, zaidi ya kutaka kuonyesha kwamba Rais ana mamlaka
makubwa katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya, mapendekezo ya
ibara ya 8 hayana maana wala sababu yoyote na yanaweza kuondolewa bila kuathiri
maudhui ya Muswada. Aidha, kwa kuzingatia mapendekezo ya ibara ya 9,
haijulikani Rais atatoa maelekezo gani ya ziada yanayohusu kazi za Tume na
namna ya kuzitekeleza. Kwa upande mwingine, mapendekezo ya ibara ya 8 yanaweza
kuleta mkanganyiko na mgogoro wa kisiasa na kisheria usiokuwa wa lazima endapo
Rais atatoa hadidu za rejea zinazotofautiana na matakwa ya kisheria kama yanavyopendekezwa
na ibara 9 ya Muswada Mpya. Pendekezo letu, kwa hiyo, ni kwamba ibara ya 8
ifutwe yote na ibara za 9 na 16 zifafanuliwe vizuri ili kuweka wazi zaidi
hadidu za rejea za Tume na namna ya kuzitekeleza.
Mheshimiwa Spika,
Kuna mapendekezo mengine yaliyoko kwenye Muswada yanayoonyesha hatari za Urais
wa Kifalme. Kama tulivyoona, Tume inatakiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano na kwa Rais wa Zanzibar. Baada ya hapo, kwa mujibu wa ibara
ya 18(2) ya Muswada, “baada ya mashauriano na makubaliano na Rais wa Zanzibar na baada ya kumalizika kwa taratibu za ndani
zinazohusu utungaji wa sera, Rais atamwelekeza Waziri kuwasilisha Muswada
wa Katiba katika Bunge la Katiba kwa ajili ya kupitishwa kwa vifungu vya Katiba.”
Pendekezo hili ni la hatari kubwa. Kwanza, ‘kumalizika kwa taratibu za ndani
zinazohusu utungaji wa sera’ maana yake ni baada ya kukamilika kwa utaratibu wa
kawaida wa kiserikali unaohusu utungaji sera na sheria. Chini ya utaratibu huu,
rasimu ya muswada hupelekwa kwanza kwenye Kamati ya Watalaam ya Baraza la
Mawaziri (Inter Ministerial Technical
Committee of the Cabinet) kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho na Makatibu
Wakuu kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa maamuzi ya mwisho. Baada
ya maamuzi ya mwisho ya Baraza la Mawaziri, rasimu ya muswada hurudishwa Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuandikwa upya ndipo upelekwe
Bungeni la Katiba.
Katika hatua zote hizi, muswada wa sheria huweza kufanyiwa marekebisho makubwa.
Kwa maana hiyo, pendekezo la kuuwasilisha Muswada wa Katiba Mpya katika Bunge
la Katiba baada ya kuupitisha kwanza kwa Makatibu Wakuu ambao wote ni wateuliwa
wa Rais, na kwenye Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake wote (ukiacha Makamu
wa Rais na Rais wa Zanzibar) ni wateuliwa wa Rais ni kutengeneza mazingira ya
kisheria yatakayoruhusu uchakachuaji wa Muswada huo kwa lengo la kuhakikisha
matokeo yake ya mwisho, yaani Katiba Mpya, yanakidhi maslahi ya Rais na chama
chake cha CCM. Kwa vyovyote vile, pendekezo hili halikubaliki kwa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni.
SIFA ZA WAJUMBE
Mheshimiwa Spika,
Muswada Mpya unapendekeza sifa zifuatazo wanazotakiwa kuwa nazo wajumbe wa
Tume:
(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za
wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na sayansi ya
jamii;
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
(c) Maslahi ya umma;
(d) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbali mbali ya kijamii; na
(e) Vigezo vingine ambavyo Rais ataona vinafaa. (ibara ya 6(3)
Zaidi ya sifa zilizotajwa, ibara ya 6(4) inakataza watu wenye sifa zifuatazo
kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume:
(a) Wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, madiwani na
viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote kuanzia Wilaya hadi Taifa;
(b) Watumishi wa vyombo vya usalama;
(c) Watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au wanaotuhumiwa mahakamani
kwa mashtaka ya kukosa uaminifu au uadilifu;
(d) Watu wasiokuwa raia wa Tanzania.
Mapendekezo haya yana athari kubwa kwa mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba
Mpya. Kwanza, kwa kukataza viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya
siasa kuteuliwa wajumbe wa Tume kunaondoa kwenye mchakato wa Katiba Mpya kundi
kubwa la watu wenye utaalamu na uzoefu katika masuala mbali mbali ya kisiasa,
kikatiba, kisheria, kiuchumi, kiutawala, kifedha na kisayansi jamii. Vile vile,
viongozi wa vyama vya siasa wanawakilisha makundi makubwa ya kijamii yenye
mtawanyiko wa watu na wa kijiografia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na
wanawakilisha watu wa umri na jinsia zote kama inavyopendekezwa katika Muswada
Mpya.
