Ben Komba/Pwani/11/20/2009 7:02 PM
Mkazi wa Bwawani , Bagamoyo mkoani Pwani, BW. MJANAEL ALLY amefariki dunia baada ya kupigwa na fimbo kichwani na BW.CHARLES NYANGA katika kile kinachosemekana wivu mkali.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Bw. Mohamed Mbwana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amesema tukio hilo limetokea Nov 17.
Amesema marehemu na mtuhumiwa walikuwa na urafiki wa kimapenzi na mwanamke mmoja, ambapo kamanda hakumtaja jina lake, hali ambayo ilikuwa ikimsononesha mtuhumiwa na mpaka akaamua kuchukua hatua ya kumshambulia marehemu kwa fimbo kichwani.
Kaimu Kamanda MBWANA amesema siku ya tukio mtuhumiwa alimwendea marehemu na kuanza kumshambulia, na kumfanya marehemu kuumia vibaya mpaka kiasi cha kukimbizwa zahanati ambapo alipatiwa huduma ya kwanza na kuruhusiwa, lakini hata hivyo usiku huohuo akafariki dunia.
Kamanda ameongeza mwili wa marehemu tayari umeshakabidhiwa kwa ndugu zake baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu kuelewa nini hasa kimemuua, na huku Jeshi la Polisi likiendelea na msako mkali kufuatia kutoroka kwa mtuhumiwa huyo.
END