JK: Kama si Mkapa leo tungekuwa shirikisho

1 view
Skip to first unread message

Fusha

unread,
Feb 5, 2007, 6:16:30 AM2/5/07
to Mtaa Kwa Mtaa
RAIS Jakaya Kikwete ameshangazwa na hatua ya baadhi ya wanasheria na
wanasiasa kumlaumu yeye kutokana na kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa
Shirikisho la Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2013.

Kikwete aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na kamati
inayokusanya maoni kuhusu uanzishwaji wa shirikisho hilo, Ikulu jijini
Dar es Salaam.

"Wazo la kwamba tuwaachie wananchi waamue kuhusu shirikisho, lilikuwa
ni wazo la Tanzania, wenzetu waliona tunapoteza wakati, waliona
viongozi wanaweza kuamua tu kuwapo kwa shirikisho. Nawashangaa sana
wale wanaosema eti tumekosea kuwashirikisha wananchi," taarifa
iliyotolewa na Ikulu jana ilimnukuu Rais Kikwete akisema.

Aliiambia kamati hiyo kuwa, baada ya tume iliyokuwa ikiongozwa na
Mwanasheria wa Kenya, Amos Wako kuhusu shirikisho kuja na 'road map',
"sisi Tanzania tulisema ngoja tuwashirikishe wananchi ili tupate
uhakika kwamba wananchi wanaridhika kuwa na shirikisho au la."

Aidha, katika kile kinachoonyesha kuwa kuna nchi wanachama wanalitaka
shirikisho kwa udi na uvumba, Rais Kikwete aliwaeleza wajumbe wa
kamati hiyo kuwa, kuna nchi moja (hakuitaja) ilifikia hatua ya kuandaa
rasimu ya muundo wa shirikisho bila kuzishirikisha nchi nyingine,
achilia mbali wananchi.

"Tulipogundua hili, Rais Mkapa alinituma mimi, wakati huo nikiwa
Waziri wa Mambo ya Nje, kwenda Kenya na Uganda, tukawaeleza wenzetu
jamani hapana, hivi sivyo tunavyotakiwa kwenda, tukawapa somo,
hatimaye wenzetu wakatuelewa. Lakini wenzetu waliona kuwaachia
wananchi waamue ni kama vile viongozi tunajivua madaraka," alisema.

Akionyesha kuwa uamuzi wa kuwashirikisha wananchi hauna lengo la kuwa
ghiliba, Kikwete alisisitiza kuwa, maoni yatakayotolewa na wananchi
yataheshimiwa, kuzingatiwa na kupewa umuhimu unaostahili.

Akizungumzia kuhusu nafasi ya Zanzibar katika shirikisho, alisema
hakuna maslahi ya nchi kama nchi, na kwamba jambo la msingi la
kujadili ni namna ya kuisaidia Zanzibar kukuza sekta yake ya
uzalishaji ili iwe na bidhaa za kuuza katika soko la Afrika
Mashariki.

"Muundo wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki si sawa na ile
iliyovunjika ambayo angalau kulikuwa na maslahi kama nchi, hii ya sasa
inazungumzia zaidi soko. Tusipoteze muda kujadiliana nani atafaidika
vipi na namna gani. Tujadili namna gani tutaisaidia Zanzibar iwe na
viwanda, izalishe bidhaa," alisema.

Alisema suala la msingi la kujadili ni kuwa Tanzania inaingiaje katika
ushirikiano huo chini ya muundo wa muungano wake.

Kuhusu hofu ya wananchi wengi kupoteza ardhi na ajira, Kikwete alisema
masuala hayo hayatakuwa katika shirikisho, bali yatadhibitiwa na nchi
husika.

Rais Kikwete alitoa maelezo hayo licha ya majuzi kukataa kulizungumzia
suala hilo, alipoulizwa na wahariri akisema kwa kuwa suala hilo bado
lipo kwa wananchi, ni vema wakaachiwa watoe maoni yao kabla ya yeye
kulisemea.

Ili kuhakikisha kuwa kamati inakusanya maoni kutoka kwa watu wengi,
Rais Kikwete aliitaka kuhakikisha inakutana na watu wengi kadiri
inavyowezekana.

"Ningependa pale mtakapofika kwenye makundi kama vile vyama vya siasa,
hakikisheni kwamba mnawapata wanachama wengi wa vyama hivyo, badala ya
kukutana na viongozi peke yao," alisema na kubainisha kuwa, lengo liwe
ni kupata mawazo mchanganyiko.

Akitoa ripoti ya kamati hiyo, mwenyekiti wake, Profesa Samuel Wangwe,
alisema kazi imekwenda vizuri, ingawa kuna changamoto kubwa kutokana
na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu suala zima la Jumuiya ya Afrika
Mashariki.

Alisema uelewa mdogo, ambao umeonyeshwa hata na wasomi, umeifanya
kamati hiyo kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja; kuwaelimisha wananchi
na kisha kukusanya maoni na kusababisha ionekane kana kwamba inafanya
kazi ambayo si yake.

Utetezi huo wa rais unakuja wakati makundi ya wanasiasa na wanasheria
yakionyesha waziwazi kutofautiana na mchakato huo, na kupinga kitendo
cha Rais Kikwete kuruhusu hoja ya kuundwa kwa Shirikisho la Afrika
Mashariki.

Wengine wamefikia hatua ya kuhoji uhalali wa kikatiba uliompa nguvu
Rais Kikwete kuteua tume ya kukusanya maoni kuhusu suala ambalo
hatimaye litasababisha kufa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Source:Mtanzania Daima

Reply all
Reply to author
Forward
0 new messages