Aidha, kwa kuwa maneno ‘maslahi ya umma’ hayajafafanuliwa katika Muswada,
hakuna anayeweza kudai kwamba viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya
siasa vilivyosajiliwa kisheria baada ya kutimiza masharti yote husika ya
kisheria, na ambao wanaungwa mkono na mamilioni ya wananchi wa Tanzania kwa
kupewa nafasi za uwakilishi katika taasisi za uwakilishi za umma kama Bunge,
Baraza la Wawakilishi na Halmashauri za Serikali za Mitaa hawajui wala
hawazingatii maslahi ya umma na kwa hiyo hawafai kuwakilishwa katika Tume ya
Mabadiliko ya Katiba! Kama ingekuwa hivyo, Rais – ambaye pia ni Mwenyekiti wa
CCM na kwa hiyo kiongozi wa chama cha siasa – naye pia atakuwa hana sifa za
kuteua Tume! Na wakati haja ya kutoshirikisha watumishi wa taasisi za ulinzi na
usalama katika mchakato wenye ubishani wa kisiasa kama utungaji wa Katiba Mpya
inaeleweka, ni matusi kwa watu waliochaguliwa na wananchi kuwa Wabunge,
Wawakilishi au Madiwani au viongozi wa vyama vya siasa vilivyowapendekeza watu
hao, kuwekwa pamoja na wahalifu na kutamkwa kuwa hawana sifa za kuteuliwa kuwa
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba!
Inaelekea lengo kuu la pendekezo hili ni kuhakikisha kwamba vyama vya upinzani,
hasa hasa CHADEMA, vyenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Bunge havipati fursa
ya kuamua muundo na maudhui ya Katiba Mpya hasa katika hatua muhimu za uundaji
wake. Pili, lengo kuu vile vile ni kuhakikisha kuwa Rais, na kwa hiyo chama
chake cha CCM, wanadhibiti mchakato wa Katiba Mpya katika hatua muhimu ya
uundaji wake. Endapo watafanikiwa katika hili, Rais na chama chake cha CCM
watakuwa na nafasi kubwa ya kuamua aina ya Katiba Mpya itakayotokana na
mchakato walioudhibiti kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya. Hii ni kwa
sababu, kwa kutumia uzoefu wa Tume nyingine zilizopata kuteuliwa miaka ya
nyuma, wajumbe wengi huwa ni watumishi au waliopata kuwa watumishi wa Serikali
na/au taasisi zake. Wajumbe wa aina hii wamekuwa hawana uthubutu wa kupendekeza
mabadiliko makubwa yanayohitajika katika mfumo wa utawala wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Badala ya kukataza viongozi wa vyama vya siasa kama inavyopendekezwa na Muswada
Mpya, na kwa kuzingatia nafasi ya vyama vya siasa katika historia yetu na mfumo
wetu wa utawala, na kwa lengo la kuhakikisha Tume inakuwa na utaalamu, uzoefu
na uhalali wa kisiasa unaohitajika, watu wanaostahili kuteuliwa kuwa wajumbe wa
Tume wawe ni wale wenye sifa zinazopendekezwa na ibara ya 6(3)(a), (b), (c) na
(d) ya Muswada. Kwa sababu hiyo, hakutakiwi kuwa na vigezo vingine
visivyojulikana wazi kwa wananchi. Kwa maneno mengine, pendekezo la kuwa na
‘vigezo vingine ambavyo Rais ataona inafaa’ halikubaliki kwani linampa Rais
mwanya wa kuteua marafiki zake au watu ambao hawana sifa zinazojulikana. Kwa maoni
yetu vile vile, badala ya kuwa sababu ya disqualification, uongozi wa kuchaguliwa na wananchi katika taasisi
za uwakilishi au katika vyama vya siasa unatakiwa kuwa an added advantage pale ambapo
kiongozi husika ana sifa za kitaaluma zinazotakiwa!
MISINGI MIKUU YA KITAIFA
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kuwepo kwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ambayo Tume
inatakiwa kuizingatia kwa lengo la kuihifadhi na kuidumisha. Misingi mikuu
inayopendekezwa ni:
(a) Kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) Uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) Mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) Umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(e) Uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa
kuzingatia haki ya watu wote kupiga kura;
(f) Ukuzaji na na uhifadhi wa haki za binadamu;
(g) Utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo wa sheria; na
(h) Uhuru wa kuabudu na uvumilivu wa dini nyingine. (ibara ya 9(2)
Kifungu hiki kimefanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno ‘Tume itahakikisha ...
kutokugusika na utakatifu (inviolability
and sanctity) wa mambo yafuatayo’ yaliyokuwa katika Muswada wa Zamani, na
badala yake yamewekwa maneno mapya ‘... kuhifadhi na kudumisha mambo
yafuatayo....’ Mabadiliko haya yamefanywa ili kujaribu kuondoa hofu
iliyojitokeza wakati wa mikutano ya kukusanya maoni ya wadau kwamba lengo la
pendekezo hilo lilikuwa kuzuia mjadala juu ya masuala ya kikatiba yenye utata
mkubwa kama vile suala la Muungano. Hata hivyo, hatari ya kuzuiliwa kwa mjadala
juu ya misingi mikuu ya kitaifa bado haijaondolewa kwani, kwa mujibu wa ibara
mpya ya 9(3), “... Tume itatoa fursa kwa
watu kutoa maoni yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala
hayo.” Tafsiri halisi ya maneno haya ni kwamba mjadala pekee utakaoruhusiwa
juu ya ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni ule ambao lengo lake ni ‘kuendeleza na
kuboresha masuala hayo.’
Kwa maoni yetu, lengo kuu la pendekezo linalohusu kuendeleza na kuboresha
‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni kuzuia mjadala wenye kuhoji ‘kuwepo kwa Jamhuri
ya Muungano’ ili kuendeleza mfumo wa sasa wa Muungano wenye Serikali mbili. Hii
ni kwa sababu katika mambo yote yanayopendekezwa kuwa misingi mikuu ya kitaifa,
ni ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ yenye Serikali mbili ndio ambayo imekuwa na
mgogoro mkubwa kwa muda wote wa maisha ya Jamhuri ya Muungano. Ukiacha ‘ukuzaji
na uhifadhi wa haki za binadamu’ ambalo lilikataliwa na Serikali ya Mwalimu
Nyerere kwa miaka yote ya utawala wake, mambo mengine yote yanayotajwa kuwa
‘misingi mikuu ya kitaifa’ hayajawahi kubishaniwa kwa miaka yote ya uhai wa
Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo la ‘misingi mikuu ya kitaifa’ linastaajabisha sana kwani, kwa mujibu
wa ibara ya 98(1)(b) ya Katiba ya sasa, ‘kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano, Ofisi
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Kamhuri ya Muungano,
kuwapo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Zanzibar,
Orodha ya Mambo ya Muungano na idadi ya Wabunge kutoka Zanzibar’ ni mambo
yanayoweza kubadilishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ili mradi tu mabadiliko
hayo yaungwe mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa kutoka Tanzania Bara na
wa Tanzania Zanzibar. Kwa sababu hiyo, pendekezo la ibara ya 9(3) ya Muswada
kwamba ‘misingi mikuu ya kitaifa’ izungumzwe kwa lengo la kuiendeleza na
kuidumisha tu halikubaliki kwa sababu linazuia uhuru wa kuhoji na/au kupinga
mambo ambayo kwa Katiba ya sasa ni ruhusa kuyahoji, kuyapinga na/au hata
kuyabadilisha! Tunapendekeza ibara ya 9(2) na (3) za Muswada zifutwe kabisa ili
kuwepo na uhuru kamili wa kujadili, kwa kupinga au kuunga mkono, kila jambo
linalohusika na Katiba Mpya.
NAFASI YA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Pengine mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika Muswada ni mapendekezo
yanayohusu nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Itakumbukwa
kwamba moja ya masuala yaliyozua tafrani kubwa katika mchakato wa kukusanya
maoni juu ya Muswada wa Zamani hasa katika kituo cha Zanzibar ni kuwepo hisia
kwamba nafasi ya Zanzibar ilikuwa imepuuzwa katika Muswada huo. Muswada sio tu
kwamba umetekeleza matakwa yote ya ushirikishwaji wa Zanzibar, bali umekwenda
mbali zaidi kwa kuifanya Zanzibar mwamuzi wa mustakbala wote wa kikatiba wa
Tanzania. Hii imefanyika kwa njia mbili: kwanza, kwa kumfanya Rais wa Zanzibar
kuwa mshirika sawa wa kikatiba wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; na pili, kwa
kuipa Zanzibar nafasi kubwa ya uwakilishi katika mchakato mzima wa Katiba
Mpya.
NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kwamba utekelezaji wa mamlaka yote ya Rais, Waziri na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano lazima ufanyike kwa
‘mashauriano na makubaliano’ na Rais, Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Kwa mfano, ibara ya 5 inayohusu kuundwa kwa Tume inamtaka Rais ‘kushauriana na
kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar na kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Vile vile,
ibara ya 6(1) inayohusu uteuzi wa wajumbe wa Tume; ibara ya 8(1) na (2)
inayohusu hadidu za rejea na kuongeza muda wa Tume; na ibara ya 13(2) inayohusu
uteuzi wa Katibu wa Tume, zote zinataka kuwepo na makubaliano na Rais wa
Zanzibar. Aidha, ibara ya 13(5) inayohusu uteuzi wa watendaji wengine wa Tume
inalazimu makubaliano kati ya Waziri na Waziri mwenzake wa Zanzibar ambao nao
ni wateuliwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.
Mamlaka ya Rais wa Zanzibar hayaishii tu kwenye uteuzi wa wajumbe na watendaji
wa Tume, bali pia yanaingia hata katika uwasilishaji wa ripoti ya Tume. Kwa
mujibu wa ibara 18(1) ya Muswada, mara baada ya kumaliza kazi yake, Tume
itawasilisha ripoti yake kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar. Aidha, kwa mujibu wa
ibara ya 18(2), mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais, ‘baada ya kushauriana
na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar, “... atamuagiza Waziri kuwasilisha Muswada
wa Katiba katika Bunge la Katiba.” Kwa mapendekezo haya pia, Rais wa Zanzibar
sio tu kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia
ana kura ya turufu katika mchakato wa Katiba Mpya. Maana yake ni kwamba Rais wa
Zanzibar asipopatiwa nakala ya ripoti ya Tume au asipokubaliana na Rais wa
Muungano, basi Muswada wa Katiba hautawasilishwa kwenye Bunge la Katiba!
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo haya yanaashiria kuwepo kwa mtazamo ambao chanzo chake ni
Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Tanganyika ya tarehe 25 Aprili 1964. Kwa mtazamo huo, Zanzibar ni nchi huru
kama ilivyokuwa mwaka 1964 na kwa hiyo ni lazima sio tu ishirikishwe kwa usawa,
bali pia lazima ikubaliane na mabadiliko yoyote ya kikatiba yanayopendekezwa na
Muswada. Kama Profesa Palamagamba Kabudi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam alivyosema kwenye Semina ya Wabunge Juu ya Muswada wa Sheria
ya Marekebisho ya Katiba iliyofanyika tarehe 12 Novemba 2011: ‘Katika kuandika
katiba mpya, wabia wa Muungano wanarudi kwa usawa.’
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mtazamo huu sio sahihi. Kwanza kabisa, Zanzibar
sio nchi huru tena kama ilivyokuwa mwaka 1964, kama ambavyo hakuna tena nchi
inayoitwa Tanganyika wala serikali yake. Hii ni kwa sababu tangu kusainiwa kwa
Hati za Muungano mwaka 1964, na kwa mujibu wa ibara ya 4(3) ya Katiba ya sasa,
masuala yote yanayohusu Muungano kama vile Katiba ya Tanzania yamekasimiwa kwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambayo pia imekasimiwa mamlaka juu ya masuala
ya iliyokuwa Tanganyika. Masuala haya ya Muungano hayawezi kujadiliwa upya na
kwa usawa kati ya nchi hizi mbili kwa vile moja kati ya nchi hizo haipo tena na
iliyobaki imepoteza sehemu ya uhuru wake kutokana na Muungano huo! Hii ndio
kusema hakuwezi tena kuwa na wabia wa Muungano bila kwanza kuirudisha
Tanganyika kama nchi na bila kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yenye uhuru
na mamlaka kama iliyokuwa nayo kabla ya Muungano!
Pili, kuna dhana kwamba Rais wa Zanzibar hakushirikishwa katika mchakato wa
maandalizi ya Muswada wa Zamani. Dhana hii vile vile ni potofu. Kwanza, Rais
Ali Mohamed Shein mwenyewe ametamka wazi kwa waandishi wa habari kwamba
alishiriki katika hatua zote za maamuzi kwenye Baraza la Mapinduzi. Pili,
mujibu wa ibara ya 54(1) ya Katiba ya sasa, Rais wa Zanzibar ni mmoja wa
wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa hiyo ni
mshiriki wa maamuzi yote ya Serikali hiyo. Kwa maana hiyo, maslahi ya Zanzibar
yanawakilishwa ndani ya ‘chombo kikuu cha kumshauri Rais’ katika Jamhuri ya
Muungano. (ibara ya 54(3) Hii ni licha ya ukweli kwamba, kwa mlolongo wa
madaraka uliopo katika ibara ya 54(2), Rais wa Zanzibar sio mmoja wa wajumbe
wanaoweza kuongoza mikutano ya Baraza hilo.
Aidha, ndani ya Baraza la Mawaziri, Zanzibar inawakilishwa pia na Makamu wa
Rais ambaye – kwa mujibu wa ibara ya 47(1) ya Katiba ya sasa – “... ndiye
Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano....” Kwa maana
hiyo, mapendekezo ya Muswada yanayomfanya Rais wa Zanzibar kuwa sio tu mshiriki
sawa lakini pia mwamuzi wa mustakbala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanaenda
kinyume sio tu na Katiba ya sasa bali pia na Hati za Muungano wenyewe. Kwa
mapendekezo haya, endapo Rais wa Zanzibar hatakubaliana na uteuzi wowote wa
wajumbe wa Tume au Katibu wake au watendaji wake wengine, anaweza kusimamisha
mchakato mzima wa kikatiba hata kama unahusu masuala ya Tanzania Bara yasiyo ya
Muungano!
UWAKILISHI WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa
Zanzibar pekee yake. Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi
kubwa iliyo nayo katika vyombo vya maamuzi vinavyopendekezwa na Muswada. Kwa
mfano, kwa mujibu wa ibara ya 6(2), “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa
kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Hii
ina maana kwamba wajumbe wa Tume na Sekretarieti yake wanatakiwa wawe sawa kwa
sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Ikumbukwe kwamba Tume hii inatengeneza
Katiba inayohusu masuala ya Muungano, ambayo ni haki kwa Zanzibar kushirikishwa
kwa usawa kabisa, na vile vile masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara
ambayo Zanzibar haina haki ya kushiriki.
BUNGE LA KATIBA
Mheshimiwa Spika, Eneo la pili ambalo Zanzibar ina ushawishi mkubwa
kutokana na uwakilishi wake ni katika Bunge la Katiba linalopendekezwa katika
Sehemu ya Tano ya Muswada. Kwa mujibu wa ibara ya 20(2), wajumbe wa Bunge la
Katiba watakuwa ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano; wajumbe wote
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar; mawaziri wa katiba na sheria wa Jamhuri ya
Muungano na wa Zanzibar; Wanasheria Wakuu wa Jamhuri ya Muungano na wa
Zanzibar; na wajumbe mia moja kumi na sita wakaoteuliwa kutoka asasi
zisizokuwa za kiserikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vyenye usajili wa
kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalum katika jamii.
Inaelekea kwamba, kwa mujibu wa ibara ya 20(4), wajumbe wasiokuwa wabunge ama
wawakilishi nao pia watateuliwa na Rais licha ya kutoka nje ya mfumo wa
kiserikali!
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(a) ya Katiba ya sasa ya
Muungano, wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni pamoja na wabunge wa
majimbo ya uchaguzi. Kwa composition ya
sasa ya Bunge, kuna jumla ya majimbo ya uchaguzi 239 ambayo kati yao majimbo ya
Zanzibar ni hamsini. Vile vile, kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(c) ya Katiba,
Baraza la Wawakilishi Zanzibar linawakilishwa na wabunge watano katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano. Aidha, kama inavyotakiwa na ibara ya 66(1)(b), kuna
wabunge wanawake mia moja na mbili wanaojulikana kama ‘wabunge wa viti maalum.’
Kwa mgawanyo wa sasa wa wabunge hawa, idadi ya wanaotoka Zanzibar ni ishirini
na tano kwa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni. Na mwisho, kuna wabunge
wasiozidi 10 wanaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya
66(1)(e). Hadi sasa, Rais ameshateua wabunge watatu ambao wote ni wa kutoka
Zanzibar. Kwa hiyo, katika Bunge la sasa lenye wabunge 353, wabunge
wanaowakilisha Zanzibar ni themanini na tatu au karibu 23.5% ya wabunge wote wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Tano ya Katiba ya Zanzibar, wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni pamoja na wawakilishi wa majimbo hamsini
ya uchaguzi, wawakilishi kumi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar na wawakilishi
ishirini wa viti maalum na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Kwa hiyo, jumla ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa sasa ni
themanini na moja. Kwa maana nyingine ni kwamba endapo mapendekezo ya ibara ya
20(1)(b), (c) na (d) ya Muswada yatakubaliwa, idadi ya wajumbe wa Bunge la
Katiba wanaotoka Zanzibar itaongezeka hadi kufikia mia moja sitini na nne kati
ya wajumbe 545 wa Baraza hilo kwa mujibu wa ibara ya 20(2). Idadi hii ni sawa
na 30% ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Idadi hiyo ya uwakilishi wa Zanzibar bado haitakidhi matakwa ya Muswada kwani
ibara ya 20(3) inapendekeza kwamba “...
idadi ya wajumbe wa Baraza la Katiba kutoka Tanzania Zanzibar ... haitapungua
theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba”! Theluthi moja ya wajumbe
wa Bunge la Katiba ni wajumbe 182. Kwa hiyo ili kukidhi matakwa ya Muswada
kuhusu uwakilishi wa Zanzibar, itabidi wajumbe 18 kati ya 116 waliotajwa na
ibara ya 20(2)(e) watoke Zanzibar ili kufikisha idadi ya wajumbe 182 ambayo
ndio theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Mheshimiwa Spika,
Kuna maeneo mengine ya Muswada ambayo pia yanazua maswali mengi juu ya nafasi
ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Kwa mfano, wakati ibara ya 21(1)
inapendekeza kwamba Spika na Naibu Spika wa Bunge la Katiba wachaguliwe kutoka
miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo, ibara ya 21(2) inapendekeza kwamba endapo
Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano basi Naibu wake lazima atoke
upande mwingine. Sambamba na pendekezo hili, ibara ya 22(1) inapendekeza Makatibu
wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
watakuwa ndio Katibu na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba. Aidha, sawa na ibara
ya 21(2), ibara ya 22(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja
wa Jamhuri ya Muungano, basi Katibu wa Bunge la Katiba lazima atoke upande
mwingine.
Mapendekezo haya yanaonyesha sio tu nafasi na ushawishi mkubwa wa Zanzibar
katika mchakato wa Katiba Mpya, bali pia ni mwendelezo wa dhana potofu kwamba
Zanzibar ni mshirika sawa wa Jamhuri ya Muungano. Hii inathibitishwa pia na
pendekezo la ibara ya 24(3) ya Muswada inayotaka Katiba Mpya ikubaliwe na
theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Tanzania Bara na vile
vile theluthi mbili ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba
iwe ni kwa masuala ya Muungano yanayoihusu Zanzibar pia, au kwa masuala
yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo hayaihusu, Zanzibar itakuwa na
kura ya turufu kwa mujibu wa mapendekezo ya Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, Uwakilishi mkubwa wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano umetumika kihistoria kwa lengo la kuwatuliza Wazanzibari wakati
Serikali ya Mwalimu Nyerere ilipokuwa inamomonyoa uhuru wa Zanzibar kwa
kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano kwenye Katiba ya Muungano. Katika kitabu
chake Pan Africanism or Pragmatism?
Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union, Profesa Issa Shivji, mwanazuoni
mashuhuri wa kikatiba na mwanafunzi wa historia ya Muungano huu amemnukuu
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa utawala wa hayati Sheikh Abedi
Amani Karume, Bw. Wolfgang Dourado akimnukuu Sheikh Karume juu ya nafasi ya
Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano: “‘Msiwe na wasi wasi, sisi tuna
haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao lakini wao hawana haki ya kuwakilishwa
katika Baraza letu la Mapinduzi’”!
Mheshimiwa Spika, Sababu nyingine inatokana na kuongezeka kwa ushawishi na
nafasi ya Zanzibar katika siasa za ndani ya CCM, hasa hasa katika zama hizi za
vyama vingi na vita za makundi mbali mbali ndani ya chama hicho. Katika mazingira
haya, mtu yeyote anayetaka kupitishwa kuwa mgombea urais kwa kupitia CCM
anakuwa anahitaji kura za CCM Zanzibar ili kushinda katika kinyang’anyiro
hicho. Kwa kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwenyewe katika kitabu
chake Uongozi Wetu na Hatima ya
Tanzania, “sababu moja kubwa iliyofanya viongozi wetu wasitake kuwaudhi
‘Wazanzibari’ ... ni umuhimu wa kura za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa
CCM kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi yeyote
anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu kupita mengine yote, kuwaudhi
‘Wazanzibari’ ni dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila njia.” Kwa maoni ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hofu hii ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ndio
imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano - juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano uliofanywa
na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya
Katiba ya Zanzibar, 2010.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba upendeleo wa Zanzibar
unaopendekezwa katika Muswada huu kuhusiana na uwakilishi katika Bunge la
Katiba na katika vyombo vingine vya maamuzi juu ya mchakato wa Katiba Mpya sio
wa haki na haukubaliki tena. Kwanza, ibara ya 64(2) ya Katiba ya sasa inaweka
wazi kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina mamlaka ya kutunga sheria
katika Zanzibar ‘... juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano....’ Hii pia
ndio lugha ya ibara ya 78(1) ya Katiba ya Zanzibar kama ilivyofanyiwa
marekebisho mwaka jana. ‘Katiba ya Tanzania’ ni jambo la kwanza katika orodha
ya Mambo ya Muungano iliyoko kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano. Kwa Muswada Mpya kupendekeza kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar
liwe sehemu ya Bunge la Katiba ni kukiuka wazi wazi matakwa ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano na ya Katiba ya Zanzibar. Ni ajabu iliyoje kwamba wale
wanaojifanya ni machampioni wa Muungano wanaweza kunyamazia ukiukaji huu wa
Katiba!
Mheshimiwa Spika, Thomas Paine, mwandishi maarufu wa Marekani ya wakati wa
Mapinduzi ya mwaka 1776, aliwahi kuandika kijitabu alichokiita Common Sense juu ya uhalali wa
Uingereza kutawala Bara la Amerika ya Kaskazini ambako alisema: ‘... [T]here is something very absurd in
supposing a continent to be perpetually governed by an island [for] in no
instance hath nature made the satellite larger than its primary
planet...’! Yaani, ni ujinga kudhani kwamba bara linaweza kutawaliwa
milele na kisiwa kwa sababu utaratibu wa asili haujawahi kufanya kitegemezi
kuwa kikubwa kuliko sayari yake ya msingi. Hata kama ni kweli kwamba Tanganyika
sio bara kama ilivyokuwa Marekani ya Kaskazini, bado tunakubaliana na Tom Paine
kwamba ni ujinga kudhani kwamba
Visiwa vya Zanzibar vitaendelea kuwa na maamuzi na ushawishi mkubwa katika
masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika kwa sababu utaratibu wa asili
haujawahi kufanya maslahi ya Visiwa hivyo kuwa bora zaidi ya maslahi ya
Tanganyika!
Kwa maoni yetu, wakati umefika kwa Muungano kuwekwa kwenye msingi wa usawa na
imara zaidi. Msingi huo unahitaji kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika
ambayo ndio ilikuwa – pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – mbia mkuu
wa Muungano wa mwaka 1964. Kurudishwa huko kwa Tanganyika kutaiwezesha Zanzibar
kujadiliana nayo kwa usawa juu ya masuala yote yanayohusu Muungano. Haya yote
yanawezekana tu endapo Muungano huu utawekwa mbele ya wananchi ili waamue – kwa
kura ya maoni - kama wanataka kuendelea nao au la; na kama wanataka kuendelea
nao ni muundo gani wa Muungano wanaoutaka.
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya kurudishwa kwa Tanganyika na Serikali yake sio mapya. Miaka
ishirini iliyopita, Tume ya Rais ya
Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa (Tume ya Nyalali)
ilipendekeza hivyo hivyo. Miaka saba baadae, Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba, White Paper Na. 1 ya 1998 (Tume
ya Kisanga) nayo ilipendekeza hivyo hivyo. Kuendelea kupuuza mapendekezo haya
wakati Zanzibar inavunja Katiba ya sasa ya Muungano; kuendelea kukaa kimya kwa
hofu ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ wakati wao wanajitwalia uhuru wa kujiamulia
mambo yao wenyewe huku wakiendelea kushiriki katika maamuzi ya mambo ya Tanganyika
yasiyokuwa ya Muungano; kuendeleza kile alichokiita Mwalimu Nyerere falsafa ya
‘changu ni changu, chako ni chetu’ katika mahusiano ya Zanzibar na Tanzania
Bara, ni kutulazimisha tuipinge dhana nzima ya Muungano kati ya nchi zetu mbili
kitu kinachoweza kupelekea kuvunjika kwa Muungano wenyewe. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni isingependa tufike huko lakini ndoa hii ya kulazimishana
haiwezi ikadumu muda mrefu kwa taratibu za aina hii.
UDHOOFISHAJI WA UPINZANI
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya Muswada juu ya uwakilishi katika Bunge la Katiba yana athari
nyingine kubwa katika majadiliano na maamuzi ndani ya Bunge la Katiba. Kwa
mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Profesa Issa G. Shivji kwa Kamati ya Katiba,
Sheria na Utawala, endapo mapendekezo ya ibara ya 20(2) ya Muswada
yatapitishwa, CCM itakuwa na kati ya wajumbe 350 hadi 400 katika Bunge la
Katiba ambalo lina wajumbe 545. Kwa upande mwingine Chama cha Wananchi (CUF)
ambacho kina Wawakilishi 29 katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kitakuwa na
wajumbe 65 katika Bunge la Katiba. Kwa maana ya uwakilishi katika Bunge la
Katiba, CUF itakuwa ndio chama cha pili kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge
hilo, licha ya kuwa na wabunge wawili tu wa kuchaguliwa kwa upande wa Tanzania
Bara na licha ya kupata kura chache sana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
jana.
Na kama inavyojulikana, tangu Muafaka wa Kisiasa Zanzibar kati ya CCM na CUF wa
mwaka 2010 na kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, upinzani wa kisiasa
Zanzibar umekufa na kwa upande wa Tanzania Bara, na hasa Bungeni na kwenye
chaguzi ndogo kama ule wa Igunga, CUF imekuwa ikishirikiana na CCM kuipinga
CHADEMA. Kwa mapendekezo haya, kambi ya CCM na CUF katika Bunge la Katiba
inaweza kufika hata zaidi ya wajumbe 465 katika ya wajumbe 545 wa Bunge hilo!
CHADEMA ambayo kwa sasa ndio chama kinachoongoza Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, itabakia na Wabunge wake
48 na vyama vya kibunge vilivyobaki, yaani NCCR-Mageuzi, TLP na UDP vitabaki na
jumla ya Wabunge sita. Kwa hiyo, CHADEMA itakuwa chama cha tatu kwa nguvu
za kisiasa ndani ya Bunge la Katiba licha ya kuwa ni chama kikuu cha
upinzani chenye nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini!
Kwa maana nyingine, iwe ni kwa makusudi au bila ya kujua au kwa kunuia, athari
mojawapo kubwa ya mapendekezo ya Muswada kuhusu uwakilishi katika Bunge la
Katiba itakuwa ni kuiongezea nguvu zaidi kambi ya CCM/CUF na kupunguza nguvu na
ushawishi wa CHADEMA ambayo ndio chama pekee kinachobeba matarajio na matamanio
ya Watanzania wengi wanaotaka mabadiliko ya kimsingi ya kisiasa, kiuchumi na
kijamii katika nchi yetu. Haihitaji kuwa na shahada ya uzamivu kujua kwamba
Bunge la Katiba lenye uwakilishi wa aina hii litapitisha Katiba Mpya ambayo
pengine itatofautiana na Katiba ya sasa kwa jina tu! Na wala haihitaji kisomo
kikubwa kujua kwamba Bunge la Katiba la aina hii halitagusa ‘msingi mkuu’
uliobaki wa Jamhuri ya Muungano, yaani Serikali mbili. Hapa pia ni wazi kuwa
lengo halisi la mapendekezo haya ni kuhakikisha kwamba mchakato wa Katiba Mpya
utazaa matunda yasiyokuwa tofauti sana na ya Katiba ya sasa!
‘UWAKILISHI’ WA BUNGE LA
KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Sio Bunge hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wala Baraza la Wawakilishi
Zanzibar lenye mamlaka kikatiba na kisiasa ya kutunga Katiba Mpya ya Tanzania.
Hii ni kwa sababu sisi wote tulioko humu ndani tulichaguliwa kwa mujibu wa
Katiba ya sasa na mamlaka yetu yote yako ndani ya kona nne za Katiba hiyo. Kama
ni kweli, kama anavyodai Profesa Kabudi, kwamba kitendo cha kutunga Katiba Mpya
vile vile ni kitendo cha kuua Katiba ya Zamani, basi sisi Wabunge na
Wawakilishi wa Zanzibar hatuna mamlaka ya kuiua Katiba ya sasa kwa sababu sisi
wote tulikula kiapo cha kuilinda, kuihifandhi na kuitetea.
Pili, sisi sote ni Wabunge na Wawakilishi wa vyama vya siasa kwa sababu, kwa
mujibu wa Katiba ya sasa sheria zote husika, tumechaguliwa kwa sifa kuu ya kuwa
wanachama wa, na tuliopendekezwa na, vyama vya siasa. Kuligeuza Bunge la
Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa Bunge la Katiba ni sawa
na kusema kwamba wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa hawana haki ya
kushiriki katika kutunga Katiba Mpya kwa sababu ya kuwa na kilema cha kisheria
kinachowakataza kuchaguliwa kuwa Wabunge na Wawakilishi! Ibara ya 20(4) ya
Katiba ya sasa inatamka wazi kwamba “... ni marufuku kwa mtu yeyote
kulazimishwa kujiunga na chama chochote....” Sio kosa, kwa hiyo, kwa mamilioni
ya Watanzania ambao wameamua kwa hiari zao kutokuwa wanachama wa vyama vya
siasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikubaliani, na haiwezi kukubali,
ubaguzi wa aina hii dhidi ya Watanzania walioamua kutumia haki zao za kikatiba
ya kutokujiunga na chama chochote cha siasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni haitakubali Watanzania hao waadhibiwe kwa kunyimwa kushiriki katika
Bunge la Katiba kwa sababu tu ya kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa.
Tatu, wajumbe 116 wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa mujibu
wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa, wawakilishi
wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi zao
kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza
wateuliwe na Rais. Pili, Bunge la Katiba ni chombo cha uwakilishi wa moja kwa
moja wa wananchi na kwa mila na desturi zinazokubalika na kutumika kimataifa,
wajumbe wa Bunge la Katiba huchaguliwa moja kwa moja na wananchi bila ya kujali
vyama vya siasa na huwa na kazi moja tu: kutunga Katiba Mpya. Kwa sababu zote
hizi, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wajumbe wa
Bunge la Katiba wachaguliwe moja kwa moja na wananchi na kusiwe na masharti
yoyote kuhusu uanachama wa vyama vya siasa.
UHALALISHAJI WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
Muswada una mapendekezo ambayo yanaashiria kuachana na utaratibu wa kihistoria
wa utungaji wa Katiba ambao umewaweka wananchi kando katika michakato wa
kikatiba tangu miaka ya mwanzo ya uhuru. Kwa mujibu wa ibara ya 27(1), kutakuwa
na kura ya maoni kwa lengo la kuihalalisha Katiba Mpya. Kwa mujibu wa ibara ya
30, watu wote walioandikishwa kuwa wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Taifa na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, watakuwa
na haki ya kupiga kura katika kura hiyo ya maoni. Aidha, kufuatana na ibara ya
32(2), matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa msingi wa kuungwa mkono kwa
zaidi ya 50% ya kura zote zilizopigwa Tanzania Bara na kiasi hicho hicho kwa
Zanzibar.
Mapendekezo ya ushirikishwaji wa wananchi katika kuipa Katiba uhai wa kisheria
ni jambo la maana sana na linaonyesha kuwa tumeanza kuachana na urithi wa
kikatiba wa kikoloni ulioanza na Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961. Hata hivyo,
mapendekezo haya yamejaa mitego na vichaka vingi vya hatari. Kwanza, ibara ya
27 inapendekeza kwamba kura ya maoni itaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume hizi mbili –
kwa mashauriano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar - ndizo zitakazotengeneza swali litakaloulizwa
kwenye kura ya maoni. (ibara ya 28(1) na (2) Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 31,
utaratibu utakaotumika katika kura ya maoni ni ule unaotumika katika chaguzi za
kawaida katika nchi yetu, yaani Sheria
ya Uchaguzi wa Taifa, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na
Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kauli yake
ndani ya Bunge hili wakati wa kujadili Makadirio na Matumizi ya Wizara ya
Katiba na Sheria tarehe 24 Agosti, 2011: “Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani, sio tu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
bali pia na mfumo mzima wa kisheria na kitaasisi unaoendesha chaguzi za nchi
yetu. Mfumo huu na watendaji wake wameonyesha wazi kutokuwa huru na kutumiwa na
Chama cha Mapinduzi kuchakachua matokeo ya chaguzi mbali mbali hapa nchini. Kwa
maana hiyo, Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na ile ya Zanzibar, haiwezi kuachiwa
jukumu kubwa la kuendesha kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya. Kambi
Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Serikali ilete bungeni muswada wa
mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba na ya sheria husika za uchaguzi kwa lengo
la kuiunda upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha inasimamia
zoezi la kura ya maoni kwa uhuru na bila upendeleo kwa chama tawala.”
Kuna maeneo mengine ambayo nayo yanaonyesha kwamba lengo halisi la Muswada huu
ni kupata Katiba ambayo haitabadilisha mambo ya msingi ila itakuwa mpya kwa
jina tu. Kwanza, ibara ya 26(2) inapendekeza kumpa Rais mamlaka ya “kuliitisha
tena Bunge la Katiba lenye wajumbe wale wale siku zijazo kwa ajili ya kutunga
masharti ya katiba kabla ya kuizindua Katiba inayopendekezwa kwa lengo la
kurekebisha masharti yaliyomo kwenye Katiba iliyopendekezwa.” Maana halisi ya
maneno haya ni kwamba Rais atakuwa na mamlaka ya kuita tena Bunge la Katiba ili
lifanye marekebisho ya mambo ambayo yeye au serikali yake au chama chake
hawayapendi katika Katiba Mpya kabla haijapigiwa kura ya maoni na wananchi!
Kama chombo huru cha wananchi, Rais hawezi kujipa madaraka ya kupingana na
kauli ya wananchi kupitia Bunge la Katiba.
Pili, wakati ibara ya 32(3) inapendekeza kurudiwa kwa kura ya maoni endapo kura
za ‘NDIYO’ na ‘HAPANA’ zitalingana, ibara ya 32(4) inaelekeza kwamba “endapo
wingi wa kura ya maoni utakuwa ni ‘HAPANA’, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
mwaka 1977, itaendelea kutumika.” Endapo pendekezo hili litapitishwa na kuwa
sheria, hii itakuwa ni kualika maasi kwa vile, kwa vyovyote vile, wananchi wa
Tanzania – baada ya kupitia mchakato mrefu wa kutengeneza Katiba Mpya –
hawatakubali tena kuvishwa minyororo ya Katiba ya sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inapendekeza kwamba badala ya kurudi kwenye status quo ante kama inavyopendekezwa, mchakato wa Katiba Mpya
uanze tena hadi hapo utakapopatikana muafaka wa kitaifa wa katiba.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, 2011 ni Muswada muhimu kuliko pengine miswada yote ambayo
Bunge la Kumi litapata fursa ya kuijadili na kuipitisha. Ni muswada wa
kihistoria kwa vile, tangu uhuru wa Tanganyika miaka hamsini iliyopita, na
tangu Muungano miaka karibu arobaini na nane iliyopita, Watanzania hatujawahi
kupata fursa ya kujadili na kuamua mustakbala wa taifa letu kikatiba kwa
utaratibu kama unaopendekezwa katika Muswada huu. Hata hivyo, kwa jinsi ambavyo
Muswada huu ulivyoandaliwa na kwa maudhui yake na kwa jinsi ulivyoletwa Bungeni
kwa kukiuka makusudi Kanuni za Bunge, ni wazi – kama utapitishwa jinsi ulivyo –
Watanzania tutakuwa tumekosa fursa ya kuamua mustakbala wa taifa letu kwa njia
ya amani na maridhiano. Bunge hili tukufu lina wajibu mbele ya historia na kwa
vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu
ya Tanzania tunayoitaka. Hukumu ya historia, endapo Bunge hili tukufu
litaendekeza ushabiki wa kisiasa na kufanya maamuzi ya mambo makubwa kama haya
kwa kupiga kelele au kwa kuzomea au kwa kugonga meza kwa nguvu, itakuwa ni kali
sana. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiwezi kuwa sehemu ya maamuzi makubwa
kama yanayopendekezwa na Muswada huu bila kwanza wananchi wa Tanzania na
Wabunge wenyewe kupata muda wa kutosha wa kuyatafakari masuala haya yote kwa uzito
unaoyastahili na kuyafanyia maamuzi ya busara.
Kwa sababu hizi zote, Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja chini ya kanuni ya
86(3)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge hili tukufu kwamba Bunge hili likatae
Muswada huu Kusomwa Mara ya Pili kwa sababu Serikali imeleta Muswada Mpya na
wenye mabadiliko makubwa na ya msingi bila kufuata masharti ya kanuni ya 84(3)
ya Kanuni za Kudumu za Bunge; na pia kwa sababu Serikali haijatekeleza maagizo
ya Bunge hili tukufu kuhusu kutoa muda zaidi kwa Kamati na wananchi kuufikiria,
kuuelewa na kuutolea maoni Muswada huu kinyume na matakwa ya ibara ya 18(a) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano juu ya uhuru wa wananchi kutoa maoni yao; ibara
ya 21(1) na (2) juu ya haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wan chi, na
haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo
yanayowahusu wananchi, maisha yao au yanayolihusu Taifa.
Mheshimiwa Spika,
naomba kuwasilisha.
---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI& WAZIRI KIVULI, KATIBA NA
SHERIA